Picha ya pamoja ya Naibu katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandisi Nadhifa Kemikimba na washiriki wa mafunzo ya mfumo wa pamoja wa kusimamia shughuli za Taasisi na huduma za ankara kwa Mamlaka za Maji Tanzania.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandisi Nadhifa Kemikimba akizungumza na washiriki wa mafunzo ya mfumo wa pamoja wa kusimamia shughuli za Taasisi na huduma za ankara kwa Mamlaka za Maji Tanzania. (hawapo Pichani)
Washiriki wa Mafunzo ya mfumo wa pamoja wa kusimamia shughuli za Taasisi na huduma za ankara kwa Mamlaka za Maji nchini wakimsikiliza Naibu Katibu Mkuu wakati wa kufunga mafunzo mjini Morogoro. (hayupo Pichani)
……………………………………………………………………………………………
Na Evaristy Masuha
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandisi Nadhifa Kemikimba amezitaka Mamlaka za Maji kote nchini kuhakikisha zinaanza kutumia mfumo wa pamoja wa kusimamia shughuli za Taasisi na huduma za ankara kwa Mamlaka za Maji.
Agizo hilo amelitoa leo wakati akifunga mafunzo ya wiki moja yaliyofanyika mjini Morogoro yakiwahusisha Maafisa TEHAMA na wadau wengine wa Mamlaka za Maji nchini ambao wanatumia mifumo hiyo. Amesema kumekuwepo na mapungufu mengi kwa baadhi ya taasisi za Wizara hasa Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira za Miji Midogo, Miji Mikuu ya Wilaya, Miradi ya Kitaifa, Ofisi za Bodi za Maji nchini pamoja na Maabara za Maji kutokuwa na Mifumo ya TEHAMA kwa ajili ya kukusanya mapato kinyume na Miongozo ya utekelezaji wa Bajeti za Serikali.
Amesema hata zile ambazo zimekuwa na mifumo ya TEHAMA zimekuwa na changamoto ya gharama za uendeshaji huku baadhi ya mifumo ikiwa inamilikiwa na wakandarasi au ikiwa chini ya wataalamu washauri.
“Pamoja na jitihada za Serikali, Taasisi zetu bado zina Mifumo ya TEHAMA ambayo uendeshaji wake ni gharama kubwa na umiliki wake upo nje ya taasisi hizo na hata nje ya nchi. Aidha, kila taasisi hutumia mifumo hiyo kwa gharama tofauti tofauti hata pale ambapo mifumo ni ya aina moja. Mfano mzuri ni Billing Systems zilizopo kwenye Mamlaka za Maji nchini ambapo pia mifumo hii kwa asilimia kubwa inamilikiwa na Wakandarasi au Wataalamu Washauri.
Amesema hali hii imekuwa ikipunguza ufanisi wa kazi, na kuruhusu udanganyifu katika baadhi ya maeneo hali ambayo imewasukuma wizara kutengeneza mfumo ambao utaondoa changamoto hizo.
Amesema mfumo huu ambao umetengenezwa na Wizara kwa kushirikiana na wataalamu wa Wakala wa Serikali Mtandao (e-GA) umelenga kuondoa changamoto hiyo ambapo sasa mifumo yote inakuwa imeunganishwa katika mawasiliano ya pamoja.
“Kwa muktadha huo, mnaporejea katika vituo vya kazi, naagiza kila mshiriki ahakikishe anawafundisha watumiaji wengine kwenye Taasisi yake, ahakikishe anahakiki idadi halisi ya Wateja kwenye mamlaka yake. Hili lianze hata kwa Mamlaka ambazo hazijapata mafunzo haya.
Pia hakikisheni mnafanya uhakiki wa Taarifa zote za Wateja zinazowekwa kwenye Mfumo huu mpya wa Serikali.” Amesema Kemikimba huku akizitaka Mamlaka za Miji Mikuu ya Wilaya na Miradi ya Kitaifa (Districts/Township WSSAs & National Projects) waliopata mafunzo waanze kuutumia Mfumo mara moja kwa sababu wengi hawana mfumo na wengine wanatumia mifumo inayosimamiwa na Wakandarasi/Wataalamu Washauri.
Kwa upande wa Mamlaka za Miji Mikuu ya Mikoa waliopata mafunzo amewapa siku zisizozidi 60 ili waanze kufanya majaribio na maandalizi mengine kwa kushirikiana kwa karibu na Wizara/EGA ili ndani ya siku 60 wawe wamekamilisha taratibu za Kuhamia kwenye Mfumo wa Serikali.
Akizungumzia utendaji wa mifumo hiyo mtaalamu wa TEHAMA kutoka Wakala wa Serikali Mtandao Leward Maligila amesema mfumo huo umeondoa changamoto nyingi na kwamba uatapunguza kwa kiasi kikubwa gharama na kurahisisha matumizi.
Ametaja baadhi ya huduma zilizounganishwa kwenye mfumo huo kuwa ni pamoja na ujumbe wa maandishi, barua pepe, Mfumo wa vitambulisho vya Taifa (NIDA), GPG na mifumo mingine ya serikali, hivyo wananchi wategemee huduma za haraka na zenye ufanisi.
Amesema zoei la mafunzo kwa watalaamu litaendelea kwa awamu ili kuhakikisha kila mdau anafikiwa na elimu hii.