MGOMBEA Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM Dk.Hussein Ali Mwinyi, akizungumza katika mkutano wa kampeni za CCM Wilaya ya micheweni.
BAADHI ya Wanachama wa CCM wakisikiliza sera na nasaha za viongozi wakuu wa Chama Cha Mapinduzi.
MAKAMU Mwenyekiti wa CCM Zanzibar ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi(CCM),akiwanadi wagombea wa CCM kwa nafasi za urais,ubunge,uwakilishi na udiwani huko Wilaya ya micheweni Pemba.
…………………………………………………………………………………………..
NA IS-HAKA OMAR,PEMBA.
MGOMBEA Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM Dk.Hussein Ali Mwinyi akipata ridhaa ya wananchi na kuwa rais,atapandisha hadhi hopitali ya michweni na kuwa hospitali ya Wilaya sambamba na kuwaajiri madaktari bingwa ili wananchi wapate huduma bora za afya.
Ahadi hiyo ameitoa katika mwendelezo wa mikutano ya kampeni ya CCM ya kuwanadi na kuwaombea kura wagombea wa CCM katika uwanja wa mikutano wa Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Alisema ataimarisha sekta ya afya kwa kuongeza ununuzi wa dawa na kuajiri wataalamu mbalimbali wa sekta ya afya.
Alieleza kuwa ili wananchi washiriki kikamilifu katika shughuli za ujenzi wa nchi, ni lazima wawe na afya bora pia na vyanzo vya mapato vya uhakika.
Ameahidi wakulima wa mazao ya karafuu na mwani kuwa endapo atachaguliwa kuwa rais, atajenga viwanda vikubwa kwa ajili ya kusanifu zao hili ili liongezeke thamani na kuwanufaisha wakulima hao.
Kwa upande wa sekta ya elimu aliahidi kuajiri walimu wa masomo ya sayansi na kujenga shule za kisasa ili kuongeza ufaulu kwa wanafunzi nchini.
Alisema vipaumbele vyake katika serikali ijayo ataendeleza pale serikali ya sasa itakapoishia.
Katika sekta ya kilimo atahakikisha panajengwa matuta makubwa ya kuzuia maji ya bahari kuingia katika mashamba ya wananchi.
Pia atahakikisha mabibi shamba na mabwana shamba wanawafikia wakulima wa mazao mbalimbali kwa lengo la kutoa mafunzo na kuwasaidia Pembejeo.
Alisema katika kulinda mazingira atawapatia kazi mbadala vijana wanaochonga matofali na kusababisha uharibifu wa mazingira kwa kuwapatia mitaji na mikopo ili wafanye kazi zingine.
Atawapatia vifaa vya kisasa na mikopo wavuvi wa maeneo mbalimbali ili wafanye uvuvi wenye tija.
Alieleza kwamba moja ya vipaumbele vyake ni kuinua wajasiriamali kwa kuwapatia mikopo,mafunzo na kuwatafutia soko la bidhaa zao ili kuongeza thamani ya bidhaa zao.
Alisema atajenga viwanda vikubwa vitakavyotoa ajira nyingi kwa vijana wengi ambao wamesoma na wale wenye ulimu ya kawaida watapewa mafunzo ya amali.
Aliwataka wananchi na wana CCM kwa ujumla kulinda amani nchini na kuepuka kutumiwa na wanasiasa waohubiri machafuko na migogoro.
Alitumia mkutano huo kuwaombea kura wagombea wote wa CCM wa nafasi za urais,ubunge,uwakikishi na udiwani.
Dk.Mwinyi alisema kuwa serikali ya awamu ya saba imejenga skuli za kisasa za Wingwi na Micheweni zenye vifaa vya kisasa vya masomo ya sayansi.
Alisema elimu ya msingi na sekondari zinaendelea kutolewa bure bila ya malipo.
Alisema wakulima wa mazao ya karafuu na mwani wameendelea kunufaika kwa kuuza mazao yao kwa gharama inayokidhi mahitaji yao.
Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein, amewataka wananchi wa kisiwani pemba kuwapigia kura wagombea wa CCM ili waendeleze mambo mema yaliyoasisi na serikali ya awamu ya saba.
Alisema Dk.Mwinyi, ndiye mgombea urais pekee wa Zanzibar mwenye sifa ya kulinda muungano na Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964.
Alimtaja Dk.Mwinyi kuwa ni msomi wa fani ya udaktari wa moyo hivyo ana uwezo na uzoefu mkubwa katika kujali utu na maisha ya wananchi wote bila ubaguzi.
Alisema Dk.Mwinyi amekuwa kiongozi aliyehudumu kwa miaka mingi serikali kwa uadilifu mkubwa na mchapa kazi.
Alisema mgombea huyo aliyeteuliwa na CCM apeperushe bendera ni mmoja wa viongozi wenye sifa ya uadilifu,mpole na mbunifu kiutendaji.
“Dk.Mwinyi,ni mtu makini asiyependa kukurupuka ama kusema sema ovyo kama walivyo baadfhi ya wagombea wa vyama vingine vya kisiasa,,,,lakini pia bado ni kijana anayehimili mbio za utendaji wa nafasi ya urais bado umri wake unamruhusu.”,alisema Dk.Shein.
Alisema Zanzibar imepiga hatua kubwa za maendeleo kupitia utekelezaji mzuri wa ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020, na kwamba chama kimejipanga kuendelea kutekeleza ilani mpya ya mwaka 2020/2025.
Kupitia mkutano huo Dk.Shein,aliwanadi na kuwaombea kura sambamba na kuwakabidhi Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020/2025.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Mabodi,alisema kuwa CCM imeendelea kufanya kampeni za kisitaarabu kwa kueleza namna kitakavyotekeleza sera zake kwa vitendo.
Alieleza kuwa mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM Dk.Mwinyi, amefanya kampeni za kisayansi za kuwafuata wananchi katika makaazi yao na kusikiliza changamoto zinazowakabili ili akipata ridhaa za kuwa rais azitatue kwa haraka.
Aliwasihi wananchi kisiwani Pemba kuwachagua wagombea wote wa CCM, ambao ndio watakaotekeleza Ilani ya CCM ya mwaka 2020/2025.
Aliwasihi wananchi hao wasikubali kutumiwa na baadhi ya wanasiasa wanaowashawishi siku ya octoba 27,mwaka huu kwenda kupiga kura jambo ambalo sio sahihi badala yake wasiende kwani siku hiyo wanaopiga kura ni watu maalum ambao ni askari wa majeshi ya ulinzi na usalama, vikosi vya Idara maalum za SMZ na Watumishi wa Tume za Uchaguzi.
“Siku yenu ya kupiga kura ni octoba 28,mwaka huu nakuombeni mjitokeze kwa wingi kuwapigia kura nyingi wagombea wote wa CCM ili wawatumikie kwa uadilifu,,na sifa kubwa ya CCM ni kuahidi na ikatekeleza kwa wakati”,alisema Dk.Mabodi.
Nao wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi kwa nyakati tofauti waliwaomba wananchi ifikapo octoba 28,2020 wawachague kwa kuwapigia kura zili washinde na kuleta maendeleo.