Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Busega Anderson N. Kabuko akitangaza matokeo kwa nafasi ya Ubunge na Udiwani.
****************************************
Washindi katika nafasi ya Ubunge na Udiwani Jimbo la Busega wametangazwa hii leo tarehe 29/10/2020. Matokeo ya nafasi hizo yametangazwa na Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Busega Anderson N. Kabuko.
Nafasi ya Ubunge Jimbo la Busega iliwaniwa na wagombea wanne (4) kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM), Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ACT Wazalendo na Civic United Front (CUF)
Kura zilizopigwa ni 48,230, kura halali zikiwa ni 46,634, kura zilizoharibika zikiwa ni 1,596, huku jumla ya idadi ya waliojiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura ikiwa ni 124,316. Nafasi ya kiti cha Ubunge imechukuliwa na Simon Songe Lusengekile kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) aliyepata kura 35,770, akifuatiwa na Adam Alphonce Komanya kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) aliyepata kura 9,063.
Kwa upande wa nafasi za kiti cha Udiwani kutoka katika kata 15 zilizopo Jimbo la Busega, CCM imeshinda jumla ya kata 14 huku CHADEMA ikishinda kata moja.
Aidha Kabuko amevishukuru vyama vya siasa, vyombo vya ulinzi na wananchi kwa ujumla kwa kuonesha utulivu kwa kipindi chote cha uchaguzi. Uchaguzi mkuu Jimbo la Busega umefanyika huku hali ya usalama ikiwa shwari, hali iliyopelekea utulivu wa wananchi.