Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Joseph Joseph Mkirikiti akizungumza mjini Babati, kushoto ni Mganga Mkuu wa Mkoa huo Dkt Damas Kayera
****************************************
Na Joseph Lyimo, Manyara
ILI kujikinga na magonjwa ya milipuko wananchi Mkoani Manyara wametakiwa kutumia vyoo na kunawa mikono pindi wanapotoka chooni.
Mganga mkuu wa mkoa wa Manyara Dkt Damas Kayera ameyasema hayo wakati akielezea hatua za kujikinga na magonjwa mbali mbali ya milipuko, ikiwemo matumbo ya kuharisha.
Dkt Kayera amesema suala la usafi wa kuwa na vyoo kutumia linamuhusu mwananchi mwenyewe katika eneo lake, na ni jambo la lazima kwa muhusika mwenyewe katika kujikinga.
Amesema usafi wa kutumia vyoo iwe baada ya haja ndogo ama kubwa, kwa kutumia sabuni ili kuulia vimelea vya magonjwa, ni jambo jema kwa jamii, ili kujikinga na magonjwa hayo ya milipuko.
“Magonjwa kadhaa ya milipuko iwe kipindupindu, tumbo lakuharisha damu, minyoo, macho tongo, maradhi ya vikope, homa ya mapafu yanaweza kuepukika kwa mtu kuwa msafi mwenyewe,’’ amesema Dk Kayera.
Amesema unawaji mikono uwe ndio tabia na isiwe baada ya COVID-19 imepungua na wananchi wakapuuzia, maana yapo magonjwa kadhaa yanayosababishwa na kutonawa mikono kama wanavyoshauri.
“Pia inawezekana wananchi wakanawa mikono wanadhani ni kama vile wanavyonawa baada au kabla ya kula, ila upo utaratibu uliokubaliwa na shirika la afya Dunia ‘WHO’ ambao ndiyo unaoua vimelea,’’ amesema Dk Kayera.
Ameitaka jamii waendeleze utamaduni wa kuosha mikono kwa maji tiririka na sabuni kila wakati, ikiwa ni miongoni mwa kinga ya magonjwa ya milipuko.
Hivi karibuni Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro mhandisi Zephania Chaula ameagiza wakazi wa eneo hilo ambao hawana vyoo wajenge ili kuepuka magonjwa ya milipuko.
Mhandisi Chaula amesema ametoa maagizo kwa maofisa Tarafa, watendaji wa kata na vijiji kuhakikisha wanasimamia hilo ili vyoo vijengwe.
Mkazi wa kata ya Terrat John Mollel amesema jamii ya wafugaji huwa na mwamko mdogo kwenye suala zima la matumizi ya choo kutokana na utamaduni walionao.
“Mtu kuwa na choo kisha atumie choo kimoja na mtoto wake wa kike au mama mkwe inakuwa vigumu mno kwenye suala hilo kwa jamii yetu hivyo elimu iendelee kutolewa,” amesema.