MGOMBEA Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) Dk.Hussein Ali Mwinyi, akizungumza na walimu wa shule za msingi na sekondari (hawapo pichani) za Unguja huko katika ukumbi wa Kituo cha uangalizi wa Wazee Sebleni Zanzibar.
BAADHI ya Wazanzibar wanaishi nje ya nchi wakisikiliza nasaha za Mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM Dk.Hussein Ali Mwinyi katika ziara zake kampeni za kuzungumza na makundi ya wananchi huko katika ukumbi wa Hoteli ya Park Hytt Zanzibar.
…………………………………………………………………………….
IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.
MGOMBEA wa nafasi ya urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi(CCM) Dk.Hussein Ali Mwinyi amesema akipata ridhaa ya kuiongoza Zanzibar serikali atakayoiongoza itahakikisha inaboresha mazingira ya walimu visiwani Zanzibar.
Dk.Mwinyi amesema miongoni mwa mambo serikali atakayoiongoza itaboresha mazingira kwa walimu hao ikiwemo kuongeza posho kwa walimu wakuu,kuwapandisha madaraja walimu.
Kauli hiyo ameitoa jana wakati akizungumza na walimu shule za Msingi na Sekondari mjini Unguja ikiwa ni mwendelezo wa ziara zake za kukutana na makundi mbalimbali.
Dk.Mwinyi alisema akipata ridhaa ya kuiongoza Zanzibar serikali atakayoiongoza itahakikisha inalishughulikia suala la nyongeza za posho hizo kutokana na kuwa posho inayotolewa hivi sasa ni ndogo.
“Sioni tatizo kuongeza posho kwa walimu kwa walimu wa kuu hawa kama serikali itakuwa na uwezo wa fedha kwa mujibu wa taarifa za Chama Cha Walimu Zanzibar(ZATU) inaonyesha kuwa ombi hili lilikuwa limekubalika lakini utekelezaji wake ulikuwa bado kutokana na covid-19 hivyo nitalishughulikia,”alisema
Alisema jambo hilo kwa upande wake halitoliona tabu kutokana na kuwa posho inayotolewa hivi sasa ni ndogo na kwamba serikali ikiwa na uwezo hakuna sababu ya posho hizo zisiongezwe.
Dk.Mwinyi alisema akipata ridhaa ya kuiongoza Zanzibar serikali atakayoiongoza itahakikisha inawapandisha madaraja walimu na kwamba ni jambo muhimu sana.
“Na hapa suala la kuwepo kwa Tume ya utumishi wa walimu ndio litafanya kazi vizuri haiwezekani mwalimu aliyefanya kazi miaka 10 anaingia mwingine kijana leo anakuwa sawa sawa kwa kila kitu,”alisema
Alisema kuhusu suala la walimu kutolipwa posho zao kwa wakati wanapokwenda safari za kikazi katika maeneo ya Unguja na Pemba amelipokea na atalifanyia kazi akipata ridhaa ya kuiongoza Zanzibar.
Dk.Mwinyi alisema akipata ridhaa ya kuiongoza Zanzibar serikali atakayoiongoza itahakikisha inaiagiza Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kukutana mara kwa mara na Chama cha Walimu angalau mara mbili kwa mwaka.
“Sasa mimi ninapo wateua watendaji ambao hawakutani na watu wanaowaongoza kiukweli utakuwa huongozi sababu hatakuwa anafanya mambo ambayo anayoyataka yeye wadau hujui wanataka nini yaani mara mbili kwa mwaka kuna ukubwa gani sasa haya tutayaweka sawa na mrejesho ufike kwa Rais,”alisema
Alisema kuhusu suala la mikopo ya elimu ya juu kwa walimu amelipokea na kwamba kuna haja ya kuhakikisha walimu walioajiriwa wanapewa mikopo hiyo ikilinganishwa na ilivyo sasa ambapo wanapewa wasioajiliwa.
