Katibu mkuu wizara ya maji Mhandisi Nadhifa Kemikimba kushoto akimtua mmoja wa wanawake ndoo ya maji kichwani mara baada ya kukagua mradi wa maji wa kitongoji cha Maizigela kijiji Kiteme kata Kasharunga wilaya Muleba okitoba 12, mwaka huu.
Wakazi wa kitongoji Maizigela wakifurahia huduma ya maji safi ambayo kwa miongo kadhaa wameikuwa wakiifata umbali mrefu na sasa imeweza kuwafikia karibu na maeneo yao wanayoishi.
Meneja wa wakala wa maji mjini na vijijini wilaya ya Muleba Mhandisi Jerome Patrick kulia akimtua ndoo ya maji mmoja wa wakina mama wa kitongoji Maizigela.
Wananchi wa kitongoji Mizigela kijiji Kiteme Kata Kasharunga wakimsikiliza Naibu katibu mkuu wa wizara ya Maji Mhandisi Nadhifa Kemikimba mwenye sketi nyeusi aliyefika kitongojini hapo kukagua mradi wa maji baada ya ukarabati kukamilika.
Muonekano wa kituo cha kuchotea maji DP katika kiongoji Maizigela baada ya kukarabatiwa na kuanza kutoa huduma ya maji kwa wananchi kwa masaa 24 kwasasa.
………………………………………………………………………………………
Na Allawi Kaboyo – Muleba.
Jamii ya kitongoji Maizigela Kijiji Kiteme kata Kasharunga Halmashauri ya wilaya Muleba Mkoani Kagera wameishukuru na kuipongeza serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Magufuli kwa kazi kubwa ambayo imekuwa ikifanyika hasa katika miradi ya maji.
Wananchi hao wametoa shukrani hizo mbele ya naibu katibu mkuu wa wizaya ya MajiMhandisi Nadhifa Kemikimba aliyefika kitongojini hapo kwa lengo la kukagua upatikanaji wa huduma ya maji pamoja na kukagua miradi mbalimbali ya maji oktoba 12, mwaka huu.
Paskazia Frolian ni mkazi wa kitongoji hicho ambaye ameishukuru serikali kwa kuweza kuwaboreshea mradi wa maji abao ulikuwa umekufa kwa miaka mingi na kuwapelekea kutembea umbali mrefu kwenda kufata maji huku wakipanda milima na kushuka huku wakishindwa kufanya baadhi ya kazi nyingine kutokana na uchovu.
“Kwanza niseme tu ukweli tunamshukuru Rais Magufuli kwa kutuangalia na sisi wananchi wa vijijini, sisi wakina mama tulikuwa tukiteseka kufata maji mbali mtu unabeba dumu moja umechoka na huwezi kufanya kazi nyingine hata kuwahudumia waume zetu tulikuwa tukishindwa na wengine kutishiwa kuachwa, lakini kwasasa maisha ni safi maji tunachota muda wowote.” Ameeleza Bi. Paskazia.
Kwaupande wake mmoja wa mabalozi wa kitongoji hicho Vedasto Tindibaiyukao Tofiri amesema mradi huo umekuwa msaada mkubwa kwa wananchi wa kitongoji hicho pamoja na wananchi wa vitongoji jirani kutokana na utoaji wa maji kwa kipindi kirefu na kwa uhakika.
Amesema kuwa tangu anakuwa mradi huo aliukuta lakini kipindi hicho maji yalikuwa hayatoki kwa uhakika hali iliyokuwa ikiwapelekea wanawake wa kijiji na kitongoji hicho kuhangaika kutwa nzima wakitafuta maji na wengine kutumia gharama nyingi kununua maji kwa gharama ya kuanzia shilingi mia 300 hadi shilingi mia tano 500 kwa dumu la lita 20 ambapo kwa sasa wananchota maji hayo kwa shilingi 50 kwa ndoo ya lita 20.
Hata hivyo mwenyekiti wa jumuiya ya watumiaji maji Shaaban Juma ameeleza kuwa mradi huo umekuwa msaada mkubwa kwa wananchi wa kitongoji kizima ambapo amesema kuwa kwa kipindi cha miezi miwili tangu mradi huo uanze kutoa maji, jamii tayari imechangia kiasi cha zaidi ya shilingi laki tatu kutokana na kununua maji.
Ameongeza kuwa awali ulipotambuishwa mradi huo alipata changamoto kubwa ya jamii kukataa kununua maji na kuendelea kuchota maji katika mito waliyoizoea na kuongeza kuwa baada ya kuwapatia elimu ya kutosha kwa kufanya mikutano mbalimbali sasa jamii imekuwa na muamko wa kuyatumia maji hayo ambayo amesema kuwa ni maji safi na salama.
Awali akisoma taarifa ya utekelezaji wa mradi huo kwa naibu katibu mkuu, Jerome Patrick amesema kuwa kuwa mradi huo umegharimu kiasi cha shiingi milioni 48 katika ukarabati wake ambapo ulianza kutoa maji tangu tarehe 15, mei mwaka huu ambapo hadi sasa unaendelea huku vikiwa vimejengwa vituo vya kuchotea maji 10.
Jerome amesema kuwa mradihuo chanzo chake ni chemichemi ambapo kwasasa kinahudumia zaidi ya watu 3500, ambapo amebainisha kuwa moja ya changamoto iliyokuwa ikisumbua ni uwepo wa vyanzo vya asili ambavyo wananchi walikuwa wakivitumia na kukataa kulipia maji.
Kwaupande wake naibu katibu mkuu wizara ya Maji ameupongeza uongozi wa RUWASA Mkoa wa Kagera pamoja na wilaya Muleba kwa kusimamia vyema miradi ya maji ambayo sasa imeanza kutoa matunda kwa wananchi walengwa.
Aidaha ameitaka jamii kuwa walinzi wa miradi hiyo kwa kuhakikisha inakuwa salama wakati wote ili iendelee kuwahudumia kwa kuhakikisha miundombinu yake haihujumiwi na kuharibiwa na watu ambao sio wazalendo na wenye nia hovu.
“Niwapongeze kwa kupata maji, ila niseme tu mradi huu sio wa serikali mradi huu ni wa kwenu hivyo kila mmoja wenu anawajibika kuwa mlizi hapa, tunataka na watoto hawa wakikuwa waukute mradi huu ukifanya kazi .” Amesisitiza Naibu katibu mkuu.
Hata hivyo meneja wa wakla wa maji mjini na vijijini RUWASA Mkoa wa Kagera Mhandisi Walioba Sanya amewaeleza wananchi hao kuwa waendelee kutumia maji hayo kwa kuchangia kwa kuwa fedha hiyo ya maji inabaki kwenye miliki yao ambayo wataweza kuitumia hata kufanyia marekebisho ya miundombinu pale itakapoonekeana kuharibika.