********************************
NA BALTAZAR MASHAKA, MWANZA
MAHAKAMA Kuu Mwanza itasikiliza na kutoa uamuzi wa majibu ya mapingamizi yaliyotolewa mjibu maombi ya kesi ya maombi ya mapitio namba 2 ya 2020.
Shauri hilo maombi ya mapitio lililofunguliwa na Bodi ya Wadhamini ya Msikiti wa Ijumaa dhidi ya Bodi ya Shule ya Thaqaafa lilosikilizwa na Jaji A.Z. Mgeyekwa wa Mahakama Kuu Mwanza,liliahirishwa jana hadi Disemba 8, mwaka huu.
Wakili wa wajibu maombi Wilbard Kilenzi, akiwasilisha pingamizi la kwanza aliiambia mahakama hiyo kuwa kiapo cha Abdallah Amin Abdallah,ni kibovu kwa sababu hana mamlaka ya kisheria kuapa kwa niaba ya Msikiti wa Ijumaa.
Kwenye pingamizi la pili wakili huyo alidai kiapo hicho cha mleta maombi kimeambatanishwa kwenye maombi ya mapitio bila ruhusa ya mahakama.
Wakili huyo katika pingamizi la tatu alidai kiapo hicho hakikufuata misingi ya kisheria na kuomba mahakama itupilie mbali maombi hayo ya waleta maombi.
Hata hivyo, Wakili wa waleta maombi Godfrey Samson wa LZone Allied Advocate anayesaidiana na Steven Henga, akijibu hoja hizo aliiomba mahakama kuyatupa mapingamizi ya wajibu maombi sababu hayakutastahili kuletwa kwa misingi ya kisheria.
Alisema katika hoja ya pingamizi la kwanza inahitaji ushahidi na haijakidhi kuwa pingamizi la kisheria,pia pingamizi la pili hakuna sheria inayotajwa kuvunjwa kama mapingamizi ya kisheria yanavyotaka.
Aidha wakili Samson alipinga hoja ya pingamizi la tatu kuwa haliko wazi ni kitu gani kinakosekana na kina athari gani.
“Pingamizi la pili, wakili amejielekeza kuwa Abdallah Amin ameapa bila kuthibitishwa kwenye kiapo na hakijataja kesi bali kinazungumzia jina la muapaji kuwa halijaandikwa na aliyeandaa ni mtu asiyeruhusiwa kisheria na hivyo kuvunja sheria ya mawakili na inavyodaiwa na wakili wa wajibu maombi,”alisema na kuongeza;
“Hakuna sheria inayozungumzia kiapo kuwa ushahidi ukiwekwa kwenye maombi lazima upate ruhusa ya mahakama hivyo tunaiomba mahakama mapingamizi hayo yaondolewe kwa gharama,”alisema wakili huyo.
Samson alifafanua kuwa mapingamizi hayo yameletwa yakiambatanishwa na kiapo si maombi ya mapitio hata yakikubaliwa hayataathiri maombi yao mahakamani hapo.kwamba wakili wa wajibu maombi alijielekeza
Kutokana na hoja za pande hizo mbili Jaji Mgeyekwa aliahirisha shauri hilo hadi Disemba 8,mwaka huu, mahakama hiyo itakaposikiliza mapingamizi ya wajibu maombi na kutoa uamuzi.