Bondia Jose Carlos Paz na kocha wake Alberto Ramon wakiwasili kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA terminal 3) tayari kwa pambano la ubingwa wa uzito wa super-welter wa WBF dhidi ya bingwa mtetezi Hassan Mwakinyo Novemba 13 kwenye ukumbi wa Net Door Arena Oysterbay
Bondia Jose Carlos Paz wa Argentina( wa pili kulia) akiwasili kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA terminal 3) tayari kwa pambano la ubingwa wa uzito wa super-welter wa WBF dhidi ya bingwa mtetezi Hassan Mwakinyo Novemba 13 kwenye ukumbi wa Net Door Arena Oysterbay. Wa pili kulia ni baba yake Ramon Paz ambaye pia ni kocha wake. Wengine katika picha ni Don Hala wa Jackson Group Sports (wa kwanza kushoto) na wa kwanza kulia ni Katibu Mkuu wa Kamisheni ya ngumi za kulipwa nchini (TPBRC), Yahya Poli.
…………………………………………………………………………………………….
Na Mwandishi wetu
Dar es Salaam. Bondia Jose Carlos Paz atakayezichapa na Hassan Mwakinyo Novemba 13 kwenye ukumbi wa Next Door Arena Oysterbay amewasili na kutamba kutwaa ubingwa wa uzito wa Super Welter wa WBF unaoshikiriwa na Hassan Mwakinyo.
Paz ambaye amewasili na baba yake Alberto Ramon Paz ambaye pia ni kocha wake kama ilivyo kwa bondia Floyd Mayweather.
Akizungumza mara baada ya kuwasili, Paz alisema kuwa amesafiri umbali mrefu kwa ajili ya kutwaa ubingwa katika pambano hili linalojulikana kwa jina la Jackson Group Fight Night.
Paz alisema kuwa amechukua tahadhari kubwa kwa ajili ya Mwakinyo na kwamba siyo bondia mbaya.
“Nimefika mapema zaidi ili kuzoea hali ya hewa, hii ni moja ya mikakati ya ushindi, nilisafiri kwa basin a baadaye kupanda ndege, siku mbili nipo njiani, sitakuwa tayari kushindwa katika pambano hili,” alisema Paz.
Kocha wake, Alberto Ramon naye alisema kuwa wamemsoma Mwakinyo katika mapambano yake na kujua mbinu zake ambazo amezifanyia kazi.
“Tumefanya mazoezi magumu kuelekea pambano hili, tumefanya mazoezi ya ufundi na mbinu, hayo yote ni kwa ajili ya kusaka ushindi ambao tunaamini asilimia 100, tutashinda,” alisema Ramon.
Mkurugenzi Mtendaji wa Jackson Group Sports, Kelvin Twissa alisema maandalizi yanaendelea vizuri na mabondia wa Zambia, Zimbabwe na Kenya watawasili wiki ijayo kwa ajili ya pambano hilo.
Twissa alisema kila kitu kiko katika hatua za mwisho na tiketi zitaanza kuuzwa kwa njia ya Nilipe na Selcom kwa Sh 3 Milioni kwa meza ya watu 10 na Sh150,000 kwa kwa viti vya kawaida.
Pambano hilo litatanguliwa na mengi matatu ambapo bondia nyota wa kike nchini, Zulfa Macho atazipiga na Alice Mbewe kutoka Zambia, Hussein Itaba atazichapa na Alex Kabangu wa DR Congo na Fatuma Zarika wa Kenya atacheza na Patience mastara wa Zimbawe.