Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Kusaya akiwa ameshika mche bora wa kahawa wakati alipotembelea kikundi cha wakulima wazalishaji miche ya kahawa ” SHABADI” kijiji cha Biatika kata ya Buhemba wilaya ya Butiama leo. Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa Kahawa (TACRI) Dkt. Deusdedit Kilambo. Kikundi hicho cha wakulima kimepewa kazi ya kuzalisha miche 500,000 ya kahawa na kuiuza kwa wakulima chini ya usimamizi wa TACRI ili kufufua zao la kahawa mkoani Mara.
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Kusaya ( kulia) akisaini kitabu cha wageni wakati alipotembelea kukagua shamba la kahawa na migomba la mkulima Mama Hellena Mtika wa kijiji cha Kinyariri wilaya ya Butiama leo. Shamba hilo linatumika kama darasa kwa wakulima kufundishwa kilimo bora cha kahawa na migomba chini ya usimamizi wa TACRI. Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya ( katikati) akikagua shamba darasa la alizeti akiwa na Mkuu wa Wilaya ya Butiama Mhe. Anna Rose Nyamubi ( kushoto) na kulia ni Katibu Tawala Mkoa wa Mara Bi. Karoline Muthapula leo wakati alipotembelea kukagua kituo maalum cha Mafunzo Wakulima cha Mama Maria Nyerere kilichopo Butiama. Kituo hicho kimeanzishwa ili kuwa eneo maalum la taasisi za umma na binafsi kuweka mashamba darasa ya mfano ya kufundisha kanuni bora za kilimo ikiwemo teknolojia za uzalishaji mazao. Lengo la mkoa wa Mara ni kuwa na viwanja hiyvo kutumika kama ilivyo viwanja vya Nane nane.
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Kusaya akizungumza na Katibu Tawala Mkoa wa Mara Bi. Karoline Muthapula (kushoto) mara baada ya kukagua eneo la ekari 3 zilizotengwa kwa ajili ya wizara ya kilimo na taasisi zake kuanzisha mashamba darasa kwenye viwanja vya Mama Maria Nyerere Butiama. Akiwa katika eneo hilo Kusaya ameagiza Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Mbegu (ASA) Dkt. Sophia Kashenge kwenda Butiama na kuanzisha shamba darasa la kufundishia wakulima ubora wa mbegu zinazozalishwa ili kujenga imani ya ubora na pia kuvutia masoko. Aidha, ameagiza taasisi ya utafiti TARI kwenda haraka Butiama na kuanzisha shamba darasa la mbegu za mihogo ikiwemo kufundisha matokeo ya utafiti wa visumbufu vya mihogo.
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Kusaya ( kushoto) akitazama samaki wanaofugwa kwenye vizimba alipotembelea mradi wa kufuga samaki kwenye vizimba Rwamkoma JKT katika bwawa la Kyrarano wilaya ya Butiama. Uongozi wa wilaya ya Butiama umeomba wizara ya Kilimo usaidie kufufua skimu ya umwagiliaji katika eneo hilo ili wakulima wazalishe mazao kama ambavyo Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alikusudia kwa kujenga bwawa hilo.
( Habari na picha na Wizara ya Kilimo)
**************************************
Serikali imeupongeza uongozi wa mkoa wa Mara kwa mkakati wake wa kufufua zao la kahawa sambamba na mazao ya pamba na mkonge ili kuwa na uhakika wa kipato kwa wakulima wake.
Pongezi hizo zimetolewa leo ( 20.11.2020) na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya aliyetembelea kituo maalum cha mafunzo ya wakulima kwenye viwanja vya maonesho vya Mama Maria Nyerere wilayani Butiama .
” Naupongeza sana uongozi wa mkoa wa Mara kwa jitihada zake za kufufua mazao ya kimkakati ikiwemo kahawa,pamba na mkonge kwani yana mchango mkubwa katika kumaliza umasikini wa wananchi wetu” alisema Kusaya.
