***************************************
Mchezaji nyota wa zamani wa Argentina, Diego Armando Maradona amefariki dunia leo Novemba 25, 2020 akiwa na umri wa miaka 60.
Taarifa za kifo cha Gwiji huyo zimethibitishwa na Shirikisho la soka nchini Argentina kupitia kwa Rais wake Claudio Tapia.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka vyombo mbalimbali vya habari duniani, Maradona alifanyiwa upasuaji wa ubongo mapema mwezi huu huku madaktari wakithibitisha kuwa alifaulu upasuaji huo na huenda wangeanza kushughulikia tatizo lililokuwa likimsumbua la uraibu wa pombe.
Katika maisha yake ya soka Maradona amevitumikia vilabu mbalimbali duniani akiwa kama mchezaji na kocha baada ya kustaafu soka mwaka 1997 alipokuwa akiadhimisha siku ya kuzaliwa kwake (miaka 37) katika klabu ya Boca Juniors.
Mwaka 2008 aliteuliwa kuwa Kocha Mkuu wa Argentina lakini alibwaga manyanga baada ya kipigo cha mabao (4-0) dhidi ya Ujerumani kwenye mashindano ya Kombe la Dunia mwaka 2010 yaliyofanyika kwa mara ya kwanza barani Afrika (Afrika Kusini).
Hadi umauti unamkuta, Maradona alikuwa kocha wa Gimnasia y Esgrima inayoshiriki ligi kuu nchini Argentina baada ya kuachana na vilabu alivyopita katika mataifa ya Falme za Kiarabu pamoja na Mexico.