Kamishna Msaidizi wa Ardhi mkoa wa Tabora Jabir Singano akifafanua jambo wakati akielezea utendaji kazi wa sekta yake tangu kuanzishwa kwa Ofisi za Ardhi za Mikoa mapema mwaka huu ikiwa ni makakati wa serikali ya awamu ya tano kusogeza huduma ya sekta za ardhi kwa wananchi.
Kamishna Msaidizi wa Ardhi mkoa wa Tabora Jabir Singano (kulia) akionesha eneo la wazi la Kata ya Mpera katika Manispaa ya Tabora kwenye Ramani wakati wa zoezi la kutambua maeneo ya wazi na kukabidhi Ramani na kuonesha mipaka ya maeneo hayo kwa watendaji kata mkoani Tabora mwishoni mwa wiki ikiwa ni makakati wa ofisi hiyo kulinda maeneo ya wazi yasivamiwe. Wa pili kulia ni Mtendaji wa Kati ya Mpera katika Manispaa ya Tabora Grace Kasegezya.
Kamishna Msaidizi wa Ardhi mkoa wa Tabora Jabir Singano (kulia) akisisitiza jambo kwa Maafisa wa Ofisi yake na Mtendaji wa Kata ya Mpera Grace Kasegezya (wa pili kulia) wakati wa kuanza zoezi la kutoa elimu na kuhamasisha ulipaji kodi ya pango la ardhi katika Manispaa ya Tabora mkoani Tabora mwishoni mwa wiki.
Afisa kutoka ofisi ya Ardhi mkoa wa Tabora Evod Kerete akimuelimisha mmoja wa wakazi wa Kata ya Mpera Manispaa ya Tabora wakati wa zoezi la kuhamasisha ulipaji kodi ya ardhi na utoaji elimu kuhusiana na masuala ya sekta ya ardhi mkoa wa Tabora mwishoni mwa wiki.
Afisa kutoka Ofisi ya Ardhi mkoa wa Tabora Evod Kerete (wa pili kushoto) na Afisa Ardhi Mteule Manispaa ya Tabora Daud Msinde (kushoto) wakimpatia Ankara ya malipo ya kodi ya pango la ardhi mmoja wa wakazi wa Kata ya Mpera Manispaa ya Tabora wakati wa zoezi la kuhamasisha ulipaji kodi ya ardhi na utoaji elimu kuhusiana na masuala ya sekta ya ardhi mkoa wa Tabora mwishoni mwa wiki. (PICHA ZOTE NA MUNIR SHEMWETA WIZARA YA ARDHI)
……………………………………………………………………………………..
Na Munir Shemweta, WANMM TABORA
Ofisi ya Ardhi mkoa wa Tabora imeanza mkakati wa kuyatambua maeneo yote ya wazi katika halmashauri za mkoa wa Tabora na kugawa ramani za maeneo hayo kwa Watendaji wa Kata ili kuyalinda maeneo hayo yasiweze kuvamiwa.
Hayo yamebainishwa mwishoni mwa wiki mkoani Tabora na Kamishna Msaidizi wa Ardhi mkoa wa Tabora Jabir Singano wakati akielezea utendaji kazi wa ofisi yake tangu kuzinduliwa rasmi mapema mwaka huu na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ikiwa ni mkakati wa Serikali kusogeza huduma za sekta ya ardhi karibu na wananchi.
Alisema, katika mkoa wa Tabora kumekuwa na tabia ya uvamizi wa maeneo ya wazi katika halmashauri za mkoa huo na katika kukabiliana na tatizo hilo ofisi yake imeanza mkakati wa kuyatembelea maeneo yote ya wazi katika halmashauri za mkoa huo na kuanza na Manispaa ya Tabora wakiwa na watendaji Kata ili kuyatambua na kuwaonesha mipaka sambamba na kuwakabidhi ramani ili kuyalinda.
