***********************************************
Na Mwandishi wetu, Manyara
MGOMBEA Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt John Magufuli amewaahidi kujenga barababa ya lami inayopita Wilayani Mbulu Mkoani Manyara ikitoka Wilaya ya Karatu Mkoani Arusha hadi Mkoani Singida.
Dkt Magufuli ametoa ahadi hiyo Mjini Babati kwenye mkutano wa kampeni ya CCM uliofanyika uwanja wa Kwaraa Mkoani Manyara.
Amesema ahadi hiyo ya ujenzi wa barababa ya lami ipo kwenye ilani ya uchaguzi wa CCM ya mwaka 2020/2025 hivyo itatekelezwa.
Amesema barababa hiyo itakayotoka Wilayani Karatu Mkoani Arusha itapitia Mbulu Mjini hadi hospitali ya rufaa ya Haydom Jimbo la Mbulu Vijijini hadi Mkoani Singida.
“Nichagueni kwa kipindi kingine cha miaka mitano nijenge hiyo barabara kwani nimeweza kujenga barababa za juu fly over na kununua ndege sasa nitashindwaje kujenga barabara ya Mbulu?” amehoji Dkt Magufuli.
Hata hivyo, mbunge wa jimbo la Mbulu Vijijini Flatei Maasay amemshukuru Rais Magufuli kwa ahadi hiyo na kudai kuwa atahakikisha wananchi wa eneo hilo wanamchagua tena kwa kura nyingi.
“Wapiga kura wa Jimbo la Mbulu Vijijini wanakufuatilia kwenye vyombo vya habari bila shaka yoyote watakupa kura nyingi za ndiyo,” amesema Maasay.
Mgombea ubunge wa jimbo la Mbulu Mjini Paul Zacharia Isaay amemshukuru Rais Magufuli kwa kuwapa ahadi ya utekelezaji wa ujenzi wa barabara hiyo ya lami.
“Hakuna haja ya wewe kufika Mbulu kupiga kampeni mimi mwenyewe natosha kukunadi hadi upate kura za kishindo,” amesema Isaay.
Mbunge mteule wa viti maalumu Mkoani Manyara, Martha Umbullah amemuahidi Dkt Magufuli kupata kura nyingi za kishindo kupitia maendeleo aliyoyafaya mkoani humo.
Mbunge mteule wa viti maalumu Mkoani Manyara, Regina Ndege amesema wananchi wa mkoa wa Manyara wana imani kubwa na Dkt Magufuli hivyo atashinda kwa kura nyingi.
Mbunge mteule kupitia vijana Asia Halamga amewapigia magoti wananchi wa mkoa huo na kuwaomba wamchague Dkt Magufuli kwa kura nyingi za ndiyo.