“Mimi kwa maoni yangu mimi nitakaowateua katika nafasi nitahakikisha wanafanya mapitio ya sheria na sera za elimu ili kuleta tija kwenye sekta hii muhimu ambapo sheria hii ya elimu imepitwa na wakati ambapo ni ya mwaka 1982 na imepitiwa mwaka 1986 hivyo kuna mambo yatakuwa yamepitwa na wakati lazima yafanyiwe marekebisho,”alisema
Akimuelezea changamoto za walimu wanazokutanazo walimu wa shule za Msingi na Sekondari Katibu Mkuu wa Chama Cha Walimu Zanzibar (ZATU),Mussa Omar Tafurwa alisema kuna haja ya serikali atakayoiongoza ihakikishe inapitia upya sera ya elimu ambayo ilipitiwa mwaka 2006.
Alisema kuanzia mwaka huo ambao sera hiyo imepitiwa ikianaza kutumika mwaka 2010 na kwamba mpaka hivi sasa kuna maeneo ambayo yametekelezwa na kuna maeneo hayajatekelezwa na kuna maeneo ambayo si muhafaka kwa sasa.
Katibu huyo alisema katika sera ya elimu kifungu namba sita
imelezwa kuwa kwa wakati huo ilikubali kuwepo kwa asilimia 10 ya walimu ambao hawajapata mafunzo ya ualimu kwa maana hawana taaluma ya ualimu kutokana na kuwa kipindi hicho kulikuwa na uhaba wa walimu.
“Moja ya kilio cha muda mrefu wa walimu Zanzibar ni upandishwaji wa madaraja wa kiutumishi kuna wakati miaka minne iliwahi kutoka barua Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali lakini ikaonekana kuna mapungufu na hatimaye zikafutwa barua hizo zote sasa madaraja yanajenga heshima hivyo tunaomba walimu tupandishwe daraja,”alisema
Alisema jambo lingine ambalo walimu wanaomba kupewa bima ya afya na kwamba gharama za huduma za matibabu ya afya zinawasumbua sana walimu.
Katibu huyo alisema Kilio chingine kinachowasumbua walimu ni malipo ya walimu wanapokwenda kwenye safari zao za kutekeleza majukumu yao ya kikazi hasa wanapo safiri kwenda Unguja na Pemba.
Katibu Mkuu huyo alisema ZATU ilimuomba Rais Dk.Ali Mohamed Shein kuongezewa posho za walimu wakuu na kwamba hoja ya chama ilikuwa ni kuwa mwalimu mkuu anakuwa na dhamana ya wanafunzi zaidi ya 300.
Alisema hoja nyingine ya walimu hao wakuu kupewa posho hiyo ni kuwa walimu hao wanapewa vitu vyenye thamani kubwa katika shule zao wanazozisimamia.
“Posho za walimu hao wakuu ni sh.40,000 huku kwa walimu wakuu wa shule za Msingi na Maandalizi wanapewa sh.2,5000 kwa hivyo tulikuwa tunaomba Dk.Mwinyi ukipata ridhaa ya kuiongoza Zanzibar serikali atakayoiongoza iongeze posho angalau asilimia 15 ya mshahara wake,”alisema
Kwa upande wake Rais wa ZATU, Seif Mohamed Seif alisema kazi ya walimu imekuwa ni miongoni mwa kazi ambazo zimekuwa zikidhalilishwa na kwamba kuna haja ya kuhakikisha maslahi ya walimu yazingatiwe.
“Wapo baadhi ya viongozi na wananchi wamekuwa hawaoni umuhimu wa walimu ambapo imejionyesha katika kipindi ambacho kulikuwepo ugonjwa wa covid-19 walidai walimu wasilipwe mishahara kutokana na kuwa hawakuwa wanakwenda kazini lakini Rais wa Zanzibar Dk.Ali Mohamed Shein aliona umuhimu wa walimu na kuamua kuendelea kuwalipa mishahara walimu,”alisema
Rais huyo wa ZATU alimuomba Dk.Mwinyi pindi akipata ridhaa ya kuiongoza Zanzibar ahakikishe serikali atakayoiongoza inaishirikisha chama hicho cha walimu hatua kwa hatua ikilinganishwa na kipindi cha hivi sasa walimu wamekuwa wakiamuliwa mambo yao.
