Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji wa Tanzania-TIC, Dkt. Maduhu Kazi (wa tatu kulia) akikata utepe kufungua chuo cha ufundi Kasoli iliyojengwa kwa msaada na Mwekezaji wa Kampuni ya Alliance Ginnery na baadaye kukabidhiwa kwa Serikali jana katika Kijiji cha Kasoli wilayani Bariadi mkoani Simiyu.
Sehemu ya majengo ya chuo cha ufundi Kasoli iliyojengwa kwa msaada na Mwekezaji wa Kampuni ya Alliance Ginnery na baadaye kukabidhiwa kwa Serikali iliyopo katika Kijiji cha Kasoli wilayani Bariadi mkoani Simiyu.
Meneja Mkuu wa Alliance Ginnery Limited, Bw. Boaz Ogola akitoa maelezo kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji wa Tanzania-TIC, Dkt. Maduhu Kazi (mwenye skafu) juu ya shule ya ufundi Kasoli iliyojengwa na kampuni hiyo kwa msaada na kuikabidhi kwa serikali, baada ya kukifungua chuo hicho jana katika Kijiji cha Kasoli wilayani Bariadi mkoani Simiyu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji wa Tanzania-TIC, Dkt. Maduhu Kazi akiyaangalia maji yanayotoka katika kisima kilichochimbwa kwenye shule ya ufundi ya Kasoli iliyojengwa kwa msaada na kampuni Alliance Ginnery na kuikabidhi kwa serikali, baada ya kuifungua chuo hicho jana katika Kijiji cha Kasoli wilayani Bariadi mkoani Simiyu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji wa Tanzania-TIC, Dkt. Maduhu Kazi, Meneja Mkuu wa Alliance Ginnery Limited, Bw. Boaz Ogola, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka wakifurahia na wananchi katika kijiji cha Kasoli baada ya ufunguzi wa chuo cha ufundi Kasoli iliyojengwa kwa msaada na kampuni Alliance Ginnery na kuikabidhi kwa serikali jana kijijini hapo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji wa Tanzania-TIC, Dkt. Maduhu Kazi, Meneja Mkuu wa Alliance Ginnery Limited, Bw. Boaz Ogola, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka wakifurahia na wananchi katika kijiji cha Kasoli baada ya ufunguzi wa chuo cha ufundi Kasoli iliyojengwa kwa msaada na kampuni Alliance Ginnery na kuikabidhi kwa serikali jana kijijini hapo.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka(kushoto ) akiteta jambo na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji wa Tanzania-TIC, Dkt. Maduhu Kazi mara baada ya makabidhiano ya chuo cha ufundi Kasoli iliyojengwa kwa msaada na kampuni ya Alliance Ginnery na kuikabidhi kwa serikali, katika Kijiji cha Kasoli wilayani Bariadi mkoani Simiyu.
Meneja Mkuu wa Alliance Ginnery Limited, Bw. Boaz Ogola akiwaongoza Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji wa Tanzania-TIC, Dkt. Maduhu Kazi (mwenye skafu) na viongozi wengine kukagua chuo cha ufundi ya Kasoli iliyojengwa kwa msaada na kampuni Alliance Ginnery na kuikabidhi kwa serikali, baada ya kuifungua shule hiyo jana katika Kijiji cha Kasoli wilayani Bariadi mkoani Simiyu.
…………………………………………………………………………………………
Na Stella Kalinga, Simiyu RS
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka ametoa wito kwa wazazi na walezi kuwapunguzia kazi wanafunzi walio katika madarasa ya mitihani ya Taifa (darasa la nne, kidato cha pili na kidato cha nne) ambayo inatarajiwa kufanyika hivi karibuni ili waweze kujipatia muda mwingi wa kujisomea kujiandaa na mitihani hiyo.
Mtaka ameyasema hayo jana wakati makabidhiano ya Chuo cha Ufundi Kasoli katika Kijiji cha Kasoli wilayani Bariadi kilichojengwa na mwekezaji Alliance Ginnery Limited na kukabidhiwa kwa Serikali na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Dkt. Maduhu Kazi kwa niaba ya kampuni hiyo na kupokelewa na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka kwa niaba ya wananchi.
