******************************************
Na Emmanuel J. Shilatu
Ni miaka 5 sasa tangu Dk. John Pombe Joseph Magufuli ale kiapo mnamo Novemba 5, 2015 cha kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tumeyaona haya yakitokea na kufanyika;-
1. Mapambano ya wazi wazi ya Serikali ya Rais Magufuli ya vita dhidi ya rushwa na ufisadi nchini. Leo hii Tanzania imepanda kwa nafasi 13 katika mwaka 2016 na 2017 na pia ikishika nafasi ya pili (2) kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
2. Serikali ya Rais Magufuli imefanikisha zoezi zima la Serikali kuhamia Dodoma. Ni vyema tukakumbuka zoezi la kuhamia Dodoma liliasisiwa na kushindwa kufanyika toka enzi ya utawala wa awamu ya kwanza wake Rais Mwalimu Nyerere lakini ndani ya kipindi kifupi cha miaka miwili tu Serikali ya Rais Magufuli imeweza kuuvunja mfupa huu mgumu.
3. Ujenzi wa Miundombinu ya kipekee na ya kisasa. Kupitia Serikali hii ya awamu ya 5 ya Rais Magufuli tumeshuhudia ujenzi wa flyovers na ujenzi wa reli ya kisasa kwa kiwango cha standard gauge inayotumia umeme na inayokwenda kwa kasi. Haijawahi kutokea hii tangu Tanzania iumbwe.
4. Serikali ya awamu ya 5 ya Rais Magufuli hutumia Tsh.Bilioni 24 kutoa ELIMU BURE kuanzia elimu ya Msingi mpaka kidato cha nne. Mara ya mwisho Tanzania kushuhudia elimu ikitolewa bure ni katika utawala wa awamu ya kwanza ya Mwalimu Nyerere.
5. Mafisadi Papa, Wala rushwa Papa wamepandishwa Mahakamani na wengine mpaka leo hii wanasota Magerezani mpaka kesho. Katika miaka ya nyuma ilikuwa suala gumu sana kwa Watuhumiwa “Mapapa” kuguswa tu, achilia mbali kupandishwa Mahakamani.
6. Tumeshuhudia akisimamia kwa vitendo kauli yake ya Tanzania ya viwanda. Tangu Rais Magufuli aingie madarakani zaidi ya viwanda vikubwa na vidogo zaidi ya 8000 vimezinduliwa na vinafanya kazi. Uwepo wa idadi kubwa ya viwanda inasaidia sana kupunguza tatizo la ajira nchini.
7. Uwajibikaji na uadilifu kwa Watumishi wa umma umeongezeka na kuimarika vilivyo. Leo hii Mtumishi wa umma hana majivuno, kiburi wala dharau kwa wale anaowahudumia. Siku hizi watumishi wa umma wanawahi makazini, wanachapa kazi nyakati zote na wanazingatia ubora na umakini wa kazi.
8. Suala la matabaka ndani ya jamii linazidi kupungua kwa kasi tangu utawala wa awamu ya 5 uingie madarakani. Leo hii Watoto wa Maskini nao pia wanakwenda shule kupitia sera ya elimu bure; hakuna tena ubabe wa dhuruma Mahakamani, kwenye masuala ya ardhi; leo hii hakuna tena zile kauli kandamizi za “unanijua mimi nani” ama “Kijana kaa mbali, nitakupoteza”. Hakika Watu wanyonge Maskini nao pia wanafurahia maisha vilivyo, hakuna tena ubabe wala matabaka.
9. Serikali ya Rais Magufuli imeimarisha na kuzingatia suala la amani na uhuru wa kidemokrasia ndani ya nchi. Mathalani Machi 5, 2018 tumesikia Umoja wa Mataifa (UN) ukimpongeza Rais Dk. Magufuli kwa kudumisha amani na usalama ndani na nje ya Tanzania.
10. Kasi kubwa ya viongozi wa upinzani wakubwa kujiunga na CCM umekuwa mkubwa sana. Tumeshuhudia Madiwani, Wabunge na viongozi waandamizi wa upinzani wa upinzani wakijiunga na CCM ili kumuunga mkono Rais Magufuli kwa yale mambo mazuri ya kiutendaji anayoyafanya. Kujiunga kwa upinzani na dalili tosha ya Watu kulidhishwa na kiwango kikubwa cha utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi 2015 – 2020.