Katika hatua nyingine akizungumza na wanzanzibar wanaoishi nje ya nchi ‘wanadiaspora’ Dk.Mwinyi alisema serikali atakayoiongoza itahahakisha inawashirikisha wanadiaspora hao katika kuleta mageuzi makubwa ya uchumi wa Zanzibar.
Alisema katika serikali ambayo atakayoiongoza wanadiaspora watakuwa ni sehemu ya watakaoleta mageuzi hayo ikiwemo kuwatumia katika kuwaleta wawekezaji wa kutoka nje ya nchi.
“Bado tunawahitaji wanadiaspora kuja kuwekeza Zanzibar na kwamba mnaweza kuja kuwekeza nyinyi wenyewe lakini pia mnaweza kutusaidia kuwaleta wawekezaji kwa kuzungumzanao na jambo lingine ni fedha zenu mnazozipata huko aidha ukiwa mfanyabiashara muajiriwa muone muhimu wa kuja kuwekeza Zanzibar,”alisema
Dk.Mwinyi alisema ahadi ya serikali atakayoiongoza itakuwa ina kazi ya kulinda maslahi ya vitu ambavyo wanadiaspora watakuwa wamewekeza visiwani Zanzibar kwa maana ya kuwawezesha kupata haki zao wanazostahili.
Alisema katika hatua hiyo ambayo serikali atakayoiongoza kuleta mageuzi makubwa ya uchumi wa Zanzibar itajikita katika uchumi wa bahari na utalii kutokana na kuwa bado visiwa vya Zanzibar havijatumika vizuri kwenye utalii.
Katika maelezo yake Dk.Mwinyi alisema utalii unaofanyika kwa sasa ni wa aina moja wa fukwe na kwamba bado hajakuwa na utalii wa kutosha hivyo kuna haja ya kuwa na utalii wa kisasa wenye kuleta uchumi mkubwa.
Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa(SUKI) wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Zanzibar, Kombo Hassan Juma alisema chama kinatoa shukrani kubwa kwa wanadiaspora hao ambao waliojitokeza kuzungumza na Dk.Mwinyi na kutoa maoni yao juu ya serikali atakayoiongoza iweje.
Alisema lengo na kukutana na wanadiaspora hao ni kutoa maoni yao mambo gani wangependa yafanywe pindi akipata ridhaa ya kuiongoza Zanzibar.
Kwa upande wake Ali Mbamba mwanadispora anayeishi Denmark, alimuomba Dk.Mwinyi pindi akiongoza Zanzibar kuikuza idara ya Diaspora na ikiwezekana iwe Wizara kamili na kwamba kwa kufanya hivyo itasaida kuwashughulikia wana diaspora mambo yao.
Alimuomba Dk.Mwinyi kuwa akipata ridhaa ya kuiongoza Zanzibar serikali atakayoiongoza iahakikishe Idara ya Diaspora inandelea kutoa elimu kwenye taasisi za serikali katika kuwatambua diaspora kwenye suala la ajira.
“Ni ngumu sana kwa diaspora kupata ajira nchini licha ya kuwa ni wazaliwa wa Zanzibar lakini wanakosa kutambulikana kama ni wazanzibar,”alisema
Kwa upande Mohammed Kassim Mohammed mwanadiaspora anayeishi Saudi Arabia alimuomba Dk.Mwinyi akipata ridhaa ya kuiongoza Zanzibar awapatiie kipaumbele wanadiaspora hao katika kukodi majengo ya serikali kutokana na kuwa kukodi nyumba za watu binafsi huwa wanapata changamoto kubwa.
“Ninaomba serikali utakayoiongoza iwape nguvu idara ya Diaspora kwenye mabalozi wa nchi ambazo wanatoka ili kuweza kujua changamoto zao au vitu muhimu ambavyo wanahitaji kuwa navyo ili viweze kupatikana kwa haraka,”alisema