********************************
Ndugu wanahabari mabibi na mabwana, nimewiwa kutumia fursa hii mimi binafsi na kwa niaba ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kuwashukuru watanzania wote na wakazi wa Mbeya, Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama Mkoa wa Mbeya Mhe. ALBERT CHALAMILA pamoja na wajumbe wake wote kwa kushiriki vyema kwenye zoezi la Upigaji kura lililofanyika nchini kote 28.10.2020 kwa Amani na Utulivu.
Pili ninapenda kuwaasa baadhi ya mashabiki wanao waasa wenzao kutokubali matokeo na kuwarubuni washiriki katika matendo ya uvunjifu wa amani, waache kufanya hivyo na yeyote atakayeamua kufanya fujo au uhalifu wowote Jeshi la Polisi hatutasita kumkamata na kumchukulia sheria ikiwa ni pamoja na kumfikisha mahakamani.
Aidha ninawasihi vijana wote kuna watu wanaochukizwa san ana maendeleo ya nchi yetu hivyo wanatamani kuona tunaingia kwenye machafuko, kamwe tusishawishike kwa gharama yoyote kuingiza nchi yetu kwenye janga la mgogoro, amani yetu ni tunu tuliyoasisiwa na wahenga wetu.
Jeshi la Polisi tunaendelea na doria maeneo yote ila nitoe rai kwa mashabiki ambao vyama vyao vimeshinda washerehekee maeneo salama na kwa ustaarabu ili kujiepusha na shari.
Nawaasa tusishiriki kwenye mambo yafuatayo:-
⦁ Maandamano yasiyo na vibali.
⦁ Kuchoma matairi, kuchoma barabara
⦁ Kuharibu miundombinu yoyote ya Umma/Serikali
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linaendelea kuimarisha ulinzi katika maeneo yote kwa kuhakikisha “section” za askari zinafanya doria kuzungukia maeneo mbalimbali ili kuhakikisha hali ya Amani na Utulivu inaendelea kuwepo katika maeneo yote.
Aidha katika siku ya kupiga kura 28.10.2020 yapo baadhi ya matukio ya uvunjifu wa Amani yaliyoripotiwa na jumla ya watuhumiwa 67 walikamatwa ambapo kati yao 12 bado tunaendelea kuwashikilia na kesho tutawafikisha mahakamani, watuhumiwa 55 wameachiliwa kwa dhamana. Baadhi ya matukio hayo ni pamoja na shambulio la kudhuru mwili, kuharibu mali, wizi wa kadi ya kupigia kura na kufanya fujo kituo cha kupigia/kuhesabu kura.