“Darasa la saba wameshafanya mtihani wao, watoto wa darasa la nne, kidato cha pili na kidato cha nne waendelee kufanya maandalizi, wazazi na walezi wapunguzieni kazi watoto wote walio kwenye madarasa haya na wakiwa nyumbani wafanye majadiliano ya pamoja,” alisema Mtaka.
Aidha, Mtaka amewaonya wazazi na walezi wenye nia ya kuwaozesha wanafunzi wa kike waliohitimu elimu ya msingi kuwa watakaofanya hivyo watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria, huku akitoa wito kwa jamii yote kuwa walinzi wa watoto wa kike ili waweze kutimiza ndoto zao.
Mtaka ameishukuru Kampuni ya Allience Ginnery kujenga chuo cha ufundi Kasoli na kutoa wito kwa wasichana na wanawake kijiji cha Kasoli kujitokeza kupata mafunzo ya ushonaji bila malipo katika chuo hicho katika kipindi cha mwezi Oktoba hadi Desemba, kabla ya kuanza kwa mafunzo yatakayoanza mwakani kwa mtaala wa Serikali na kuahidi kutoa vyerehani 25.
Meneja Mkuu wa Alliance Ginnery Limited, Bw. Boaz Ogola amesema Kampuni hiyo imekuwa inajihusisha sana na maendeleo ya jamii katika sekta ya elimu, afya na maji kwa kuwa wao ni sehemu ya jamii, ni wajibu wao kufanya hivyo na ni sehemu ya maelekezo ya TIC wanayopewa wawekezaji wote.
“Tunashiriki kwenye masuala ya jamii kwa sababu sisi ni sehemu ya jamii, sisi tunashughulika na wakulima na wanaotulimia pamba na kutuuzia kutuwezesha kuendesha kiwanda chetu, siku za nyuma tulijikita kwenye afya, maji na elimu ya msingi na sekondari; tumeona haja ya kujenga chuo cha ufundi ili wanafunzi watakaoshindwa kuendelea na masomo, wapate mafunzo ya ufundi ili waweze kujitegemea,” alisema Ogola.
Aidha, Ogola amesema pamoja na mafunzo ya ufundi mipango ya baadaye ya kampuni ya Alliance Ginnery kuongeza darasa moja la wakulima kwa lengo la kutoa warsha na mafunzo kwa wakulima ili waweze kulima kilimo chenye tija ili kampuni hiyo iweze kupata malighafi bora kwa ajili ya kiwanda chake cha kuchambua pamba..
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Dkt. Maduhu Kazi ameipongeza na kuishukuru Kampuni ya Alliance Ginnery kujenga chuo cha Ufundi na kutoa wito kwa wawekezaji wengine kuona umuhimu wa kuwafikia wananchi walio katika maeneo yao huku akiahidi kuwa TIC itahakikisha kinakuwa mstari wa mbele kutatua changamoto zinazowakabili wawekezaji.
“TIC inashirikiana na Serikali hata ngazi ya mikoa na tumejielekeza zaidi kuongeza ufanisi katika shughuli zetu za kuwasaidia wawekezaji masuala ya vibali kwa kushirikiana na Taasisi zinazohusika; pia tumejipanga hata kuwafikia wawekezaji wadogo Watanzania maana baada ya tathmini tumeona eneo hilo kuna mapungufu maana wengi wanadhani sisi tunahusika na wawekezaji wa kigeni tu,” alisema Dkt. Kazi.
Naye Mkazi wa Kijiji cha Kasoli Shamsa Abdallah amesema anaishukuru Kampuni ya Alliance Ginnery kwa kuwajengea chuo cha ufundi na anaamini kuwa kitawasadia kwenye mafunzo ya ushonaji na mafunzo yanayohusiana na kilimo yatakayowasaidia kujikwamua kiuchumi.
Kampuni ya Alliance Ginnery Limited imejenga majengo ya chuo cha ufundi Kasoli kwa gharama ya zaidi ya shilingi milioni 180, kuchimba kisima cha maji chenye uwezo wa kutoa lita 5000 kwa saa pamoja na kuweka vifaa kama vyerehani, majiko ya gesi na vifaa mbalimbali vya kujifunzia upishi,vifaa vya kujifunzia uashi na useremala meza na viti vya ofisi.