Waandaji wa mkutano huo wakiwa katika picha ya pamoja na Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Tiba wa Wizara ya Afya, Dkt. James Kihologwe.
……………………………………….
Na Sophia Mtakasimba
Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ikishirikiana na wadau wa afya Novo Nordisk Haemophilia Foundation (NNHF) , Novo Nordisk foundation (NNF) na Kenya Haemophilia association (KHA), leo imezindua mradi utasaidia upatikanaji wa haraka na ukaribu wa huduma , vipimo na matibabu kwa wagonjwa wa Haemophilia na Selimundu.
Akizindua Mradi huo wa miaka mitatu kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Serikari, Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Tiba kutoka Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. James Kihologwe amesema kwa mradi huo utatekelezwa kwa ushirikiano kati ya nchi ya Tanzania na Kenya.
“Lengo kuu la mradi huu ni kuwezesha upatikanaji wa vipimo vya magonjwa haya katika hospitali zote za rufaa nchini , upatikanaji wa wataalamu wa afya waliobobea kwenye magonjwa haya pamoja na upatikanaji wa miundombinu sahihi kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa hawa,” amesema Dkt. Kihologwe
Dkt. Kihologwe amesema kuwa mradi utasaidia uanzishwaji wa Klinic za Haemophilia na Selimundu kwenye hospitali zote za rufaa pamoja na kutoa mafunzo elekezi kutoka kwa wataalamu wabobeza wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, utaziwezesha hospitali za rufaa kuanzisha na kutoa huduma za mazoezi tiba kwa wagonjwa (Physiotherapy) Pamoja na vipimo maalumu vya kugundua magonjwa haya mapema.
Amesema kuwa ugonjwa wa Selimundu tayari umeshafanyiwa tafiti mbalimbali ambazo zimesaidia uboreshaji wa huduma kwa wagonjwa na kuwezesha kuwepo kwa mwongozo wa kitaifa wa utoaji wa huduma kwa wagonjwa na pia umewekwa kwenye mpango mkakati wa kitaifa wa magonjwa yasiyoambukiza.
Dkt. kihologwe amesema Tanzania inasadia kuwa na wagonjwa wa haemophilia kati ya 6000 hadi 12000 nchini, lakini wanaofahamika na wanaoendelea na matibabu 167 tu.“Mradi huu utasaidia kuongeza kasi katika upatikanaji wa takwimu za ugonjwa wa Hemophilia , utasidia kufanyika tafiti za ugonjwa huu na pia utaharakisha uboreshaji wa huduma kwa wagonjwa hawa pamoja na kuweka ugonjwa wa Hemophilia katika Mpango mkakati wa magonjwa yasiyoambukiza (NDC) na hatimaye kuwa na mwongozo wa utoaji huduma (National Treatment Guadline ) kwa ugonjwa huu katika Hospitali zote nchini” amesema Dkt kihologwe
Naye, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya damu Hospitali ya Taifa Muhimbili ambaye pia ni mratibu wa mradi, Dkt. Stella Rwezaura amesema Haemophilia ni ugonjwa wa damu kukosa uwezo wa kuganda ambao unasababishwa ukosefu wa kiwango cha kutosha cha chembechembe za protini zinazotakiwa kugandisha damu na kusababisha damu kuvuja kwa muda mrefu.
Amesema kuwa asilimia 97 ya wagonjwa wa haemophilia hawajui kama wanaougonjwa huo na hawajawahi kupatiwa vipimo vyovyote ili kujua hali ya ugonjwa, hivyo wengi hujikuta wakihusisha ugonjwa huo na ushirikina.
Amewataka wananchi kufika hospitali mara moja pale wanapokuwa na viashiria vya kutokwa damu mfululizo kwa muda mrefu unapotokea mchubuko, kukatwa au kujikata.