Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Kassim Majaliwa akihutubia mkutano wa kampeni kwenye viwanja vya Kituo cha Mabasi cha Songe wilayani Kilindi, Mkoa wa Tanga Oktoba 8, 2020.
***********************************
MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa amesema Serikali imepanga kujenga hospitali za halmashauri 98 ikiwemo na ya halmashauri ya wilaya ya Kilindi katika awamu ya pili ya ujenzi wa hospitali hizo ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya CCM ya 2020-2025.
Ameyasema hayo leo (Alhamisi, Oktoba 8, 2020) wakati alipozungumza na wananchi kwa nyakati tofauti katika kata za Songe na Kwediboma wilayani Kilindi, Tanga katika mikutano ya kumuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM Rais Dkt Magufuli pamoja na mgombea ubunge wa jimbo la Kilindi Omari Kigua na wagombea wa udiwani wa CCM.
“Serikali inaendelea kutoa huduma za tiba kwa ngazi ya Wilaya kupitia Hospitali teule ya KKKT (DDH) ambapo asilimia 90 ya watoa huduma ni wa Serikali. Wilaya imetenga eneo la ekari 100 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ambapo Serikali imetoa sh. bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali hiyo.”
Mheshimiwa Majaliwa amesema mbali na ujenzi wa hospitali hiyo, pia Serikali imetoa shilingi milioni 800 kwa ajili ya ujenzi wa vituo viwili vya afya vya Songe na Kwediboma ambavyo vyote vimekamilika na wananchi wanapata huduma zikiwemo na za upasuaji wa mama na mtoto.
Amesema pia Serikali imetoa sh. milioni 454.2 za ujenzi wa zahanati mbili za Msente na Msagalu pamoja na ukarabati wa Kwekivu na sh. bilioni 1.97 kwa ajili ya ununuzi wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi katika kipindi cha miaka mitano ambapo wastani wa kila mwezi ni sh. milioni 33.
Akizungumzia kuhusu miradi mikubwa ya maji inayotekelezwa katika wilaya hiyo, Mheshimiwa Majaliwa amesema jumla ya fedha shilingi bilioni 7.421 zimetolewa kwa ajili ya ujenzi wa bwawa la maji Kwamaligwa, ujenzi wa mradi wa maji Kwinji /Muungano, ujenzi wa mradi wa maji Mafuleta;, mradi wa maji Bokwa, mradi wa maji wa Jungu/Balang’a, mradi wa maji Saunyi na mradi wa maji Songe/Vilindwa.
Pia, Mheshimiwa Majaliwa amesema miradi mingine ya maji ya jumla ya shilingi milioni 812 imetekelezwa katika wilaya hiyo ambayo ni mradi wa maji Saunyi, ujenzi wa mradi wa maji Gitu, mradi wa maji Kwadudu, mradi wa maji Kilindi, mradi wa maji Kimbe na mradi wa Maji Mabalanga.
Amesema Serikali imeanza ujenzi mpya barabara zenye urefu wa kilomita 6,006.04 na ukarabati wa barabara kwa kiwango cha lami ikiwemo ya Handeni – Kiberashi – Kondoa – Singida na sehemu ya Handeni – Kiberashi (km 50) na kwamba barabara hizo zitanufaisha maeneo ya Kilindi kwa kiasi kikubwa.
Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa amesema shilingi bilioni 4.638 zimetolewa kupitia TARURA kwa matengenezo ya kawaida, matengenezo ya sehemu korofi, hizo zimetumika kwa muda maalum na madaraja kwa barabara za Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi ikiwemo ujenzi wa barabara ya Muungano-Kilindi-Kimbe,
Amesema miradi mingine ni pamoja na ujenzi wa barabara ya Muungano-Kimembe-Tamota-Vyadigwa, ujenzi Barabara ya Negero-Lukole-Vunila, ujenzi wa Barabara Songe-KKKT-Mvungwe, ujenzi wa Barabara ya Kwediswati-Saunyi na ujenzi wa Barabara ya Kibirashi-Gitu-Komuhingo.
Pia, Mheshimiwa Majaliwa amesema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita (2015 – 2020) Serikali imefanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa kilomita 5,974.2 za barabara ikiwemo barabara ya Handeni – Kiberashi – Kondoa – Singida (km 460), Mziha – Handeni (km 68), Magole – Turiani – Handeni na sehemu ya Turiani – Mziha – Handeni (km 128) ikiwa ni utekelezaji wa ilani ya CCM.