Mgeni rasmi siku ya nne ya maonesho ya Siku ya Chakula Duniani Kitaifa Njombe na Mkuu wa Wilaya ya Wanging’ombe Lauteri Kanoni (kushoto) akipata maelezo ya namna bidhaa za kilimo zinavyozalishwa na kiwanda kidogo cha chuo cha Mafunzo ya Kilimo (MATI) Ilonga. Kulia ni Mkufunzi Kilimo Mariam Malianda na katikati ni Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Mafunzo Wizara ya Kilimo Dkt.Mashaka Mdangi.
Kaimu Mkurugenzi Idara ya Usalama wa Chakula Wizara ya Kilimo Dkt.Honest Kessy ( mwenye miwani) akiongea na Meneja Ubora wa kiwanda cha Maji Kitulo Bw. Njoroge leo wakati kamati ya uratibu maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani ilipotembelea kiwanda hicho kilichopo Njombe.
Sehemu ya wajumbe wa kamati ya uratibu wa maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani wakiwa kwenye kiwanda cha Maziwa Njombe kujifunza namna kinavyozalisha bidhaa za maziwa. Kiwanda hicho kimefanikiwa kurejesha uzalishaji wake baada ya kupata mkopo toka Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) kikiwa na uwezo wa kusindika lita 6000 za maziwa kwa siku.
Mkuu wa Wilaya ya Wanging’ombe na Mgeni rasmi siku ya nne ya maonesho ya Siku ya Chakula Duniani Mhe.Lauteri Kanoni (kushoto) akisaini kitabu cha wageni wakati alipotembelea banda la Kitengo cha Mazingira Wizara ya Kilimo kinachotoa elimu kuhusu mabadiliko ya tabia nchi. Kulia ni Afisa Kilimo Mwandamizi Evelny Kagoma.
************************************
Vyuo vya mafunzo ya kilimo nchini (MATIs) vimetakiwa kubuni mbinu mbadala ya kufundisha kwa vitendo wanafunzi kuchakata bidhaa za kilimo na mifugo ili kuongeza thamani ya mazao ya wakulima na wafugaji watakapohitimu.
Wito huo umetolewa leo (13.10.2020) na Mkuu wa Wilaya ya Wanging’ombe Lauteri Kanoni wakati alipotembelea banda la Idara ya Mafunzo ,Ugani na Utafiti la Wizara ya Kilimo ikiwa ni siku ya nne ya maonesho ya Siku ya Chakula Duniani yanayofanyika mkoani Njombe.
Mkuu huyo wa wilaya alisema hayo baada ya kuona bidhaa za kilimo ikiwemo mchele, mafuta ya alizeti, unga wa lishe na bidhaa zitokanazo na nyuki zilizozalishwa na wanafunzi wa vyuo vya mafunzo ya kilimo (MATI) Ilonga cha Morogoro na Mubondo cha Kigoma.
“Nimefurahi kuona jinsi wanafunzi hawa wa vyuo vya kilimo walivyoweza kuzalisha bidhaa zilizoongezwa thamani kwa kutumia mashine ndogo ikiwa ni sehemu ya mafunzo yao vyuoni hali inayokuza stadi za kujitegemea kiuchumi na kuongeza uhakika wa masoko” alisema Kanoni.
Kanoni alitoa wito kwa Wizara ya Kilimo kuhakikisha inaviwezesha vyuo vya kilimo nchini kuanzisha viwanda vidogo vidogo vitakavyotumika kama madarasa ya wanafunzi kujifunza uzalishaji bidhaa zilizoongezwa thamani na kuwa na uhakika wa masoko na bei nzuri hali itakayochangia kukuza ajira vijijini na mijini.
Akizungumza kwenye tukio hilo Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Mafunzo, Utafiti na Ugani Dkt. Mashaka Mdangi alisema vyuo vyote vya mafunzo ya kilimo vya umma 14 vimeelekezwa kubuni miradi ya kujiongezea kipato ikiwemo viwanda vidogo vidogo ndio maana wameleta bidhaa za chakula kwenye maonesho.
