*************
.
Katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume viongozi mbali mbali wa Serikali, vyama vya siasa pamoja na wakuu wa vikosi vya ulinzi na usalama wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wakiongozwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd walimuaga Rais Dk. Shein.
Dk. Shein katika safari hiyo, amefuatana na Mkewe Mama Mwanamwema Shein pamoja na Watendaji wengine wa Serikali.
Wakati huo huo, Rais Dk. Shein amemtumia salamu za rambirambi Mtawala wa Sharjah Sheikh Sultan Bin Mohammad Al Qasimi pamoja na kuwatumia salamu za pongezi Rais wa Muungano wa Visiwa vya Comoro Azali Assoumani na Rais wa Malawi Arthur Peter Mutharika kufuatia siku ya uhuru wa Mataifa hayo.
Rais Dk. Shein alituma salamu hizo kwa Mtawala wa Sharjah kufuatia kifo cha mwanawe Sheikh Khalid bin Sultan bin Mohammad Al Qasimi kilichotokea London, nchini Uingereza Julai 1, mwaka huu.
Dk. Shein alieleza kuwa amepokea kwa huzuni kubwa taarifa ya kifo cha mtoto wa kiongozi huyo na kwa niaba yake binafsi pamoja na wananchi wote wa Zanzibar, wanatoa salamu zao za pole kwa familia, ndugu na wananchi wote wa Sharjah na Taifa zima za Umoja wa Falme nchi za Kiarabu kwa jumla.
Aidha, Rais Dk. Shein amemtumia salamu za pongezi Rais wa Muungano wa visiwa vya Comoro, Azali Assoumani kwa kutimiza miaka 44 ya Uhuru wa Taifa hilo.
Kwa niaba yake binafsi, kwa niaba ya watu wa Zanzibar na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dk. Shein alitoa pongezi hizo kwa kiongozi huyo na wananchi wake wote katika Taifa hilo kwa kutimiza umri huo pamoja na kupongeza mafanikio ya kiuchumi na kijamii yanayondelea kupatikana.
Aidha, Dk. Shein alimuhakikishia kiongozi huyo kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendeleza ushirikiano wake sambamba na kuimarisha uhusiano wa kihistoria ulipo baina ya pande mbili hizo na watu wake.