11. Kufufuka kwa mashirika ya umma yaliyokuwa taabani. Tumeona shirika la ndege, reli na la simu yakipata uhai mara baada ya Dk. Magufuli kuingia Ikulu. Mathalani upande wa ndege jumla ya ndege 11 mpya zimeshanunuliwa, upande wa simu Serikali ya awamu ya 5 ilinunua hisa zote za shirika za simu na hivyo kuanza kuimiliki kwa asilimia mia na kuanza kuliboresha shirika.
12. Tumeshuhudia Serikali ikianzisha na kufanya miradi mikubwa na ya kihistoria ya kimaendeleo. Mathalani tumeshuhudia ujenzi wa reli ya kisasa ya umeme kwa kiwango cha Standard gauge; Mradi wa ujenzi wa umeme wa Stiegler’s Gorge (Mto Rufiji) utakao kuwa chanzo kingine cha umeme na hivyo kupunguza tatizo la umeme nchini; Ujenzi wa flyovers za Tazara na Ubungo ambayo itasaidia kupunguza msongamano wa magari mkoani Dar es Salaam.
13. Kufutwa kwa kodi mbalimbali za kilimo, Serikali kusimamia masoko ya bidhaa za wakulima na hivyo kufanya kilimo kuwa na tija nchini. Wote ni mashuhuda kwa namna gani Wakulima wa Korosho nchini wanavyonufaika, ambao walikuwa wakiuza korosho kwa bei Tsh. 800 kwa kilo hapo awali lakini tangu Rais Magufuli aingie Ikulu bei ya korosho imepanda maradufu hadi kufikia bei ya Tsh. 4000 kwa kilo. Maboresho hayo yapo hadi kwenye mazao mengine.
14. Tumeshuhudia Serikali ya awamu ya 5 yake Dk. Magufuli ikipambana vilivyo na adui maradhi. Mathalani jumla ya vituo vya kutolea huduma za afya 1,769 vimejengwa kuanzia 2015 – 2020 ambapo ni Zahanati 1198, vituo vya afya 487, hospitali za wilaya 71, hospitali 10 za mikoa na hospitali za rufaa za kanda 3. Sanjali na ujenzi ni pamoja uboreshaji wa tiba za kibingwa, kupungua kwa rufaa za Wagonjwa kwenda nje ya nchi kwa 95%.
15. Tumeshuhudia Serikali ikiweka uwazi kwenye mikataba na uchunguzi wa rasilimali za Taifa na kuweka makubaliano mapya yenye tija Mathalani tumeona uwazi wa sekta ya madini ya dhahabu, almas na Tanzanite ambapo Taifa tumeona namna ambavyo tulivyokuwa tukiibiwa na Serikali kuweka mikakati mipya ya kutokuibiwa tena. Kama haitoshi tumeshuhudia wawekezaji wakibanwa vilivyo juu ya mikataba isiyokuwa na tija kwa Taifa. Ni Serikali ya Rais Magufuli iliweka uthubutu wa kuwabana wawekezaji wa madini wa ACACIA iliyozaa matunda kwa Serikali ya Tanzania kumiliki asilimia 16 ya hisa katika makampuni ya uchimbaji wa madini, Serikali kupata gawio la faida ya madini ya asilimia 50 kwa 50. Yote haya yamewezekana kwa sababu ya uzalendo wake Rais Dk. Magufuli. Matokeo yake tumeona kwa mara ya kwanza tangu Dunia iumbwe Tanzania imepewa gawio la zaidi ya Tsh. Bilioni 100
16. Serikali ya Rais Magufuli imefanikisha vilivyo kushirikiana na nchi ya Uganda kujenga Bomba la Mafuta linalotoka nchini Uganda mpaka Tanga nchini Tanzania. Ujenzi huo wa bomba la mafuta utazalisha ajira nchini na utaongeza pato la Taifa. Hayo yote yamefanikiwa kutokana na Serikali ya Rais Magufuli kuzidi kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia na nchi nyinginezo.
17. Ni Serikali ya Rais Magufuli imeweka jitihada za kupunguza utegemezi kwa kuamua kubinya mianya yote ya upotevu wa kodi na kuanzisha vyanzo vipya vya kodi. Leo hii makusanyo ya kodi ni zaidi ya Tsh. Trilioni 1.2 mpaka Tsh. Trilioni 1.9 kwa kila mwezi. Wakati Serikali ya awamu ya 5 inaingia madarakani makusanyo ya kodi yalikuwa Tsh. Bilioni 800 tu kwa kila mwezi.
