Katibu Mkuu wa Chama Cha Upinzani nchini Tanzania National League for Democracy (NLD) Bw. Tozy Matwanga akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
……………………………………………………………………………….
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM.
Chama Cha Upinzani nchini Tanzania National League for Democracy (NLD) kimewaomba watanzania kujiepusha na wanasiasa wanaotumia lugha za uchochozi katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 28 mwaka huu .
NLD imeonesha msimamo wake kuwa hawana mpango wa kushirikiana na vyama vyingine vya upinzani kama ilivyokuwa katika uchaguzi wa mwaka 2015 kwa sababu hawaoni faida zaidi ya kuwanufaisha baadhi ya vyama.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Katibu Mkuu wa Chama Cha NLD Tanzania Bara Tozy Matwanga alisema anampongeza Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli baada kufuraishwa na utendaji kazi wake ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya barabara.
‘’Rais amefanya mambo mengi mazuri katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wake” amesema Bw. Matwanga.
Alisema NLD wamepinga kauli ya Makamo Mwenyekiti upande wa Zanzibar Bw. Hamadi Hemedi ambaye aliyedai kuwa watamuunga mkono mgombea wa urais wa Chama cha ACT- Wazalendo Maalim Seif Sharifu Hamadi.
Chama hicho kimeeleza kuwa msimamo wao watampigia kura mgombea wao Mfalme Hamisi Hassan katika nafasi ya urais Zainzbar katika uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 28 mwaka huu.
Katibu huyo wa NLD alisema Oktoba 18(Jana) mwaka huu, kamati kuu watakaa kikao kwa ajili ya kumpa nafasi Bw. Hemedi aweze kujieleza kwa sababu gani ametangaza kumuunga mkono maalim seif bila kuwa na makubaliano na uongozi wa chama.
Katika hatua nyengine amebainisha kwa sasa Mwenyekiti wa Chama cha NLD Taifa ni Bw. Mfalme Hamisi Hassan na sio Bw. Oscar Makaidi kama ilivyokuwa inafahamika na watu wengine.
Bw. Matwanga amesitiza zaidi wananchi kufikiria zaidi watakapo kwenda kwenye sanduku la kupigia kura .
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Idara ya vijana Taifa Chama cha NLD Othiniel Mizizi, alisema kuwa wamejipanga kikamilifu kushiriki uchaguzi mkuu pamoja na kuendelea kuomba kuwe na amani katika uchaguzi huo.