wa Shule ya Sekondari ya Munkinya wakisikiliza mafunzo ya ukatili wa kijinsia
yalikuwa yakiwasilishwa na watendaji wa SPRF (hawapo pichani)
wa Munkinya Sekondari wakiwasilisha mpango kazi wa utekelezaji majukumu yao
kuhusiana na vita iliyopo dhidi ya matukio ya ukatili wa kijinsia.
Wanafunzi
wa Shule ya Sekondari Siuyu wakifuatilia mafunzo hayo.
Kaimu Afisa Ustawi wa Jamii Wilaya ya Ikungi, Paul Mgelwa
akifuatilia mafunzo hayo, kulia ni wanafunzi wa Shule ya Sekondari Siuyu.
Mratibu wa Mradi kutoka SPRF, Mwalimu Bernard Maira
akizungumza na wanafunzi wa sekondari ya Siuyu (hawapo pichani)
Shule ya Sekondari Siuyu wakifuatilia mafunzo hayo.
Mratibu wa Mradi kutoka SPRF, Mwalimu Bernard Maira
akizungumza na wanafunzi wa sekondari ya Siuyu wakati wa mafunzo hayo.
Na Godwin Myovela, Singida
MATUKIO ya unyanyasaji wa kijinsia kwa wasichana wenye umri mdogo, ikiwemo mimba na ndoa za utotoni, vitendo vya ukeketaji na ubakaji yameendelea kupungua katika wilaya ya Ikungi mkoani hapa- huku sababu kubwa ikitajwa kuwa ni matokeo ya ushirikishaji wa makundi rika katika kupambana na vita hiyo ndani ya jamii, imeelezwa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika lisilo la Kiserikali la Stars of Poverty Rescue Foundation (SPRF) nchini, Dkt Suleiman Muttani, aliyasema hayo jana muda mfupi baada ya shirika hilo kutembelea na kufanya mijadala ya pamoja kwa kushirikisha shule za sekondari Munkinya na Siuyu zilizopo wilaya ya Ikungi, mkoani hapa.
“Tumeunda ‘Clubs’ za wanafunzi mashuleni ambao pamoja na mambo mengine tunawapa fursa ya kuchagua viongozi, tunawajengea uwezo na kuwasimamia kutengeneza mpango kazi ambao unawasaidia katika kuwawezesha kufichua na kupeana elimu ya matukio ya kutokomeza ukatili, mimba na ndoa za utotoni wao kwa wao,” alisema Muttani.
Afisa Ufuatiliaji na Tathmini wa shirika hilo, Mwedinuu Beleko, akiwasilisha mada kwa nyakati tofauti wakati akizungumza na wanafunzi wa shule hizo, aliitaka jamii kujitokeza haraka na kutoa taarifa yenye ushahidi pindi matukio ya ukatili yanapojitokeza ili kurahisisha mwenendo wa shauri.
“Nawaomba wanafunzi msiogope, wala msitishwe na mtu yeyote tukio lolote la ukatili linapojitokeza basi hakikisheni aliyefanyiwa ukatili huo anashiriki mara moja katika kutoa taarifa yenye ushahidi…na msipoteze huo ushahidi na vielelezo vyote ili kuharakisha mchakato wa kesi kuendelea kwa wakati,” alisema Beleko.
Kwa upande wake, Afisa Ustawi wa Jamii wilayani hapa, Paul Mgelwa aliwasihi wanafunzi kuwa makini na kutodanganyika ili kukabiliana na mimba zisizotarajiwa ambazo hufifisha ndoto na matarajio yao-na kusisitiza kuwa daima wanapaswa kuweka kipaumbele cha elimu kwanza kwa kuzingatia elimu ndio ukombozi wa maisha katika kupambana na umasikini.
Katibu wa Shirika hilo, Dkt Mwajuma Mikidadi alisema malengo ya SPRF, ambayo miradi yake ipo chini ya ufadhili wa Foundation for Civil Society (FCS), ni kukuza ushirikiano miongoni mwa wadau na jamii, taasisi za kitaifa na kimataifa katika kutokomeza umaskini wa kipato, sambamba na kuimarisha uwezo wa kitaasisi katika kukua na kutekeleza programu endelevu.
“SPRF na jamii ndio moto wetu kwa sasa, programu hii imesaidia kumfanya kila mwanafunzi wa kike kutambua haki zake, lakini madhara ya mila zilizopitwa na wakati na kandamizi, masuala ya ukeketaji na mimba na ndoa utotoni ndani ya jamii,” alisema Mikidadi
Mratibu wa mradi huo, Mwalimu Bernard Maira, alisema hata hivyo shirika hilo limefanikiwa kuanzisha Kamati za MTAKUWWA kwenye vijiji 8 zinazopinga Ukatili wa Kijinsia dhidi ya Wanawake na Watoto huku wakihamasisha uanzishwaji wa vikundi mathalani Sauti ya Mwanamke na Sauti ya Mwanafunzi, ambavyo vimekuwa chachu ya mageuzi ya kifikra dhidi ya mila potofu na masuala ya ukatili ndani ya jamii zao.