****************************************
Na. Angela Msimbira OR-TAMISEMI
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhandisi Joseph Nyamhanga amewaagiza viongozi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa nchini kuhakikisha wanatoa elimu kwa watumishi wa umma na wananchi kwa ujumla kuhusu uwepo Kituo cha kutolea huduma kwa wateja kilichoanzishwa na Ofisi ya Rais- TAMISEMI.
Akiongea kwenye ziara iliyofanywa na waandishi wa habari katika Kituo hicho leo Mhandisi Nyamhanga amesema lengo la kuanzishwa kwake ni kuwaondolea adha watumishi wa umma na wananchi kwa ujumla kusafiri mpaka Makao Makuu Ofisi za Rais TAMISEMI kwa ajili ya kupata huduma
Amesema Ofisi ya Rais TAMISEMI inahudumia wateja mbalimbali ikizingatiwa kuwa ndio wasimamizi wa Mikoa 26, Wilaya139, Halmashauri 185, tarafa 570, kata 3956, vijiji 12,319, Mitaa 4,263, vitongoji 12,384 na zaidi ya watumishi asilimia 73 ya wanatoka katika Mamlaka za Serikali za Mitaa, hivyo ni vyema kituo cha kutolea huduma kwa wateja kilichoanzishwa kikatangazwa kuanzia ngazi za Mamlaka za Serikali za Mitaa
Amefafanua kuwa kujulikana kwa kituo hicho kutasaidia kupunguza mlundikano wa Watumishi wa Umma na wananchi kwa ujumla kusafiri umbali mrefu na kuja katika Ofisi ya Makao Makuu kufuata huhuma mbalimbali.
“Wateja wakiwemo watumishi wamekuwa wakisafiri umbali mrefu kuja kupata huduma Makao Makuu, Jambo ambalo lilikuwa likileta usumbufu mkubwa, lakini tangu kuanzishwa kwa kituo hiki kumesaidia kupunguza mlundikano wa wateja na kupunguza gharama kubwa, muda na usumbufu kwa wanananchi ambao walikuwa wanakuja kufuatilia masuala mbalimbali” Amesisitiza Mhandisi Nyamhanga.
Ametoa wito kwa wananchi wote wanaohitaji kupata huduma mbalimbali katika Ofisi ya Rais TAMISEMI kukitumia kituo cha kutolea huma kwa wateja ili kuweza kupata huduma stahiki na haraka na amewaagiza watumishi wote kuhakikisha wanakitangaza ili wananchi wakijue na kukitumia.
Akitoa taarifa ya mafanikio Msimamizi wa Kituo Bi. Antelma Mtemahanji amesema mpaka sasa wameweza kupokea simu 15,886, ambapo wateja waliosajiliwa ni 5571 na hoja zilizokamilika na kufungwa ni 5526 sawa na asilimia 99
Mtemahanji anafafanua kuwa kablaa ya kuanzisha kituo hicho Ofisi ya Rais TAMISEMI ilikuwa ikipokea takribani wageni 87 hadi 129 kwa siku lakini kwa sasa inapokea wageni kati ya 20 hadi 47 kwa siku kwa ajili ya kupata huduma mbalimbali.
Amesema kuwa katika kipindi cha miezi mitatu tangu kituo kuanza wateja zaidi ya 5571 wangefika Makao makuu kutoka maeneo mbalimbali ya nchi kufuata huduma hivyo kuanzishwa kwa kituo hiki kimesaidia kupunguza msongamano katika Ofisi ya Rais – TAMISEMI
Ametoa wito kwa wananchi na watumishi wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kukitumia kituo hiki ili kupata hudum kwa haraka na wakati
Aidha waandishi wa Habari mkoani Dodoma walifanya ziara ya siku moja katika Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa lengo la kufahamu mafanikio yaliyopatikana tangu kuanzishwa kwa kituo cha kutolea huduma kwa wateja mnamo tarehe 6/08/2020