***************************************
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amezungumzia vipaumbele vya Serikali ya wamu ya tano kwenye huduma za jamii (Elimu na Afya) vinavyogusa moja kwa moja ofisi ya Rais-Tamisemi wakati akifungua Bunge la 12.
“Tunakusudia kuendelea kuboresha huduma za jamii, hususan afya na elimu. Kuhusu AFYA kama unavyofahamu kwenye miaka mitano iliyopita tumepata mafanikio makubwa, ikiwemo kujenga vituo vya kutolea huduma za Afya 1,887 (Zahanati 1,198, Vituo vya Afya 487, Hospitali za Wilaya 99, Hospital za Rufaa za Mikoa 10 na Hospitali za Rufaa za Kanda 3.
Vilevile tumepunguza vifo vya akinamama wajawazito kutoka wastani wa vifo 11,000 kwa mwaka 2015 hadi kufikia wastani wa 3,000 hivi sasa. Kwa msingi huo kwa miaka mitano ijayo tunakusudia kuendeleza ujenzi wa miundombinu ya kutolea huduma za Afya, hususan zahanati, vituo vya Afya na Hospitali za Wilaya kwenye maeneo ambako hazipo.
Tutaimarisha pia upatikanaji wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi na kuongeza watumishi wa afya pamoja na kuimarisha mifuko yetu ya Bima ya Afya ili kufikia lengo la kuwawezesha wananchi wote kupata Bima ya Afya.
Kwenye ELIMU tutaendelea kutoa elimu ya Msingi na Sekondari bila Malipo na tutaendelea kujenga na kukarabati miundombinu ya Elimu, ikiwemo shule, madarasa, mabweni, maabara, ofisi na nyumba za walimu, hosteli pamoja na kumbi za mihadhara.
Tutahakikisha tunaendelea kuboresha elimu inayotolewa ili iweze kutoa maarifa na ujuzi wa kutosha kwa Wahitimu. Tutahimiza ufundishaji wa masomo ya sayansi na hisabati hususani kwa wanafunzi wa kike ambapo tunakusudia kujenga shule moja ya Sekondari kwa kila Mkoa kwa ajili ya kufundisha masomo ya Sayansi kwa Wasichana” Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.