MABINGWA wa Tanzania, Simba SC watamenyana na Plateau United ya Nigeria katika Raundi ya Awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Mechi za kwanza zitachezwa kati ya Novemba 27 na 29 na marudiano Desemba 4 hadi 6 mwaka huu, Wekundu wa Msimbazi wakianzia ugenini.
Nao mabingwa wa Zanzibar, Mlandege SC wataanzia nyumbani dhidi ya mabingwa wa zamani wa michuano hiyo, CS Sfaxien ya Tunisia.
Mshindi baina ya Simba SC na Plateau United atamenyana na mshindi kati ya Costa do Sol ya Msumbiji na FC Platinum ya Zimbabwe kuwania kuingia hatua ya 16 Bora inayochezwa kwa mtindo wa makundi.
Na mshindi kati ya Mlandege SC na CS Sfaxien atamenyana na mshindi kati ya Buffles FC ya Benin na MC Alger ya Algeria.
Katika Kombe la Shirikisho Raundi ya Awali, wawakilishi wa Tanzania Bara, Namungo FC ya Ruangwa mkoani Lindi itamenyana na Al Rabita FC ya Sudan Kusini, wakati KVZ FC ya Zanzibar itamenyana na El Amal ya Sudan – mechi za kwanza zitachezwa kati ya Novemba 27 na 29 na marudiano Desemba 4 hadi 6 mwaka huu.
Mshindi kati ya Namungo FC na Al Rabita FC atamenyana na El HIlal Obeid ya Sudan, wakati mshindi kati ya KVZ na El Amal atamenyana na mshindi kati ya Ashanti Gold ya Ghana na Salitas FC ya Burkina Faso – mechi za kwanza zikichezwa kati ya Desemba 22 na 23 na marudiano kati ya Januari 5 na 6.