Urais kupitia ADC, Queen Sendiga akihutubia mamia ya wananchi wa Singida Mjini,
waliofika kumsikiliza kwenye uwanja wa stendi ya zamani jana.
Sendiga akionyesha mfano wa Karatasi ya Kupigia Kura na sehemu kilipo chama
chake na jina lake, ili kuwarahisishia wapiga kura kumtambua kirahisi na
kumchagua ifikapo Oktoba 28 .
Singida mjini wakisikiliza Sera na Ilani ya ADC kupitia mgombea wake wa nafasi
ya Rais.
wakifuatilia mkutano huo wa Kampeni.
Sendiga akizungumza kwenye mkutano huo.
wakifuatilia mkutano huo wa Kampeni.
ukiendelea.
Na Mwandishi Wetu,
Singida
MGOMBEA Urais kupitia Chama cha Alliance For Democratic
Change (ADC), Madam Queen Sendiga, amesema anaomba ridhaa ya kuwatumikia
wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama Rais wa kwanza mwanamke, lengo
hasa ni kutatua kero sugu hususani kwenye la afya, maji, elimu na ajira ambazo
zimeshindwa kutatuliwa na mamlaka zilizopo kwa takribani miaka 59 tangu uhuru.
Sendiga aliyasema hayo, wakati akinadi Sera na Ilani ya ADC
kwenye mkutano wa Kampeni za kuwania nafasi ya Rais kwa mwaka 2020,
alipohutubia mamia ya wananchi waliokusanyika viwanja vya stendi ya zamani
mkoani hapa jana.
“Nimesukumwa kwa dhati ya moyo wangu kama mwanamke…na kama
mama kulitumikia Taifa hili kwa nafasi ya Rais, kwa sababu CCM kwa miaka 59 tangu
tupate Uhuru imeshindwa kufanya mageuzi stahiki kwa mtanzania katika muktadha
wa kimaendeleo licha ya kujaliwa rasilimali zote muhimu,” alisema.
Alisema kitendo cha yeye kutokata tamaa, licha ya idadi ya
wagombea hai wa kinyanganyiro cha nafasi ya Rais toka 15 mpaka kubakia wanne kwa
sasa, ni dalili tosha na kiashiria cha wazi kwamba ana mapenzi ya dhati-na ya ‘kimama’
ya kutaka kulitumikia Taifa kwa upendo na matarajio chanya kwa kila mwananchi.
Akizungumzia sekta ya afya alisema suala la bima kwa kila
mwananchi bila ya masharti yoyote halikwepeki, na kwamba nchi zote
zilizoendelea zimewekeza na kutoa msukumo kwenye huduma za afya kwa kuamini
kwamba huduma bora za afya ndio msingi wa ustawi wa afya ya raia kwa matokeo
chanya ya mageuzi ya kiuchumi.
Aidha, katika elimu mwanamke huyo ambaye kama atapewa ridhaa
na watanzania atakuwa Rais wa kwanza Mwanamke tangu Uhuru na wa 3 kwa Bara la
Afrika, alisema anaamini maisha duni ni matokeo ya elimu duni.
“Elimu ni kila kitu, elimu ndio ufunguo wa maisha. Mtu
akikunyima elimu bora ujue amekunyima maisha, tusisahau pia ndugu zangu elimu
bora sambamba na maarifa yenye tija, ni matokeo chanya ya umahiri na ufanisi kwenye
taaluma nyingine mbalimbali,” alisisitiza Sendiga.
Katika suala la elimu, alisema ADC kwanza watahakikisha
wanatoa elimu bure kweli kweli, pia watajikita katika kutoa maarifa na sio
kukaririsha kama ilivyo kwa sasa, na zaidi watabadili mtaala uliopo ili
kumfanya mwanafunzi afundishwe ‘elimu maarifa’ kwa kuzingatia elimu bila
maarifa ni kazi bure.
Hata hivyo, Sendiga akizungumzia suala la ajira, alisema
mkakati wa chama hicho chini ya serikali yake ni kuhakikisha wanakwenda
kuzalisha ajira milioni 10, kwa kuhakikisha wanatengeneza miundombinu rafiki kwenye
sekta zote mtambuka, ikiwemo kilimo, uvuvi, elimu maarifa na nyinginezo.
“Chama chetu kitashughulikia kwa nguvu zote changamoto zote
zilizopo sekta ya kilimo kwa kuhakikisha kunakuwepo na pembejeo za kutosha,
masoko ya uhakika ya mazao ya wakulima, maboresho ya miundombinu kwenye sekta
mbalimbali vijijini, ikiwemo maji safi na salama, na ubora wa elimu,” alisema.
Katika kuthibitisha hali ya ukomavu wa kisiasa, uzalendo wa
kipekee na nia yake ya dhati ya kuendelea kuwa miongoni mwa wapigania maslahi
ya amani ya Tanzania, kama jina lake lilivyo maarufu “Mama wa Taifa” Sendiga
aliwasihi wananchi kuhakikisha ifikapo Oktoba 28 wakichapiga kura ya kumchagua yeye
na wabunge wa chama chake basi warudi nyumbani kusubiri matokeo.
“Ukipiga kura rudi nyumbani..tunza amani. Ukifanya vurugu
yoyote utakamatwa na kushtakiwa kwa jinai kama mhalifu mwingine yeyote na
utajikuta ukiishia kuozea jela. Hutahukumiwa kama mwanachama wa chama fulani
bali kama mhalifu,” alionya Sendiga, ambaye Singida ni mkoa wake wa 16, tangu aanze
kampeni hizo.