Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma Mustafa Bora kulia na mdau wa maendeleo Alhaji Saleh Ahmed kushoto, wakimtwisha ndoo ya maji mkazi wa kijiji cha Nandembo Hadija Baina katikati mara baada ya kufungua rasmi visima viwili vya maji kati ya kumi vilivyochimbwa na Alhaji Saleh kwa ajili ya wananchi wa kijiji hicho waliokuwa wanakabiliwa na kero kubwa ya maji safi na salama.
Picha na Mpiga Picha Wetu
…………………………………………………………………………………
Na Mwandishi Maalum Tunduru
WANANCHI wa kijiji cha Nangunguru kata ya Nandembo wilayani Tunduru, wanakabiliwa na huduma ya maji safi na salama kwa muda mrefu hivyo kulazimika kutembea zaidi ya masaa mawili kwenda kutafuta maji katika vyanzo ya asili.
Wamesema, kwa sasa wanalazimika kutumia maji ambayo sio safi na salama kutoka katika vyanzo vichache pamoja na wanyama wakiwemo wanyama pori jambo ambalo ni hatari kwa usalama wao.
Wakizungumza kwa nyakati tofauri jana wananchi hao wamesema, ukosefu wa maji safi na salama kwa ajili ya matumizi ya kila siku ni kero ya muda mrefu na hivyo kuathiri ushiriki wao katika shughuli mbalimbali za maendeleo kama ilivyo katika maeneo mengine ya wilaya hiyo.
Hadija Baina alisema, katika kijiji hicho kuna kisima kimoja kilichojengwa na mfuko wa maendeleo ya jamii Tasaf,lakini kisima hicho kiliharibika miaka saba iliyopita na hivyo wananchi kuendelea kuteseka kwa kukosa huduma hiyo.
Abuu Kundoja, ameiomba Serikali kupitia wakala wa maji vijijini Ruwasa kuangalia uwezekano wa kumaliza tatizo hilo ili wananchi hao wapate maji safi na salama kwa matumizi yao ya kila siku jambo litakalochochea na kuhamasisha wananchi kushiriki vema katika shughuli zao za maendeleo.
Mdau wa maendeleo Alhaji Saleh Ahmed amesikia kilio cha wananchi hao na kuamua kuchimba visima viwili ili kupunguza changamoto ya manji inayowakabili wananchi wa kijiji hicho.
Alhaji Saleh amesema, mpaka sasa amechimba visima kumi katika vijiji mbalimbali kwa lengo la kumaliza kero ya maji na kuwapunguzia wananchi muda mwingi wanaotumia kwenda kutafuta huduma ya maji mbalimbali na makazi yao.
Alisema, suala la maendeleo sio jukumu la serikali pekee yake bali kila mmoja ni lazima ashiriki vema na ameamua kuchimba visima vya maji ili kuunga mkono Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Dkt John Magufuri chini ya kauli mbiu ya kumtua mama ndoo kichwani.
Alisema, ameamua kuchimba visima vya maji kwa gharama zake ili kuendeleza uhusiano na Serikali pamoja na jamii ya wana Tunduru ambapo aliongeza hadi sasa visima vyote vimekamilika na vinatoa maji.
Kwa mujibu wake,visima hivyo vimechimbwa katika maeneo ambayo wananchi wote bila kujali imani zao watafika kwa urahisi na kupata maji ikiwemo misikitini ili kutoa nafasi kwa waumini kushiriki katika vema katika ibada zao.
Aidha,amewataka wananchi waliofikiwa na visima hivyo kuhakikisha wanavitunza na wanatumia maji kama chachu ya kushiriki kazi za kujiletea maendeleo na kuinua hali zao za maisha.
Kwa upande wake,mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi wilaya ya Tunduru Mustafa Bora amesema kitendo alichokifanya Alhaji Saleh ni utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya chama cha mapinduzi yenye lengo la kutua mama ndoo kichwani.
Amewataka wananchi kuhakikisha wanatunza visima hivyo ili viweze kudumu kwa muda mrefu na vifanye kazi iliyokusudiwa ya kumaliza kero ya maji ambayo ilikuwepo katika kijiji hicho kwa muda mrefu.