************************************
Na Mwandishi wetu, Manyara
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, imefanikiwa kuokoa shilingi milioni 9.8 za Halmashauri ya Wilaya hiyo zilizokuwa mikononi mwa wazabuni wasiotimiza wajibu wao.
Mkuu wa Takukuru Mkoani Manyara, Holle Joseph Makungu ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Babati.
Makungu amesema fedha hizo zimerejeshwa kutoka kwa wazabuni waliopewa fedha hizo kwa ajili ya vifaa vya ujenzi wa hospitali ya wilaya hiyo Ila hawakuwasilisha vifaa hivyo hadi hospitali hiyo ilipokamilika na kuanza kazi mwezi Mei 2020.
Amesema baada ya jitihada za Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri hiyo Yefred Myenzi kutaka kurejeshwa fedha hizo kutoka kwa wazabuni hao kukwama, aliiomba TAKUKURU iingilie kati ili fedha za umma zirejeshwe.
“Wazabuni waliohusika ni kampuni ya Shedehwa Enterprises and Logistics ya jijini Dar es salaam pamoja na kampuni ya Maura ya Mkoani Iringa,” amesema Makungu.
Amesema kufuatia uchunguzi huo, Octoba 12 mwaka huu TAKUKURU Mkoani Manyara na TAKUKURU Wilayani Simanjiro ilimshikilia kwa mahojiano Mkurugenzi wa Shedehwa na alikubali kulipa fedha hizo za halmashauri shilingi 7,064,000 kupitia akaunti ya TAKUKURU.
Anasema mzabuni Maura amesharudisha shilingi 2,736,000 TAKUKURU ambapo kwa pamoja zitarejeshwa kwa Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro.
“Hospitali ya Wilaya ya Simanjiro ni miongoni mwa hospitali mpya 67 zilizotengewa kiasi cha shilingi bilioni 1.5 kwa maelekezo ya Rais wa awamu ya tano mheshimiwa Dokta John Magufuli ” amesema Makungu.
Amesema Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro iliwapa zabuni wazabuni hao ambao hawakutekeleza wajibu wao kiasi kwamba Halmashauri hiyo ikatafuta fungu jingine ili kuziba pengo la fedha zilizolipwa kwa wazabuni ili mradi waweze kukamilisha ujenzi huo ndani ya muda uliokuwa umeelekezwa na Serikali.
“Ni rai kwa wazabuni wa ndani katika Mkoa wa Manyara kuhakikisha kuwa wanatimiza wajibu wao ili serikali iendelee kuwaamini na kuwapo kandarasi mbalimbali hali ambayo itasaidia kukuza mitaji yao,” amesema Makungu.