Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiapishwa na Jaji Mkuu wa Mahakama Kuu ya Tanzania Profesa Ibrahim Hamis Juma kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kipindi cha pili cha Awamu ya Tano leo tarehe 05 Novemba 2020 katika sherehe zilizofanyika katika uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma.
**************************************
Eleuteri Mangi, MAELEZO, Dodoma
Dkt. John Pombe Magufuli amekuwa Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuapishwa katika jiji la Dodoma mbele ya maelefu ya Watanzania na wageni waalikwa wakiwemo baadhi ya viongozi kutoka mataifa mbalimbali Duniani kuingoza Tanzania kwa kipindi cha pili kuanzia 2020 hadi 2025.
Akizungumza baada ya kula kiapo hicho, Rais Magufuli amesema kuwa siku kama ya leo Novemba 5, 2015 aliapishwa katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam kulingoza taifa kwa kwa kipindi cha miaka mitano kwa awamu iliyoishia leo tarehe 5 Novemba 2020.
“Namshukuru sana Mungu, lakini tofauti na mwaka 2015 ambapo niliapishwa jijini Dar es Salaam kwenye Uwanja wa Uhuru, mara hii nimeapishwa Uwanja wa Jamhuri jiji hili zuri la Dodoma ambapo ni makao makuu ya nchi, ninamshukuru sana Mungu”, alisema Rais Magufuli.
Rais Magufuli amewashukuru sana Watanzania kwa kumuamini na kumpa dhamana ya kuliongoza taifa kwa kipindi kingine cha miaka mitano kwa kumpa ushindi mkubwa pamoja na Chama chake cha Mapinduzi na kusisitiza huo ni ushindi wa watanzania wote.
Aidha, Rais Magufuli ameishukuru Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa kusimamia vizuri zoezi la Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu pia amewashukuru viongozi wa dini kwa kuliombea taifa wakati wote wa zoezi la uchaguzi, kumaliza kwa usalama na hatimaye kulifanya taifa kuendelea kuimarika kuwa la amani na umoja.
Vile vile amevishukuru na kuvipongeza vyombo vya ulinzi na usalama kwa kufanya kazi kwa weledi ambao umewezesha amani na usalama kutawala kwa kipindi chote cha uchaguzi.
“Kwa namna ya pekee nawashukuru na kuwapongeza sana Watanzania kwa kuonesha utulivu mkubwa katika kipindi chote cha uchaguzi, kama mjuavyo katika baadhi ya nchi nyingine uchaguzi umekuwa chanzo cha mogogoro, uhasama na mafarakano. Sisi Watanzania kwa mara nyingine tumevuka mtihani huu na kuudhihirishai ulimwengu kuwa sisi Watanzania ni wapenda amani na tumekomaa kidemokrasia”, amesisitiza Rais Magufuli.
Katika kufikia malengo ya taifa, Dkt. Magufuli amesisitiza mara tatu “uchaguzi sasa umekwisha” akizingatia nchi imejiwekea malengo ya kuwaletea maendeleo kwa taifa na sasa ni muda wa kuchapa kazi kwa ushirikiano kama walivyoahidi katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM na kuyatekeleza yote waliyoahidi pamoja na kulinda Muungano na mipaka yake, uhuru wa taifa pamoja na Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
Rais Magufuli ameapishwa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 Ibara ya 42 (5) kinachobainisha kuwa “Kila Rais mteule na kila mtu atakayeshikilia kiti cha Rais, kabla ya kushika madaraka ya Rais, ataapa mbele ya Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano, kiapo cha uaminifu na kiapo kingine chochote kinachohusika na utendaji wa kazi yake kitakachowekwa kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na Bunge.”
Wakizungumza katika hafla hiyo, Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda, Rais wa Comoro Azali Assoumani, Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe na Makamu wa Rais wa Botswana Slumber Tsogwane wamempongeza Rais Magufuli kwa kuchaguliwa kuiongoza Tanzania na Watanzania wote kwa kufanya uchaguzi wa amani.
Viongozi wengine waliohudhuria hafla hiyo ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza na Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Marais Wastaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ali Hassan Mwinyi, Dkt. Jakaya Kikwete, Rais Mstaafu wa Burundi Sylivester Ntibatunganya, Mabalozi wanaowakilisha nchi zao hapa nchini pamoja na Mawaziri Wakuu wastaafa, Majaji, Mawaziri na Manaibu Waziri ambao wamemaliza muda wao wa uongozi.
Wageni wengine ni viongozi waandamizi wa Serikali viongozi wa dini, wakuu wa mashirika ya kimataifa, wasanii kutoka Tanzania Bara na Visiwani, wanahabari na wananchi toka Dodoma na maeneo mbalimbali nchini.