Katibu wa CCM Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Ally Kidunda (kushoto) na Makamu Mwenyekiti mstaafu wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Albert Msole ambaye ni Diwani mteule wa Kata ya Ngorika, Albert Msole.
……………………………………………………………………..
Na Mwandishi wetu, Manyara
Madiwani watano wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, wamejitokeza kuwania nafasi ya Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo na madiwani wawili kuwania umakamu Mwenyekiti.
Katibu wa CCM Wilaya ya Simanjiro Ally Kidunda, amesema madiwani wateule saba wamejitokeza kuwania nafasi hizo mbili kupitia CCM.
Kidunda amewataja madiwani wateule hao waliochukua na kurejesha fomu ni Diwani wa kata ya Ngorika na aliyekuwa Makamu Mwenyekiti kwa kipindi cha miaka minne Albert Msole, Diwani wa Kata ya Loiborsiret Ezekiel Lesenga (Mardadi) na Diwani wa kata ya Komolo, Baraka Kanunga.
Amewataja waliochukua fomu wengine ni Diwani mteule wa kata ya Langai na aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Jackson Sipitieck na diwani mteule wa kata ya Naisinyai, Taiko Laizer.
Amesema diwani mteule wa kata ya Orkesumet Sendeu Laizer na kata ya Terrat Jackson Ole Materi wamemchukua fomu ya nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa halmashauri.
“Zoezi lilakalofuata ni wagombea hao kujadiliwa kwenye vikao vya kamati za siasa za wilaya na mkoa ili kuchuja majina kwa ajili ya kuchaguliwa,” amesema Kidunda.
Diwani mteule wa Kata ya Loiborsiret, Ezekiel Lesenga (Mardadi) akizungumza baada ya kuchukua na kurudisha fomu ya kugombea amesema ana imani jina lake litarudishwa na CCM na madiwani watamchagua.
“Nimekuwa na uzoefu wa miaka mitano wa kuwa Diwani kwenye halmashauri yetu hivyo huu ni wakati wa kuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Simanjiro,” amesema Mardadi.
Kwa upande wake, Msole amesema uzoefu wa miaka minne wa nafasi ya umakamu Mwenyekiti wa halmashauri hiyo unatosha kumpa fursa ya kukamata nafasi hiyo.
“Pamoja na hayo elimu niliyonayo nayo itachangia kuhakikisha naongoza kuitoa halmashauri yetu hapa ilipo hadi kwenye maendeleo zaidi ya haya tuliyonayo,” amesema Msole.
Sipitieck ambaye ni diwani mteule wa kata ya Langai, amekiri kuchukua fomu ya kuomba kuchaguliwa tena kuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo.
Diwani mteule wa kata ya Naisinyai, Taiko Laizer amesema amejipima na kuona anatosha kuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya hiyo.
Kanunga amesema anaomba nafasi hiyo kwa ajili ya kutetea maslahi ya wananchi wa Simanjiro na madiwani wake na kuwasemea mahali popote pale nchini.
Aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa halmashauri hiyo na Diwani mteule wa kata ya Orkesumet, Sendeu Laizer amesema anaomba kuchaguliwa tena ili waendelee maendeleo waliyoyafanya.
Diwani mteule wa kata ya Terrat, Jackson Ole Materi amesema anaomba nafasi hiyo ili kuwatumikia wananchi kwani anao uzoefu wa uongozi.