Katika kuadhimisha wiki ya Huduma kwa Wateja, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kupitia watoa huduma wake toka maeneo mbalimbali wamewafikia Wateja mitaani na kutoa elimu na huduma mbalimbali zihusuzo huduma na bidhaa za TANESCO.
Hayo yamesemwa na Meneja Uhusiano TANESCO, Bi. Johari Kachwamba wakati wa kilele cha maadhimisho ya wiki ya Huduma kwa Wateja leo Ijumaa Oktoba 09, 2020 kwenye viwanja vya Biafra Kionondoni jijini Dar es Salaam.
”Tangu Oktoba 5, tumekuwa tukitoa huduma mbalimbali kwa wateja wetu kote nchini, tumetoka ofisini na kuwafuata wateja mitaani waliko na hadi leo hii tunaadhimisha wiki ya Huduma kwa wateja katika Mkoa wetu wa Kinondoni Kaskazini ambapo pekee tumewahudumia wateja wengi waliotutembelea katika viwanja vya Biafra Jijini Dar es Salaama” alisema Bi. Kachwamba.
Aliongeza kuwa, Wiki ya huduma kwa wateja imekuwa ni fursa nzuri na adhimu kwa TANESCO na wateja wa Shirika kukutana.
Alisema, miongoni mwa huduma zilizotolewa na wafanyakazi wa TANESCO kwa wateja ni pamoja na elimu ya matumizi bora na salama ya umeme, kuwasikiliza wateja, wateja wameweza kujaza fomu za maombi mapya ya kuunganishiwa umeme, na pia wameelimishwa kuhusu aina mbalimbali za mita za umeme.
Akimuwakilisha Meneja wa Kinondoni Kaskazini, Mhandisi Godlove Mathayo, wateja wengi wamekuwa wakifanya wayaring kwenye nyumba zao bila kutumia Wakandarasi waliosajiliwa hivyo
wateja wameelimishwa kutambua na kutumia Wakandarasi waliosajiliwa kwa usalama wao na mali zao kuepusha hitilafu za umeme za mara kwa mara.
“Niwashauri wateja wetu wanapotaka kufanya wayaring wawatumie mafundi walioidhinishwa na EWURA kwani hao wana ujuzi wa kutosha wa kufanya kazi hiyo” alisema Mhandisi Mathayo.
Mhandisi Mathayo alifafanua kuwa, mteja anapotaka kufikishiwa umeme halazimiki kulipa gharama yoyote ya ukaguzi wa eneo (survey) kwani huduma hiyo inatolewa bure na TANESCO.