*****************************************
Na. Angela Msimbira OR-TAMISEMI
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Mjaliwa (Mb) ametoa siku 15 kwa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino, Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) na Suma JKT kuhakikisha ujenzi wa Hospitali ya Uhuru unakamilika ifikapo disemba 5, 2020.
Akikagua maendeleo ya ujenzi wa Hospitali hiyo leo Jijini Dodoma Mhe. Majaliwa amesema Hospitali ya Uhuru ni moja kati ya miradi ya kimkakati ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kuimarisha utoaji huduma katika Sekta ya afya ambayo inaanzia kuboresha kuanzia ngazi ya zahanati, vituo vya Afya, Hospitali za Wilaya, Hospitali za Rufaa na Hospitali za Magonjwa makubwa.
Anaendelea kufafanua kuwa Serikali imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha inaboresha huduma za afya kwa lengo la kutoa huduma bora kwa wananchi, hivyo imejikita katika kuhakikisha miradi yote ya kimakakati inakamilika kwa wakati ili ianze kutumika
“ Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino, Wakala wa majengo (TBA), Suma JKT, hakikisheni ujenzi wa Hospitali hii unakamilika kwa wakati, fanyeni kazi usiku na mchana, jengeni vibanda na kuhamia kwenye eneo la ujenzi, ongezeni wafanyakazi ili kukamilisha ujenzi kwa wakati uliopangwa” amesisitiza Mhe. Majaliwa
Mhe. Majaliwa amesema miradi ya Kimakakati inatakiwa ikamilike kwa wakati na Watanzania wanahamu ya kuona miradi inakamilika na kuanza kutoa huduma hivyo fanyeni kazi kwa weledi ili kuweza kukamilisha ujenzi wa Hospitali hiyo muhimu kwa jamii
Akitoa taarifa ya maendeleo ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Chamwino, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhandisi Joseph Nyamhanga amesema ujenzi wa Hospitali ya Uhuru imekadiriwa kutumia zaidi ya shilingi bilioni 3.995 na kiasi kilichotengwa ni shilingi bilioni 3.410 ambapo zaidi ya shilingi milioni 995 zilikuwa ni fedha za maadhimisho ya siku ya uhuru wa Tanganyika na shilingi bilioni 2.415 ni gawio la kampuni ya simu ya Airtel.
Naye Msaidizi wa Mkuu wa JKT Colonel Laurence Angelo Lupenge amesema mradi wa ujenzi wa Hospitali ya Uhuru umefikia asilimia 92 na kazi zilizofanyika ni kusafisha eneo la mradi,kuchimba na kujenga msingi, kujenga “frame” ya jengo pamoja na kuta, kupiga “plaster” kuta pamoja na” skimming”, kuweka njia za mifumo ya umeme,kupaua na kufunga gypsum board,kuchimba mashimo ya maji taka na kuweka “rough floor” kwa ajili ya kuweka vigae