Dkt. Mdangi alisema serikali itaendelea kubuni mitaala mahsusi ya mafunzo ya kilimo ili wanafunzi wawe na stadi nyingi ikiwemo uzalishaji wa bora wa mazao ya kilimo, uchakataji wake na uhifadhi bora ili kuongeza wigo wa uhakika wa kipato na kuepuka kuuza mazao ghafi.
“Tupo hapa Njombe kutoa elimu ya namna vyuo vya mafunzo ya kilimo (MATI) vinavyofundisha elimu ya kujitegemea na kuongeza thamani ya mazao ya kilimo na kuhamasisha wananchi na wanafunzi kujiunga na vyuo vyetu vya MATI mwaka huu 2020 “alisema Dkt. Mdangi.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Wilaya ya Wanging’ombe alitembelea banda la mradi wa kudhibiti sumukuvu (TANIPAC) na kupatiwa elimu ya udhibiti wa sumukuvu kwenye mazao hususani mahindi na karanga.
Akitoa elimu Mratibu wa kudhibiti sumukuvu Zanzibar aliyepo Njombe kushiriki maonesho Mwanaidi Ali Khatib alisema wanatoa elimu kusaidia wakulima kuepuka kuchafua mazao yao na fangasi wa kuvu wakati wa kuvuna shambani, kusafirisha kwenye magari na wakati wa kuhifadhi ghalani hususan nafaka.
Mwanaidi aliongeza kusema mradi wa kudhibiti sumukuvu unatekelezwa Tanzania Bara na Zanzibar kwa lengo la kuhakikisha wananchi wafahamu namna ya kuepuka sumukuvu inayopelekea matatizo ikiwemo magonjwa ya ini, udumavu na kuharibu soko la mazao ya mahindi yanapogundulika kuwa na sumukuvu.
“Tunaelimisha watengenezaji wa vyakula kwa kutumia mashine pia wakulima jinsi ya kuhifadhi nafaka kwenye maghala lengo chakula kisichafuliwe na fangasi wanaosababisha kuvu ndio lengo la mradi wa TANIPAC” alisisitiza Mwanaidi.
Aidha, akiwa viwanjani hapo Mkuu huyo wa wilaya Lauteri Kanoni alitembelea pia banda la Bodi ya Sukari na kufahamishwa kuwa nchi bado haijajitosheleza na uzalishaji wa sukari hali inayopelekea uagizaji toka nje licha ya uwepo fursa nzuri ya kilimo cha miwa.
Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Udhibiti Bodi ya Sukari Bahati Hakimu alieleza kuwa mahitaji ya sukari nchini kwa mwaka ni tani 470,000 wakati uzalishaji wa ndani ni tani 350,000 hali inayopelekea kuwepo upungufu mara kwa mara.
“Ukiondoa soko la ndani tunazo fursa za uhakika za uzalishaji sukari kutokana na Tanzania kuwa na ardhi na mabonde yanayofaa kwa kilimo cha miwa, hivyo tupo hapa Njombe kuhamasisha wakulima na wawekezaji kutumia fursa ya kuanzisha mashamba ya miwa ” alisema Bahati Hakimu.
Wawakilishi wa wizara ,taasisi,wakala na wadau walipata fursa ya kufanya ziara ya mafunzo kwenye viwnda vya maji ya Kitulo na Kiwanda cha Maziwa vya Njombe kujionea namna wanavyozalisha bidhaa hizo muhimu katika kuhakiksha nchi inakuwa na chakula na lishe bora kwa ustawi wa afya za watu.
Maonesho ya Siku ya Chakula Duniani Kitaifa mkoani yameingia siku ya nne leo ambapo wadau toka wizara, taasisi, wakala na sekta binafsi wanashiriki kutoa elimu na teknolojia ya uzalishaji, uchakataji na uongezaji thamani mazao ya kilimo, mifugo na Uvuvi
Kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu inasema “ Kesho Njema Inajengwa na Lishe Bora Endelevu “ na yatafikia kilele chake tarehe 16 Octoba mwaka huu mkoani Njombe.