Rais wa shirikisho la wachimba madini nchini (Femata) John Bina akizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni.
Rais wa shirikisho la wachimba madini nchini (Femata) John Bina akizungumza na wadau wa madini ya Tanzanite Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, hivi karibuni.
***************
RAIS wa shirikisho la wachimbaji madini nchini (Femata) John Bina amelaani vikali tukio la utoroshwaji wa madini ya Tanzanite, Ruby na Green Tourmarine, lililotokea Wilayani Longido Mkoani Arusha na polisi kufanikisha ukamataji wa madini hayo.
Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari ya ofisa habari wa Femata, Dk Bernard Joseph iliyotolewa jana, Bina aliiomba serikali kuwachukulia hatua kali wahusika hao kwani kitendo hicho cha
utoroshwaji wa madini hakikubaliki kabisa.
Bina alisema vitendo vya utoroshwaji madini ni kinyume cha maadili na utapeli unaofanywa na wageni unachafua taswira ya uchimbaji wa madini nchini.
“Tunawapongeza askari polisi kwa kukamata madini hayo na kukataa rushwa na pia mzalendo halisi aliyetoa taarifa pamoja na Waziri wa Madini Dotto Biteko kwa kuagiza wapewe zawadi ya sh5 milioni kila mmoja kwa maslahi ya Taifa,” alisema Bina.
Mwenyekiti wa kamati ya madini ya Tanzanite nchini, Money Yousuph alisema tukio hilo limewasikitisha mno kwani bado kuna baadhi ya watu wana hila chafu ya kutorosha madini.
Money alisema wahusika wa tukio hilo wanapaswa kupata adhabu kali kwani hawakubaliani na wizi wa madini uliofanyika kwa kutaka kusafirisha kwa wizi madini hayo.
“Hivi karibuni Rais John Magufuli aliondoa kodi zilizokuwa zinalalamikiwa lakini bado watu wengine wanafanya vitendo vya utoroshwaji wa madini,” alisema.
Mwanamke mchimbaji wa madini ya Tanzanite, ambaye hakupenda kutaja jina lake alisikitishwa na utoroshaji madini huo kwani wamekuwa wakipekuliwa hadi sehemu za siri lakini madini hayo yameibiwa.
“Wanawake tumekuwa tukidhalilishwa kwa kupekuliwa hadi sehemu za siri lakini mbona madini hayo yameibiwa na kutaka kutoroshwa hadi nje ya nchi jirani ya Kenya,” alisema.
Hivi karibuni madini aina ya Tanzanite, Green Tourmarine, Saphure, Aquamarine, Crossulite, Tsavorte, Ruby na Spiwel yenye thamani ya sh958 milioni yaliyokuwa yanasafirishwa kwenda nje ya nchi yalikamatwa na polisi wilayani Longido mkoani Arusha.