Na John Walter-Babati
Mbunge mteule wa Jimbo la Babati Vijijini katika mkoa wa Manyara Daniel Baran Sillo amesema katika miaka mitano watahakikisha vijiji ambavyo havina huduma ya nishati ya Umeme vinapata huduma hiyo.
Mheshimiwa Sillo akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Endamaghay kata ya Gidas katika mkutano wa Kampeni za Chama cha Mapinduzi, amesema katika Jimbo hilo lenye vijiji vipatavyo 102, vijiji 84 tayari vina umeme huku 18 vikiwa katika mpango wa kufikiwa na huduma hiyo.
Aidha Mbunge huyo amesema serikali ya Chama cha Mapinduzi (CCM) inayoongozwa na Rais John Pombe Magufuli katika kuhakikisha nchi inakuwa na uchumi imara imesambaza Umeme kwenye vijiji zaidi ya 9000 Tanzania bara ili kuwawezesha wananchi kuwa na Viwanda vya kutosha ambavyo vitazalisha ajira.
Sillo amewaombea kura Wagombea udiwani katika jimbo hilo kupitia Ccm na Rais John Magufuli katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28,2020.