***************************************
NJOMBE
Taasisi ya chakula na Lishe Tanzania TFNC Imebuni mchezo wa karata za mlo kamili ili kuhamasisha , kuboresha na kuwaongezea uelewa wa wananchi kuhusu mlo kamili na kukabiliana na tatizo la Utapiamlo ambalo linazitesa kaya nyingi chini hivi sasa.
Akizungumzia madhumuni ya kuanzisha mchezo huo afisa lishe mtafiti kutoka taasisi ya TFNC Elizabeth Lyimo katika maadhimisho ya wiki ya chakula duniani ambayo kitaifa yanafanyika mkoani Njombe amesema kwa kufanya hivyo kunawavutia wananchi kushiriki katika mchezo huo ambao unaenda sambamba na mafundisho ya lishe yanayotolewa na watalaamu wa afya na lishe.
Lyimo amesema katika karata kuna aina mbalimbali za vyakula hivyo endepa mshiriki anakuwa ameshinda anakabidhiwa zawadi ili kuhamasisha zaidi watu wengine kushiriki na kuzingatia lishe bora.
“Mtu yeyote anaweza kucheza mchezo wa karata za mlo kamili,wanaume wamekuwa wakishiriki kwa kiwango kidogo hivyo basi mchezo huu unaowalenga zaidi wanaume wa rika zote ili wapate uelewaa wa kupanga mlo iwe katika kununua vyakula au kuandaa mlo kwa ajili ya familia. “alisema Elizabeth.
Kuhusu Udumavu afisa mtafiti mwandamizi katika taasisi hiyo Maria Ngilisho amesema watu wengi wanapenda kupima uzito wakiamini kuwa uzito mkubwa ni kigezo cha kuwa na hali nzuri ya lishe jambo ambalo sio sahihi na kudai kwamba mtu anaezingatia makundi yote ya chakula katika mlo wake ndiyo anakuwa na afya bora bila kujali uzito na kimo.
Aidha Ngilisho amesema mtu anapopanga mlo ili uwe mlo kamili, ni lazima atumie angalau chakula kimoja kutoka kwenye kila kundi la chakula kati ya makundi matano ili aweze kujiweka vema katika suala la kuwa na lishe bora.
“Watu wengi wanapenda kupima uzito, uzito pekee sio kigezo cha kutosheleza kuashiria na hali nzuri ya lishe. Ili kupata hali halisi ya lishe ya mtu, tunatumia kipimo cha uwiano kati ya kimo/urefu na uzito ili kupata fahirisi (Body Mass Index – BMI)”alisema Ngilisho.
Katika hatua nyingine mteknolojia mwandamizi wa maabara kutoka taasisi ya chakula na lishe TFNC Juvenary Mushumbusi,amesema ili kunusuru afya za walaji taasisi ilianzisha Maabara mahususi kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa
maabara ili kuiwezesha Taasisi kutekeleza na kufanikisha majukumu yake.
Pia alisema”Maabara ya baiokemia (Biochemistry Laboratory)kazi kuu ya maabara hii ni kufanya uchunguzi wa sampuli zinazochukuliwa kutoka kwenye mwili wa binadamu ili kubaini viwango vya virutubishi au viashiria lishe mwilini (Nutritional Biomarkers) mwilini kwa mfano, vitamin, madini na elementi mbalimbali, mafuta na wingi wa damu”alisema.
“Maabara hii ina vitengo vitatu, ambayo ni mabara ya kemia ya chakula (Food Chemistry
Laboratory)kazi kuu ya maabara hii ni kufanya uchunguzi wa
sampuli za chakula ili kubaini uwepo na wingi wa viinilishe
kama vile, protini, wanga, mafuta, vitamini, madini na phytochemicals. Pia kitengo hiki hufanya uchunguzi wa kubaini ubora na usalama wa chakula Kama vile uwepo na wingi wa sumukuvu, madini tembo, sumu kwenye mihogo (cyanide) na vikolezo (food additives)”alisema.
Hata hivyo aliongeza kuwa maabara ya maikrobiolojia (Microbiology Laboratory)
kazi kubwa ya maabara hiyo ni kufanya vipimo maalumu vya kilishe kama vile folate na amino asidi kwa kutumia mbinu za maikrobiolojia.