Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mahusiano ya Dini Mkoa wa Ruvuma Shekh Ally Hassan Mahaba akitoa tamko la Kamati kuelekea uchaguzi Mkuu wa Tanzania
Katibu wa Kamati ya Mahusiano ya Dini mkoani Ruvuma Alhaj Abdulah Mohamed Ndesai akuzungumza kwenye kikao maalum katika hoteli ya Hunt Club mjini Songea.Grace Msuya Mjumbe wa Kamati toka Kanisa la KKKT akitoa maoni yake.
Baadhi ya wajumbe wakiwa kwenye kikao cha Kamati ya Mahusiano ya Dini mkoa wa Ruvuma
***************************************
WATANZANIA wametakiwa kutambua umuhimu wa kujitokeza kuchagua viongozi ngazi mbalimbali kwenye Uchaguzi Mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 28 mwaka huu.
Rai hiyo imetolewa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mahusiano ya Dini mkoani Ruvuma Shekh Ally Hassan Mahaba,wakati Kamati hiyo inatoa tamko kuelekea Uchaguzi Mkuu kwa wanahabari kwenye ukumbi wa Ruhuwiko Hunt Club mjini Songea.
Shekh Mahaba ameyataja matamko ya Kamati ya Dini Mkoa wa Ruvuma kuwa ni kuombea uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 28 mwaka huu na kusimamia amani na upendo wa nchi.
Amesema katika kuhakikisha zoezi la uchaguzi Mkuu linafanyika kwa amani,Kamati ya Mahusiano ya Dini mkoani Ruvuma imeweka utaratibu wa kuombea uchaguzi kwenye misikiti na makanisa siku mbili ambazo ni Oktoba 23 na Oktoba 25 mwaka huu.
“Tumeendelea kusisitiza kwamba,waumini wetu na wasiokuwa waumini Oktoba 28 mwaka huu,wakishapiga kura warudi nyumbani kupumzika ,wakisubiri matokeo ’’,alisisitiza Shekh Mahaba.
Makamu Mwenyekiti huyo amesisitiza kuwa isitokee vurugu baada ya wananchi kupiga kura na kwamba kupiga kura ni suala la siri ambapo ameitaja kazi kubwa ya viongozi wa dini ni kuhubiri upendo,mshikamano,amani,na ushirikiano.
Ametoa rai kwa wasimamizi wa uchaguzi kufanyakazi kwa weledi na kuwasaidia watu wenye mahitaji maalum kama wenye ulemavu ili waweze kujaza fomu zao vizuri kwenye vituo vya kupigia kura.
Amewaasa viongozi wa dini wasijihusishe na kuelekeza waumini kwamba apigiwe kura mgombea Fulani katika kipindi hiki.
Kwa upande wake Katibu wa Kamati ya Mahusiano ya Dini Mkoa wa Ruvuma Alhaj Abdalah Mohamed Ndesai amesema Kamati imedhamiria kuhubiri amani na utulivu kila wakati ili Tanzania iendelee kuwa kisiwa na amani.
Amesema nchi inapoingia kwenye uchaguzi Mkuu,viongozi wote wa dini wanapaswa kuwaeleza waumini umuhimu wa kwenda kupiga kura kwa sababu ni haki na Katibu ya nchi inaruhusu kila baada ya miaka mitano kufanya uchaguzi kwa amani na utulivu.
Mackei Mguhi ni Mjumbe wa Kamati ya Mahusiano ya Dini toka Kanisa la Anglikana,amesema Tanzania imekuwa na amani kwa miaka yote, hivyo hatutegemei katika uchaguzi wa safari hii mambo kuwa tofauti ambapo amesisitiza viongozi wa dini kuendelea kuhubiri amani na upendo kabla na baada ya uchaguzi.
Kwa upande wake Mjumbe wa Kamati ya Amani Mkoa wa Ruvuma Fatuma Misango ameunga mkono tamko la viongozi wa dini akisisitiza kuwa kila mpigakura anatakiwa kujua wajibu wake wa kwenda kupiga kura na kurudi nyumbani lengo likiwa ni kudumisha amani ya nchi iliyopo.
Amesema hakuna dini yeyote ambayo inahamasisha upotevu wa amani na kwamba amani ikitoweka ni vigumu kuirudisha hivyo ameshauri kufuata sheria za uchaguzi ili kulinda amani na utulivu wa nchi.
Mbwana Said Mjumbe ni Mjumbe toka Baraza la BAKWATA Mkoa wa Ruvuma amewahimiza watanzania kujitokeza kuwachagua madiwani,wabunge na Rais Oktoba 28 mwaka huu na kuendelea kuhamasisha amani na utulivu.
Naye Mjumbe wa Kamati ya Mahusiano ya Dini toka Kanisa la KKKT Songea, Grace Msuya amesema bila amani na upendo Tanzania haitakuwepo hivyo amesisitiza viongozi wa dini na waandishi wa habari kuwa chachu ya kuhubiri amani na utulivu wakati wote.
“Tukifanya kosa kwenye uchaguzi,tujue tayari tumekosa amani,tusali na tumuombe Mungu atuchagulie viongozi ambao wanastahili ili kuendeleza Tanzania’’,alisisitiza Msuya.