Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah akiongozana na baadhi ya wakulima wa mwani baada ya kumaliza kutembelea moja ya shamba katika kijiji cha Songosongo, wilayani Kilwa.
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah (kulia) akimkabidhi kamba kwa ajili ya wakulima wa mwani Mwenyekiti wa kijiji cha Songosongo, Bw. Swaluya Sadi (kushoto). Dkt. Tamatamah amekabidhi jumla ya kamba 700,000 zoezi lililofanyika katika kijiji cha Songosongo, wilayani Kilwa. Katikati ni Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji (WMUV), Dkt. Nazael Madalla.
Bi. Mbimbisa Omary ambaye ni mkulima wa mwani akitoa neno la shukrani kwa niaba ya wakulima wa mwani wa kijiji cha Songosongo kwa Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah (aliyevaa tisheti nyeusi) kutokana na wakulima hao kupatiwa kamba 700,000 na Wizara ya Mifugo na Uvuvi – Sekta ya Uvuvi.
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah akizungumza na wakulima wa mwani pamoja na wananchi wa kijiji cha Songosongo wilayani Kilwa (hawapo pichani) wakati alipokwenda kukabidhi kamba kwa wakulima hao.
Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Songosongo waliofika kwenye mkutano kumsikiliza Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah wakati alipotembelea Kijiji hicho kwa ajili ya kugawa kamba kwa wakulima wa mwani.
………………………………………………………………………………..
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah amekabidhi vipande vya kamba za manila 700,000 kwa wakulima wa mwani katika Kijiji cha Songosongo, wilayani Kilwa, mkoa wa Lindi.
Akizungumza na wananchi wa Songosongo jana Dkt. Tamatamah amesema serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Sekta ya Uvuvi) imetoa kamba hizo ili kuwawezesha wakulima wa mwani kwani kamba ilikuwa ni moja ya changamoto waliyokuwa wakikabiliana nayo.
Kamba hizi za manila (ambazo kila moja ina urefu wa mita 10) katika kilimo cha mwani, hufungwa katika vigingi na hutumika kwa ajili ya kuoteshea mwani ambapo mwani hufungwa katika kamba hizo zinazosaidia pia mwani kutochukuliwa na maji ya bahari pale panapokuwepo na wimbi.
Dkt. Tamatamah amesema duniani kote kwa sasa mwani unalimwa kibiashara, hivyo mwani ni moja ya zao linalopewa kipaumbele katika wizara. Katika kilimo cha mwani wakulima wanakutana na changamoto mbalimbali zikiwemo za ukosefu wa mitaji na masoko.
“Wizara kupitia sekta ya uvuvi imeanza kutoa kamba ambazo ni moja ya pembejeo muhimu kwa wakulima wa mwani ikiwa ni sehemu ya kuwawezesha wakulima hao kwa kuwapunguzia sehemu ya gharama za uzalishaji ili baadae waweze kusimama wenyewe,” alisema Dkt. Tamatamah.
Pia amesema kuwa kama wakulima watalima vizuri katika kamba moja ya mita kumi katika bamvua nne (miezi miwili) wanaweza kupata kati ya kilo 8-10, na kamba hizo walizopewa zinaweza kutumika kwa mwaka mzima. Lengo la wizara ni kusambaza kamba hizi kwa wakulima wa mwani maeneo yote Tanzania Bara.
Dkt. Tamatamah amesema kuwa ipo changamoto ya soko la mwani hasa kwenye bei kwani kwa sasa asilimia 90 ya mwani inauzwa nje ikiwa ghafi na ni asilimia 10 tu ndio inayotumika hapa nchini.
Hivyo wizara kwa sasa inawahamasisha wakulima kujiunga katika vikundi na kuwaunganisha na taasisi za kifedha ili waweze kukopesheka na waweze kuanzisha viwanda vidogo vya kuchakata mwani ili kuuongezea thamani. Hii itasaidia kupunguza kiasi cha asilimia ya mwani inayokwenda nje ya nji ikiwa ghafi na kusaidia kuongeza ajira.
Aidha, Katibu Mkuu Tamatamah amesema zao la mwani linazo faida kubwa ikiwa ni pamoja na kuongeza kipato katika jamii za maeneo ya pwani hasa kwa akina mama, inaodoa umaskini lakini pia linaingiza fedha za kigeni.
Naye mkulima wa mwani, Bi. Mbimbisa Omary amemshukuru Katibu Mkuu Tamatamah kwa kuwaletea vitendea kazi kwa ajili ya kilimo cha mwani. Bi. Mbimbisa amesema kilimo cha mwani kinawasaidia mambo mengi ikiwa ni pamoja na kuwasomesha Watoto, kununua chakula pamoja na ujenzi wa nyumba.
Bi. Jaka Farahani ambaye ni mkulima wa mwani amesema changamoto ya masoko inawasumbua sana hasa pale wanunuzi wanaowategemea wasiponunua hivyo ameiomba wizara kuwasaidia kutatua changamoto hiyo. Lakini pia amemuomba Katibu Mkuu kuendelea kuwapelekea kamba nyingi zaidi kwa kuwa eneo la kulima ni kubwa na wakulima wapo wengi.
Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji (WMUV), Dkt. Nazael Madalla amesema wizara kupitia idara yake inaendelea kuhamasisha kampuni kuendelea kuchukua leseni kwa ajili ya kununua mwani na mpaka sasa zipo kampuni 7. Lengo la kuwa na kampuni nyingi ni kuongeza ushindani hivyo kampuni zinahamasishwa kujisajili ili zitambulike na ziweze kufanya biashara ya mwani.
Zao la mwani hapa nchini Tanzania lilianza kulimwa miaka ya 1980 na lilianzishwa katika kisiwa cha Zanzibar. Baada ya kufanikiwa katika kipindi cha majaribio, miaka ya 1990 mpaka 2000 Tanzania hususani Zanzibar ilikuwa ni nchi ya kwanza duniani kwa uzalishaji wa mwani. Lakini kutokana na changamoto mbalimbali kwa sasa Tanzania ni nchi ya tatu kwa uzalishaji wa mwani ambapo nchi ya kwanza ni Ufilipino ikifuatiwa na Indonesia.