Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi akimkabidhi zawadi ya picha yenye mchoro wa tingatinga daktari bingwa wa wagonjwa walioko katika chumba cha uangalizi maalum (ICU) kutoka nchini China Cui Jian ikiwa ni ishara ya kumshukuru baada ya kumaliza muda wake wa kufanya kazi katika Taasisi hiyo. Mwezi wa sita mwaka 2018 Serikali ya China ilitoa madaktari bingwa 11 kuja kufanya kazi hapa nchini wakiwemo madaktari bingwa watatu wa magonjwa ya moyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi akimkabidhi zawadi ya ngao yenye ramani ya Tanzania daktari bingwa wa magojwa ya moyo kwa watoto kutoka nchini China Zhao Lijian ikiwa ni ishara ya kumshukuru baada ya kumaliza muda wake wa kufanya kazi kwa zaidi ya miaka miwili katika Taasisi hiyo. Katikati ni kiongozi wa madaktari hao ambaye pia ni Daktari bingwa wa usingizi QinChengwei anayefanya kazi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi akimkabidhi zawadi ya ngao yenye ramani ya Tanzania na cheti daktari bingwa wa upasuaji wa moyo kutoka nchini China Hu Bin ikiwa ni ishara ya kumshukuru baada ya kumaliza muda wake wa kufanya kazi kwa zaidi ya miaka miwili katika taasisi hiyo. Kulia ni kiongozi wa madaktari hao ambaye pia ni Daktari bingwa wa usingizi Qin Chengwei anayefanya kazi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
Kiongozi wa madaktari kutoka nchini China ambao wanafanya kazi hapa nchini ambaye pia ni Daktari bingwa wa usingizi Qin Chengwei katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) akiishukuru menejimenti ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa jinsi walivyoshirikiana na Madaktari bingwa wa magonjwa ya moyo watatu ambao wamefanya kazi katika Taasisi hiyo kwa zaidi ya miaka miwili.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi pamoja na wafanyakazi wa taasisi hiyo wakiwa katika picha ya pamoja na madaktari bingwa wa moyo kutoka nchini China mara baada kumaliza kuwaaga kutokana na muda wao wa kufanya kazi kwa zaidi ya miaka miwili katika Taasisi hiyo kumaliza. Mwezi wa sita mwaka 2018 Serikali ya China ilitoa madaktari bingwa kuja kufanya kazi hapa nchini wakiwemo madaktari bingwa watatu wa magonjwa ya moyo.Madaktari Bingwa wa magojwa ya moyo kutoka nchini China wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kuagwa na Menejimenti ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) ambako walikuwa wanafanya kazi kwa zaidi ya miaka miwili. Mwezi wa sita mwaka 2018 Serikali ya China ilitoa madaktari bingwa 11 kuja kufanya kazi hapa nchini wakiwemo madaktari watatu wa magonjwa ya moyo.
Picha na JKCI
********************************
Na Mwandishi Maalum – Dar es Saam
Oktoba 16, 2020 Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), imewaaga madaktari bingwa watatu wa magonjwa ya moyo ambao walitolewa na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kuja Tanzania kutoa huduma za matibabu ya moyo.
Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kila baada ya miaka miwili huwa inatoa wataalamu wake kwenda nchi mbalimbali Barani Afrika kutoa huduma za matibabu.
Madaktari hao akiwamo daktari bingwa wa wagonjwa walioko katika chumba cha uangalizi maalum (ICU), daktari bingwa wa magojwa ya moyo kwa watoto na daktari bingwa wa upasuaji wa moyo walikuwapo nchini baada ya kusainiana makubaliano hayo kati ya Serikali yao na Tanzania kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.
Akizungumza wakati wa hafla ya kuwaaga madaktari hao mapema hii leo, Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Profesa Mohamed Janabi, amesema madaktari hao wamemaliza muda wa kufanya kazi nchini.
“Walikuwapo kwa kipindi cha miaka miwili tangu tarehe 22 Juni, 2018 hadi kufikia mwaka huu.
“Wanatarajia kurudi nchini kwao katikati ya mwezi Oktoba, mwaka huu,tumejifunza mengi kutoka kwao, tumeshirikiana nao kwa ukaribu, niliwaona ni sehemu ya timu yetu ya wataalamu mabingwa wa JKCI,” amesema.
Ameongeza “Wanarudi nchini kwao, tutaendelea kuwakumbuka kwa kazi nzuri waliyofanya pamoja nasi, hakika walishirikiana nasi kwa ukaribu , wameshakamilisha taratibu za kusafiri kurudi China.
“Wanapoondoka tunatarajia timu nyingine ya wataalamu kutoka China ambao wameshakamilisha taratibu za kuja nchini, tutaungana nao kuendelea kuimarisha huduma zetu,” amebainisha.
Akizungumza kiongozi wa timu hiyo ya madaktari kutoka China, waliokuja nchini kushirikiana na JKCI, Dk. Qin Chengwei, amesema kipindi hicho ya mashirikiano kimekuwa chenye manufaa kwa pande zote mbili.
“Binafsi naona miaka miwili imeisha haraka mno, mmeshirikiana vizuri mno na wataalamu wetu, tunashukuru, kwa zaidi ya miaka 50 sasa Serikali yetu imekuwa ikituma madaktari nchi mbalimbali za Afrika.
“Tunaahidi kuendelea kushirikiana na kuipa kipaumbele Tanzania, Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete, kuendelea kuleta wataalamu wetu kufanya nao kazi,” amesema.
Mmoja wa madaktari hao ambaye ni daktari bingwa wa upasuaji wa moyo Hu Bin ameshukuru uongozi wa Taasisi hiyo na wafanyakazi wote kwa kufanya nao kazi vizuri na kwa ukaribu katika kipindi chote walichoishi nchini.
“Niliishi hapa kama nyumbani, mmekuwa nasi katika nyakati zote, kila hatua, hakika niliona JKCI ni hospitali yangu, ya maisha yangu,” amesema.