Mjumbe wa chama kikuu cha Ushirika wilaya ya Tunduru Tamcu na mwenyekiti wa mazao wa chama hicho Zainabu Yassin akiongea na Afisa ushirika wa wilaya ya Tunduru Georg Bisani walipotembelea shamba la chama hicho ambalo ni moja kati ya mashamba yaliyoingizwa katika mpango wa mradi mkubwa wa kilimo cha zao la ufuta katika msimu 2020/2021 ambapo jumla ya ekari 3000 zimetengwa.
Afisa kilimo anayeshughulikia mazao wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma Gallus Makwisa kulia, akiwaleza jambo Afisa ushirika wa wilaya hiyo Georg Bisani katikati na Mjumbe wa Chama kikuu cha Ushirika wilayani humo Tamcu Ltd Zainabu Yassin kuhusiana na faida ya zao la ufuta kiuchumi ambapo wilaya hiyo kupitia chama kikuu cha Ushirika Tamcu kinategemea kulima zaidi ya tani 5000 ya zao hilo katika msimu wa kilimo 2020/2021.
Picha zote na Mpiga Picha Maalum
************************************
Na Mwandishi Maalum,
Tunduru
CHAMA Kikuu cha Ushirika wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma(Tamcu) Ltd kimepanga kulima ekari zaidi ya 5000 ya zao la ufuta katika msimu wa kilimo 2020/2021 kama mkakati wa kuviwezesha vyama vya msingi vya ushirika Amcos ambazo ni wanachama wa chama hicho kujitegemea kimapato.
Mjumbe wa chama hicho Zainabu Yasin alisema hayo jana alipokuwa akionesha sehemu ya shamba la ekari 3000 kati ya ekari 5000 katika eneo la Mtetesi kijiji cha Pacha nne kata ya Namiungo kwa waandishi wa habari waliotembelea shamba hilo.
Alisema, shamba hilo lina ukubwa wa ekari 3000 hata hivyo katika msimu huu wanategemea kulima ekari 2000 tu ambapo eneo lililobaki wataendelea kulima mazao mengine ya kimkakati likiwemo zao maarufu la korosho ambalo limekuwa mkubwa mkubwa kwa wakulima.
Alisema, shamba la Namiungo ambalo linamilikiwa na chama kikuu cha Ushirika wilaya ya Tunduru(Tamcu) Ltd lina ukubwa wa ekari 3,104 kati ya hizo ekari 2,000 zitatumika kwa ajili ya mradi.
Alisema, Tamcu ina jumla ya wanachama 38 na hili kufikia malengo ya mradi kimeamua kualika vikundi na baadhi ya taasisi kwa nia ya kuongeza uzalisha na mapato ili kufikia malengo yake.
Kwa upande wake Afisa kilimo anayeshughulikia mazao wa wilaya ya Tunduru Gallus Makwisa alisema, shamba hilo litahudumiwa na makundi mbalimbali kama vyama vya msingi vya ushirika(Amcos) ekari 400,Chama kikuu cha Ushirika Tunduru(Tamcu)ekari 400,shule za msingi ekari 800,sekondari ekari 160 na halmashauri ya wilaya ekari 240.
Alisema,katika msimu wa kilimo 2019/2020 wilaya hiyo ilifanikiwa kulima ekari 9,200 lakini mwaka huu kutokana na kupata mkopo wa zaidi ya bilioni 2 kutoka Benki ya maendeleo ya kilimo Tanzania wameongeza ekari 5000 katika ekari 5000 na zile zilizoongezwa na wakulima lengo ni kufikia ekari elfu 15.5
Alisema, mwaka jana wakulima walizalisha kilo milioni 4 zilizowaingizia wastani wa shilingi bilioni 7 na mategemeo yao msimu 2020/2021 kuongeza uzalisha hadi kifikia tani milioni 7.4 sawa na ongezeko la kilo milioni 4, kutokana na kuongezeka kwa mashamba hasa baada ya baada ya wakulima kuona kilimo cha ufuta kina faida kubwa kwao.
Alisema, mradi huo ufadhiliwa na benki ya kilimo Tanzania ambapo imekubali kutoa zaidi ya shilingi bilioni 2 ambazo zitapitia Chama kikuu cha Ushirika(Tamcu) na wakulima kupitia vyama vya msingi vya ushirika(Amcos) na baadhi ya shule za msingi na sekondari nazo zitahusika katika mradi huo ambao utasaidia sana shule kujitegemea.
Alisema, katika mradi huo utahusisha pia miundombinu yote muhimu ya kilimo kama mashine za kuvunia badala ya wakulima kuvuna kwa njia ya zamani ambayo imekuwa chanzo cha kupunguza ubora wa ufuta.
Kwa mujibu wa Makwisa, katika wilaya hiyo uzoefu unaonesha kuwa, kwa kawaida ekari 1 mkulima anazalisha takribani kilo 450 lakini kutokana na usimamizi mzuri wanategemea uzalishaji kuongezeka kutoka kilo 450 kwa ekari kufikia hadi kilo 600 hadi 700.
Makwisa alitaja faida ya mradi huo ni wanachama kupata elimu ya kilimo bora cha ufuta, kuongeza uzalisha na kupata fedha ambazo zitamaliza kero ya kukopa fedha kwa ajili ya kuendesha shughuli zao za kilimo tena kwa riba kubwa kutoka kwa taasisi za fedha.
Naye Afisa Ushirika wa wilaya hiyo Georg Bisani alisema, kwa jumla mradi huu utasaidia sana vyama vya msingi vya ushirika kuongeza uzalishaji na kipato kitakachoptikana kitawasaidia kuanzisha miradi mingine ya kiuchumi na hivyo kujikwamua na umaskini.
Alitolea mfano ujenzi wa maghala ulioanza kufanywa na baadhi ya vyama ambavyo kwa sasa vinategemea kukodi maghala kwa ajili ya kuhifadhi mazao ya wakulima,lakini kama vitafanikiwa kujenga na kumiliki maghala yao vitapata faida ambayo itawezesha vyama hivyo kujitegemea na kuepuka tabia ya kukopa fedha katika taasisi mbalimbali.
Mwenyekiti wa chama cha msingi cha Ushirika Amcos Namiungo Juma Bakari alisema, amefurahishwa na hatua ya serikali kupeleka mradi huo kwani utasaidia vyama vingi vya msingi kujikwamua kiuchumi na kumaliza kero ya kuomba mkopo.
Alisema, tatizo kubwa katika uendeshaji wa vyama vya ushirika ni pamoja na gharama kubwa ya kusaifirisha mazao ya wanachama kutoka shambani hadi sokoni pamoja na wakati wa maandalizi ya msimu wa kilimo kukosa fedha za kununulia pembejeo jambo linalowakwamisha wakulima wengi.