**********************************
Na John Walter-Manyara
Siku 16 za Kupinga Ukatili wa kijinsia, Mkuu wa kitengo cha Jinsia mkoa wa Manyara Mkaguzi msaidizi wa jeshi la polisi Pili Saburi amesema wamepanga kufanya maadhimisho hayo Yaeda Chini wilayani Mbulu ambapo kumekuwa na vitendo vingi vya kikatili.
Amesema wameamua kuingia zaidi vijijini ambapo hapafikiki kirahisi kutoa elimu kwa wananchi wanaoishi maeneo hayo badala ya Mijini palipozoeleka mara nyingi ili nao wapate uelewa na muamko wa kutumia kituo cha polisi kilichofunguliwa katika eneo hilo kuripoti vitendo vya Ukatili.
Ameeleza wanatumia maadhimisho hayo kufikisha elimu kwa jamii, wanafunzi mashuleni, majukwaa mbalimbali, nyumba za ibada na kupitia njia ya redio za kijamii zilizopo mkoani Manyara.
Amesema maadhimisho hayo yamekuwa na matokeo mazuri ambapo wamezidi kupokea wateja wapya ambao wengi wao wanadai walikuwa hawafahamu kwamba vitendo vya Ukatili wa Kijinsia ni jinai, walikuwa wanadhani ni sawa Kukeketa, Vipigo ndani ya ndoa wakidhani ni utamaduni.
Wapo watu ambao wameelewa na kuguswa na kueleza kuwa hata vijana watazidi kueneza elimu hiyo kwa wenzao ili waweze kukoma wale wenye tabia ya kufanya vitendo hivyo vya Ukatili” alisisitiza Pili.