” Moja ya kitu nilichoelezwa na ofisi ya Katibu Tawala mkoa wa Tabora wakati ofisi yetu inaanza kazi ni suala la uvamizi maeneo ya wazi hivyo tumeamua kulifanyia kazi kwa kuyatambua maeneo ya wazi na kugawa ramani za maeneo hayo kwa watendaji wa kata ili waweze kuyalinda na tumeanza na Manispaa ya Tabora na baadaye tutaendelea na halmashauri nyingine” alisema Singano.
Aidha, Singano alisema mpango mwingine wa ofisi yake ya Ardhi katika kuboresha sekta ya ardhi mkoani Tabora ni kukagua maeneo yote ya umma na kuanza na yale maeneo ya shule za msingi na sekondari kwa kubainisha mipaka ambapo alisema lengo ni kuhakikisha maeneo yote ya umma hayavamiwi wakati ofisi ya ardhi mkoa ipo.
Kwa upande wake Mtendaji wa Kata ya Mpera Manispaa ya Tabora Grace Kasegezya aliishukuru ofisi ya ardhi mkoa wa Tabora kwa kuanza zoezi la utambuzi maeneo ya wazi na kuwapatia ramani zinazoonesha maeneo ya wazi Watendahi katika Kata za Manispaa ya Tabora.
Alisema, kuoneshwa mipaka na kupatiwa ramani za maeneo ya wazi katika kata siyo tu kutawasaidia watendaji wa Kata kutambua maeneo ya wazi bali kutawawezesha pia kama Watendaji kuyafuatilia na kuyalinda dhidi ya uvamizi unaoweza kufanywa.
“Huu mpango unaofanywa na ofisi ya Ardhi mkoa wa Tabora wa kutambua maeneo ya wazi na kutupatia ramani za maeneo hayo utatusaidia sana kuyatambua na kuyalinda hivyo niishukuru ofisi ya Kamishna wa Ardhi mkoa wa Tabora kwa kuanzisha zoezi hilo. Alisema Mtendaji Kata ya Mpera Grace.
Katika hatua nyingine Ofisi ya Ardhi mkoa wa Tabora imeendesha zoezi la kutoa elimu na kuhamasisha ulipaji kodi ya pango la ardhi katika mitaa mbalimbali ya Manispaa ya Tabora.
Zoezi hilo limeogozwa na Kamishna Msaidizi wa Ardhi mkoa wa Tabora Jabir Singano kwa kushirikiana na Maafisa kutoka ofisi yake ya mkoa, halmashari ya Manispaa ya Tabora na Mtendaji wa kata ya Mpera Grace Kasegezya.
Uhamsishaji ulipaji kodi ya pango la ardhi na utoaji elimu kuhusiana na masuala ya ardhi ulianzishwa na Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa lengo kujua changamoto zinazowakabili wamiliki wa ardhi katika masuala yanayohusu sekta ya ardhi na hufanyika kila siku ya ijumaa.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo la kuhamasisha utoaji kodi ya pango la ardhi Kamishna wa Ardhi mkoa wa Tabora Jabir Singano alisema, zoezi hilo linafanyika kwa kupita katika mitaa ya Manispaa ya Tabora na kuhamasisha wamiliki wa ardhi kulipa kodi sambamba na kupokea changamoto za sekta ya ardhi.
Kwa mujibu wa Singano, pamoja na ofisi yake kupita mtaa kwa mtaa kuhamasisha kodi lakini pia inahakikisha inaingiza kumbukumbu za wamiliki wa ardhi katika mfumo wa kodi ili kuhakikisha wamiliki wote wanaingizwa kwenye mfumo na kuendelea kulipa kodi.
‘’Moja ya mikakati wakati wa kutoa elimu kuhusiana na kodi ya pango la ardhi ni kuwaeleza wamiliki muhimu na kulipa kodi mapema ili kuepuka tozo ya adhabu inayoweza kuchangia wamiliki wa ardhi kushindwa kulipa’’. Alisema Singano