Mnamo tarehe 9 Septemba 2020, Benki Kuu ya Tanzania ilitoa waraka kwa benki na taasisi za fedha kuzitaarifu kuhusu utafiti kuhusu maendeleo ya matumizi ya njia mbadala za malipo katika uchumi badala ya pesa taslimu. Waraka huo uliziagiza benki na taasisi za fedha kuwasilisha taarifa kuhusu miamala ya fedha taslimu zinazotolewa na wateja kuanzia tarehe 7 Septemba 2020.
Benki Kuu inapenda kutoa ufafanuzi wa ziada kuhusu waraka tajwa kama ifuatavyo:
- Kama sehemu ya maendeleo ya sekta ya fedha, hatua mbalimbali zimechukuliwa kupunguza matumizi ya pesa taslimu katika kufanya miamala. Hatua hizi zinakwenda sambamba na maendeleo katika masoko ya fedha duniani, kwa kuzingatia faida zinazoambatana na matumizi madogo ya pesa taslimu katika uchumi.
- Pamoja na kukuza huduma jumuishi za kifedha, malipo ya kidigitali yanapunguza gharama za utoaji wa huduma za kifedha kwa watu wa kipato cha chini, yanaongeza usalama, kurahisisha upatikanaji wa huduma na kupunguza gharama za kuchapisha, kutengeneza na kusambaza noti na sarafu.
- Hatua ambazo zimechukuliwa kupunguza matumizi ya pesa taslimu ni pamoja na kutengeneza mifumo ya malipo ya kidigitali ikiwemo, Mfumo wa Malipo baina ya Benki (Tanzania Interbank Settlement System), Mfumo wa Malipo wa Afrika Mashariki (East African Payment System); Mfumo wa Malipo kwa Jumuiya ya SADC (SADC Integrated Regional Electronic Settlement System); Mfumo wa Kidigitali wa Malipo ya Hundi (Tanzania Automated Clearing House); Mfumo wa Kielektroniki wa kutuma Fedha (Electronic Fund Transfer) na matumizi ya kadi za malipo. Hatua nyingine ni pamoja na kutoa leseni kwa Kampuni za Simu ziweze kutoa huduma za kifedha kupitia simu za mkononi.
- Hivyo, lengo la waraka kwa benki na taasisi za fedha ni kuiwezesha Benki Kuu kukusanya taarifa zitakazowezesha kufanya tathmini ya matokeo ya hatua zilizochukuliwa na kuamua hatua zaidi za kuchukua kisera, kisheria na kiteknolojia ili kuendelea kupunguza matumizi ya pesa taslimu katika kufanya miamala.
Benki Kuu inawahakikishia wananchi kwamba taarifa zinazokusanywa kuhusu matumizi ya njia mbadala za malipo badala ya pesa taslimu zitatumika kwa malengo yaliyoanishwa katika ufafanuzi huu na si vinginevyo.