Wananchi wa Jimbo la Ilemela wametakiwa kumchagua kwa kura nyingi za NDIO mgombea ubunge kupitia chama cha mapinduzi katika jimbo hilo Ndugu Dkt Angeline Mabula kwa kuwa ndio mgombea pekee mwenye sifa za kuwatumikia, asiyebagua watu anaowaongoza, mwenye Ilani ya uchaguzi, anaejua changamoto za wananchi wake na mwenye uwezo wa kuzitatua.
Hayo yamebainishwa na Mjumbe wa halmashauri ya Chama Cha Mapinduzi Taifa (MNEC) Ndugu Richard Bundalla wakati akiwaombea kura wagombea wa chama chake kwa nafasi za Uraisi, Ubunge na Udiwani kwa wananchi wa kata ya Ibungilo katika viwanja vya soko la Kiloleli ambapo amewaomba wananchi hao kuhakikisha wanamchagua Rais Dkt John Magufuli kwa awamu nyengine, Mbunge awe Dkt Angeline Mabula na madiwani wote wa CCM kwa kuwa viongozi hao wametekeleza miradi mikubwa ya maendeleo yenye manufaa kwa jamii nzima
‘.. Nani kama Dkt Magufuli, Nani kama Dkt Angeline Mabula, Mama anaetuunganisha, Mama shupavu, Mama anaejua matatizo ya wazee, vijana, Mama anaetuunganisha jamii yote, Dkt Mabula ni kiongozi wa wote, Nawaomba tukamchague oktoba 28 ..’ Alisema
Kwa upande wake mgombea ubunge wa jimbo la Ilemela kwa tiketi ya CCM Dkt Angeline Mabula mbali na kuelezea miradi ya maendeleo iliyotekelezwa ndani ya jimbo hilo kama shule mpya za msingi, sekondari, ujenzi wa miundombinu ya barabara , ujenzi wa miradi ya maji ikiwemo tanki la Nyasaka, Kirumba na Nyamhongolo akawaomba kumuamini tena kwa kipindi cha miaka 5 ili akamalizie changamoto ndogo ndogo zilizobakia zinazowakabili wananchi hao ikiwemo kuongeza shule katika kata hiyo, kujenga zahanati, nakuongeza kuwa bilioni 10 imetengwa kushughulikia kero ya maji taka.
Kwa upande wake mwenyekiti wa CCM wilaya ya Ilemela Ndugu Nelson Mesha amewashukuru wananchi wa kata hiyo kwa kukiamini chama chake katika uchaguzi mkuu uliopita ambapo wagombea wote wa CCM walishinda katika uchaguzi huo hivyo kuwaomba kukiamini tena chama cha mapinduzi na kuwapigia kura wagombea wa nafasi za Uraisi, Ubunge na Udiwani ili wakamalizie shughuli za maendeleo walizozianza kuzitekeleza.
Mkutano huo wa kampeni ulihudhuriwa na wabunge watatu wateule kundi la wanawake kwa mkoa wa Mwanza akiwemo Ndugu Kabula ShitobelOo, Marry Masanja, Furaha Matondo, Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Mwanza Ndugu Hellen Bogohe, Mwenyekiti wa UVCCM mkoa wa Mwanza Ndugu Jonas Lufungulo aliyeambatana na kamati yake ya utekelezaji.