Akiwa Butiama Kusaya alipokea taarifa ya wilaya iliyotolewa na Mkuu wa Wilaya hiyo Anna Rose Nyamubi aliyesema wamepanga kuongeza uzalishaji wa zao la kahawa kwa kupanda miche 340,000 ili baada ya miaka mitatu wawe na uwezo wa kuvuna tani 1000 za kahawa kutokana na hali ya hewa nzuri na utayari wa wakulima.
Mkuu huyo wa wilaya ya Butiama aliongeza kusema kupitia kituo cha maonesho ya kilimo ya Mama Maria Nyerere taasisi za umma na binafsi zimeweka mashamba darasa maalum kufundisha wakulima namna sahihi ya kuzalisha mazao ya biashara ikiwemo kahawa, pamba, mkonge ,korosho na mazao ya chakula na mboga mboga.
Mkakati wa mkoa wa Mara ifikapo mwaka 2023 waongeze uzalishaji kahawa toka tani 1,800 za sasa hadi kufikia tani 15,000 kupitia uhamasishaji wakulima kuanzisha na kufufua mashamba .
” Butiama tulipaswa kuwa juu kwenye mafanikio ya kilimo kutokana na hali ya hewa nzuri,hivyo tunaomba wizara ya kilimo ishirikane nasi kuhamasisha upatikanaji wa mbegu bora za mazao na pia kufufua skimu za umwagiliaji ” alisema Mkuu huyo wa wilaya.
Akijibu maombi hayo Katibu Mkuu Kusaya alisema kupitia taasisi za utafiti wa zao la kahawa (TACRI) taasisi ya utafiti wa kilimo (TARI) na Wakala wa Mbegu (ASA) atahakikisha wanafika mkoani Mara mapema kutoa elimu ,kuzalisha mbegu na kutoa matokeo ya tafiti za kusaidia mkulima kuinua tija na uzalishaji wa mazao.
Kusaya alitembelea wakulima wa vijiji vya Kinyariri na Biatika wilaya ya Butiama kukagua mashamba ya kahawa na vitalu vya miche na kujionea uhitaji mkubwa wa miche ambapo ametoa agizo kwa TACRI kuhakiksha inazalisha kwa wingi miche bora ya kahawa na kuigawa kwa wakulima.
” Ni vibaya kuona wakulima wanahitaji miche ya kahawa halafu tuanyo taasisi inashindwa kufikisha huduma hiyo kwa wakulima. Nataka kuona jitihada za TACRI kuzalisha na kusambaza miche bora ya kahawa kwa wakulima wa Mara haraka” aliagiza Kusaya.
Katika hatua nyingine Kusaya ameagiza Wakala wa Mbegu( ASA) kupeleka mbegu bora za mahindi na mazao mengine mkoani Mara na kuuza za bei ya shilingi 5,500 kwa mfuko wa kilo mbili ili wakulima wapande msimu huu wa mvua.
Katika kuhakikisha mkoa wa Mara unafanikiwa kufufua mazao ya kimkakati Kusaya ameagiza wataalam wa mkoa kupanga maeneo maalum ya kuzalisha mazao ya biashara badala ya ilivyo sasa kulima kila eneo au wilaya hali inayosababisha ugumu kwa wataalam kuwafika wakulima.
” Tusiwaache wakulima walime kilimo cha mazoea, tuwashauri kitaalam na kuweka kanda ili wanufaike na utaalam na kuwa tuwashauri wapime afya ya udongo kabla ya kulima ili wajue aina ya mazao na mbolea ya kutumia kwa lengo la kuwa na uhakika wa uzalishaji” alisema Kusaya.
Wizara ya Kilimo kupitia Kituo cha Utafiti wa kilimo (TARI) Selian cha Arusha tayari wamekusanya sampili 30,400 za udongo kutoka mikoa 18 ya Tanzania kwa lengo la kupima afya yake na kutengeneza ramani itakayosaidia wakulima na wawekezaji kujua tabia za udongo kabla ya kuamua kuanza uzalishaji wa mazao.
Katibu Mkuu Kusaya alitaja faida za kujua tabia ya udongo ni kumwezesha mkulima kuachana na kilimo cha mazaoe badala yake alime kisayansi na kuweza kupata mavuno mengi na bora hatua itakayosaidia kuwa na uhakika wa masoko.