********************************************
MWENYEKITI mstaafu wa CCM Mkoa wa Manyara, Lucas Ole Mukusi amesema sheria ya uchaguzi inapaswa isisitize wagombea wa Urais kuheshimu tunu za Taifa.
Ole Mukusi ameyasema hayo kupitia maandiko yake ya soma kwa furaha wakati akielezea mustakabali wa kabla na baada ya uchaguzi mkuu wa madiwani, ubunge na urais uliofanyika hivi karibuni.
Ole Mukusi amesema uimara wa Taifa hutokana na uzalendo wa wananchi katika nchi yao na uchaguzi ni mchakato wa kidemokrasia na siyo mwanya wa kulisambaratisha taifa kwa kuhatarisha amani, usalama na utangamano wa kijamii.
Amesema uchaguzi ukigeuzwa mbinu na uchochoro wa kupandikiza ubeberu, kwa vyovyote vile ni tendo la kualika vyombo vya usalama kuwashughulikia kikamilifu wahusika.
Amesema katika kanuni na ama sheria za uchaguzi, sasa umefika wakati wa kuweka kipengele cha makatazo ya hoja za kuvunja Muungano, Iainishwe bayana kwamba mgombea yeyote atakayechochea dhana ya kuvunja Muungano wa Tanganyika na Zanzibar atakuwa amejitoa mwenyewe katika kugombea.
“Kwa mantiki hiyo atakuwa ameenguliwa kisheria katika kugombea nafasi aliyoiwania, hii ndiyo sababu kwa Wamarekani, huwezi kusikia hoja za kubomoa USA kutoka kwa wagombea.” amesema na kuongeza.
“Hiyo ni tunu muhimu na nguvu pekee waliyonayo, wanaiamini na wanaitegemea kwa kadri ya uendelevu wa vizazi vyao na haichezewi na mamluki na wala makuwadi wa ubeberu,” amesema Ole Mukusi.
Amesema kwa hapa nchini Tanzania, sheria ni matokeo ya mchakato wenye kuwahusisha wananchi.
“Vyama vya siasa hualikwa kipekee kujadili na kuweka mawazo yao katika kanuni za uchaguzi wakiwa timamu katika afya ya akili,” amesema Ole Mukusi.
Amesema ni jambo la ajabu wahusika hao kugeuka na kukana uhalali wa chombo walichoshiriki kukitengenezea mifumo ya uendeshaji, kwa kuwa tu hawakushinda katika uchaguzi huu ni udhaifu mkubwa.
Amesema Tanzania kamwe hailinganishwi na mpiga zeze wa kulipwa ambaye hupiga wimbo ambao mhusika atakuwa ameuchagua na siyo vinginevyo.
“Nchi za Magharibi haziwezi kutuwekea uongozi wa nchi yetu kwa manufaa tusiyoyajua na pia hawawezi kutuchagulia marafiki,” amesema Ole Mukusi.