………………………………………………………………………………………..
Na Alex Sonna,Dodoma
Mbunge Mteule wa Jimbo la Nyasa, Mhandisi Stella Manyanya amewashukuru wananchi wa jimbo hilo kwa kuendelea kumuamini huku akitaja vipaumbele atakavyoanza navyo ikiwemo kutatua tatizo la maji.
Akizungumza mara baada ya kukamilisha usajili kwa ajili ya kuhudhuria Mkutano wa kwanza wa Bunge la 12, Mhandisi Manyanya amesema uchaguzi umekwisha sasa kazi imeanza na tayari ameanza.
Ameeleza kuwa kuna maeneo wakati wa uchaguzi alikutana na changamoto ambazo tayari ameanza kuzifanyia kazi.
“Pamoja na changamoto zilizokuwepo kwa kiasi kikubwa utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM ilikuwa imefanyika kwa kiwango kikubwa sana kiasi cha kutoa imani kwa wananchi na kila kijiji nilichotembelea na kimsingi nilitembelea vyote wakati wa kampeni kila kata kulikuwa na mambo ambayo wananchi walikuwa wanahitaji endapo nitavuka niyafanyie kazi, yote yameratibiwa vizuri,”amesema.
Aidha, amesema ilani ya uchaguzi ndio mwongozo mkuu na katika jimbo lake barabara ya Mbinga hadi Mbambay inaendelea kukamilisha na wanategemea kupata barabara ya lami mbambay hadi Litui na Litui hadi Kitai.
“Vilevile tunategemea kupata daraja la mto Ruvuma pia tunategemea kufanya upembuzi yakinifu kwa barabara ya kuanzia Nangombo hafi Chiwindi na alipokuja Makamu wa Rais, tuliomba na tuna imani tutakubaliwa kufanya upembuzi yakinifu barabara kutoka Nyoni-Tingi hadi Mitomoni,”amesema.
Pia amesema usambazaji wa umeme unakwenda kwa kasi na awamu hii vijiji vyote 84 vitapatiwa na hayo ni mambo ambayo yalikuwa kikwazo kwao.
Hata hivyo amesema kikwazo ambacho ni kikubwa ni tatizo kubwa la maji na litakuwa ni kipaumbele kwake kushughulikia.
“Kina mama kwasasa wanafanya shughuli mbalimbali kwa hiyo ule muda ambao wanautumia kufuata maji mbali na kurudi muda umekuwa hautoshi kina mama na kina baba wamekuwa wachapakazi sana, anaporudi jioni anajikuta hana maji kufuata kule alikokuwa anafuata hawezi ndio maana kilio cha maji ni kikubwa,”amesema.
Amebainisha kuwa kasi ya maendeleo na matumizi ya vyoo bora imeongezeka na kuhitaji maji, atahakikisha anafanya jitihada zote kutatua.
Manyanya amesema ujenzi wa viwanda, uvuvi vitaendelezwa kwa kuwa miundombinu imewekwa na wananchi wanashukuru na wanatarajia makubwa miaka mitano ijayo.
“Namshukuru sana Mungu kwa kurejea bungeni kwa kipindi hiki cha pili cha ubunge wa jimbo, nawashukuru wananchi wa Nyasa kwa kuendelea kuniamini, nawashukuru pia akina mama kwa kuniunga mkono kwa nguvu kubwa kabisa,”amesema.
Pia amempongeza Rais Dk.John Magufuli kwa ushindi wa kishindo na kupata kura kwa asilimia 90 katika jimbo hilo.