18. Ukuaji wa uchumi umezidi kuongezeka kwa kasi kutoka asilimia 5.7 kwa mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 7.2 kwa mwaka 2020. Ukuaji huu wa kiuchumia unaifanya Tanzania kuwa nchi ya pili Barani Afrika kwa kasi ya ukuaji wa kiuchumi.
19. Rais Magufuli amevunja rekodi ya kuunda Serikali yake pasipo kujali itikadi, kabila, rangi, dini wala ukanda. Mathalani tumeshuhudia Rais Magufuli akiwateua Wapinzani kushika nafasi nyeti Serikali. Mfano alimteua Prof. Kitila Mkumbo wa ACT Wazalendo kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Maji, alimteua Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Anna Mgwhira kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro na pia alimteua Mwenyekiti wa TLP, Augustino Lyatonga Mrema kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Parole. Hakika Rais Magufuli ameamua vilivyo kujitenga na dhambi ya ubaguzi na kuegemea nguzo ya umoja na upendo kwa Watanzania wote.
20. Ni Serikali ya Rais Magufuli imeamua kupunguza matumizi ya anasa na pesa zote kuzielekeza kwenye shughuli za kimaendeleo. Kwa kufuta safari za nje, vitafunwa, posho, semina na walsha zisizo na tija imepelekea Serikali kuokoa pesa nyingi zinazoelekezwa kwenye shughuli za kimaendeleo ikiwemo kufanikisha miradi mikubwa nchini.
21. Tumeshuhudia Rais Magufuli akifanya maamuzi magumu, ya haraka, sahihi na kwa wakati pindi Wananchi inapolalamika juu ya kukabiliwa na tatizo la kijamii. Ilishatokea kwenye hospitali ya Muhimbili pindi Mwanamama alipopaza sauti juu ya akina Mama wanaojifungua kulala chini, hapo hapo Rais Magufuli akaamuru zilizokuwa ofisi zibadilishwe na kuwa wodi, ikafanyika hivyo. Pia tusisahau Rais Dkt John Pombe Magufuli alivyowapa wakazi wa Bagamoyo, eneo la Magereza lenye ukubwa wa heka 65. Huyo ndio Dk. John Pombe Magufuli, mwenye maamuzi magumu, sahihi na kwa wakati.
22. Serikali ya Rais Magufuli imekuwa na desturi njema ya kulipa madeni ya ndani na ya nje. Mathalani tumesikia Serikali ikilipa madeni ya ndani ya Wakandarasi, watoa huduma, Waalimu n.k.
23. Serikali ikiacha umangi meza na kwenda palipo na Wananchi, palipo na shida za jamii. Si Wakurugenzi, Wakuu wa wilaya, wa Mkoa, Mawaziri ama Makatibu wakuu wote wapo field kuhakikisha wanaenda kuzitambua na kuzitatua shida za Wananchi. Mtindo wa viongozi kubaki baki ofisini zaidi kuliko kuwa site ulishakufa tangu Rais Dk. Magufuli alipoingia Ikulu.
24. Urasimu kuwaona Viongozi umepungua; Miaka ya nyuma kumuona Kiongozi wa Serikali ilikuwa kazi ngumu kuliko hata kuisaka sarafu baharini, huo ndio ukweli. Viongozi walio wengi walijiwekea ukuta kiasi Mwananchi wa kawaida kumvikia ilihitaji uvumilivu wa hali ya juu. Tangu Rais Magufuli aingie viongozi wenyewe wa Serikali wameweka mfumo mpya wa kiutendaji kwa kutenga siku maalum (siku 2 ama 3 kwa wiki) ambazo Mwananchi anaenda kumuona kiongozi moja kwa moja pasipo kupita kwa Katibu Muhtasari (Sekretari). Pia wapo baadhi ya Viongozi wakubwa wa Serikali wanatoa mpaka namba zao za simu za mikononi ama za wasaidizi wao ili Wananchi waweze kuwasilisha kero na matatizo yao moja kwa moja. Utaratibu huo umerahisisha matatizo ya Wananchi kuweza kufika kwenye mamlaka kwa wakati na kupatiwa ufumbuzi wa haraka.
25. Viongozi wamepewa meno zaidi; Tangu Rais Magufuli aingie madarakani tumeshuhudia Viongozi, mamlaka za kitaasisi zikipata meno zaidi ya kiutendaji tofauti na hapo awali kila kitu kuachiwa mamlaka ya Urais iamue, ulikuwa ni utegeaji wa hali ya juu. Mathalani leo hii tunashuhudia TAKUKURU ikipata meno zaidi ya kupambana na rushwa nchini hali iliyopelekea kesi za rushwa kuongezeka Mahakamani.
26. Kiwango cha nidhamu, uwajibikaji na uadilifu kwa Viongozi wa Serikali kimezidi kuongezeka. Tangu Rais Magufuli aingie madarakani yale mazoea yasiyo na tija ya viongozi kuzoea kazi hayapo, ule mtindo kiongozi akiharibu hapa anahamishiwa kule haupo, suala la kiongozi anafanya madudu na bado anabaki kwenye ofisi ya umma haupo tena. Kila Kiongozi ama kila Mtumishi wa umma yupo makini akichapa kazi vilivyo kwa nidhamu na uadilifu wa hali ya juu.
27. Ufuatiliaji wa utendaji, ufuatiliaji wa maagizo umekuwa wa hali ya juu. Tangu Rais Magufuli aingie Ikulu ameiambukiza sifa zake za uadilifu, uchapakazi, uzalendo na ufuatiliaji. Naam ufuatiliaji wa majukumu, maagizo, ripoti na tafiti zinazotolewa umekuwa wa hali ya juu. Pindi inapobainika madudu kufanyika ama jambo kutokufanyika kwa wakati Rais Magufuli hasiti kabisa kufukuza Mtu na baadhi yao kuishia mikononi mwa vyombo vya kisheria.
28. Utawala wa Sheria umezidi kuimarika. Rais Magufuli aliapa kuilinda na kuitetea katiba ya nchi iliyo na sheria, taratibu na kanuni, amefanikiwa katika hilo. Leo hii tunazidi kuona mihimili ya dola inapofanya kazi kiukamilifu pasipo mwingiliano, kila mhimili upo huru; Leo hii tunaona Viongozi, Wanasiasa, Watumishi wa umma wakipandishwa kizimbani na wengine wanahukumiwa kifungo jela pindi wanapokutwa na makosa ya kisheria. Hakika, utawala wa kisheria unaoonyeshwa na Serikali ya awamu ya 5 yake Rais Magufuli ni nguzo ya utawala bora.
29. Heshima ya Tanzania kimataifa imezidi kukua zaidi; Hali ya Tanzania kusikika zaidi ilikuwa juu sana kipindi cha awamu ya kwanza kutokana na uwepo wa Mwalimu Nyerere ambapo hii leo Tanzania imezidi kupata sifa zaidi kutokana na uchapakazi wa Rais Magufuli. Nchi mbalimbali Duniani zimekuwa zikivutiwa na Rais Magufuli kutokana na namna anavyopambana na rushwa, ufisadi, matumizi mabaya ya pesa za umma, namna Serikali inavyobana matumizi na namna Rais Magufuli anavyoonyesha uzalendo wa kulinda rasilimali za Taifa zimnufaishe Mtanzania. Hayo ni baadhi tu ya mambo yanayoifanya leo hii jina, hadhi na heshima ya Tanzania kuweza kupaa juu zaidi tangu Rais Magufuli aingie Ikulu.
30. Heshima ya Mwanamke imezidi kuimarika Serikalini na kwenye jamii. Dalili njema za Rais Magufuli kuweza kuheshimu nafasi ya Mwanamke ilianza kujitokeza pindi alipomteua Mama Samia Suluhu kuwa Mgombea mwenza wa Urais ambaye leo hii ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mama Samia ni Mwanamke pekee aliyeshika nafasi ya juu kabisa kiungozi katika nchi za Afrika Mashariki. Hata mara baada ya kuingia Ikulu Rais Magufuli ameongeza imani kwa kuwateua Wanawake kwenye nafasi mbalimbali za kiuongozi Serikalini. Pia amewateua na kuwapandisha vyeo kwenye nafasi za vyombo vya dola na hata wengineo kuwateua kuwa Majaji. Imani aliyoonyesha Rais Magufuli kwa Wanawake ni ishara tosha ya heshima kubwa aliyowapa Wanawake nchini.
Hayo ni kwa uchache tu wa mambo ya JPM aliyoyafanya na mengineyo yanahitaji usimamizi wake yaweze kukamilika ndio maana Watanzania tunampa mitano tena Rais Magufuli.
Naam Magufuli kama Magufuli ana jambo lake Oktoba 28, 2020. Shime Watanzania twendeni tukapige kura ya ndio ya haki, usawa, Uhuru, historia, maendeleo ya Urais kwa Magufuli, kura ya ndio kwa Wabunge na Madiwani wa CCM. Kazi iendelee