Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Nadhifa Kemikimba akizungumza na washiriki wa mafunzo ya Bodi za Wakurugenzi na Menejimenti za Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira Kanda ya Ziwa (hawapo pichani). Washiriki wa mafunzo ya Bodi za Wakurugenzi na Menejimenti za Mamlaka 14 za Majisafi na Usafi wa Mazingira kutoka Kanda ya Ziwa wakifuatilia mafunzo.Mkurugenzi Msaidizi Utoaji wa Huduma ya Maji Wizara ya Maji, Mhandisi Lydia Joseph akizungumza wakati wa mafunzo. Kulia ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Nadhifa KemikimbaWashiriki wa mafunzo ya Bodi za Wakurugenzi na Menejimenti za Mamlaka 14 za Majisafi na Usafi wa Mazingira kutoka Kanda ya Ziwa wakifuatilia mafunzo.
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Mugango-Kyabakari, Mhandisi Cosmas Sanda akizungumza kwa niaba ya Wakurugenzi wa Mamlaka za Maji Kanda ya Ziwa wakati wa mafunzo.
Muwezeshaji wa mafunzo Mhadhiri kutoka Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Dkt. Abdulrahman Nkoba akizungumzia umuhimu wa elimu ya masuala ya fedha kwa washiriki wa mafunzo.
************************************
Na Mohamed Saif- Mwanza
Serikali imeweka mpango wa kuhakikisha huduma ya uondoshaji wa majitaka kwenye makazi katika Miji na Makao Makuu ya Mikoa inafikia asilimia 30 ifikapo Mwaka 2025.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Nadhifa Kemikimba amebainisha hayo Oktoba 7, 2020 Jijini Mwanza wakati akifunga Mafunzo ya Bodi za Wakurugenzi na Menejimenti za Mamlaka 14 za Majisafi na Usafi wa Mazingira kutoka Kanda ya Ziwa.
Mhandisi Kemikimba alisema Serikali inaendelea kufanya usanifu na kutekeleza miradi mbalimbali ya majitaka ili kuhakikisha inakwenda sambamba na ujenzi wa miradi ya majisafi kote nchini.
“Kwa sasa lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa miradi yote mikubwa ya usambazaji majisafi katika miji inakwenda sambamba na uwekaji wa mifumo imara ya uondoshaji wa majitaka,” Mhandisi Kemikimba alisisitiza.
Ili kuhakikisha lengo hilo linatimia, Mhandisi Kemikimba alizielekeza Mamlaka za Maji kuhakikisha zinakuwa na mikakati ya kutenga maeneo kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya majitaka pamoja na kuandaa maandiko kwa ajili ya kutafuta fedha za kuendeleza maeneo hayo.
Aidha, alizitaka Bodi za Mamlaka za Maji kote nchini kujenga utamaduni wa kutembelea na kukagua miradi inayotekelezwa kwenye maeneo yao kwa lengo la kupata thamani halisi ya fedha zilizowekwa katika ujenzi.
Mhandisi Kemikimba alisisitiza umuhimu wa Bodi kufanya ziara za kushtukiza kwenye miundombinu ya maji, mitambo ya kusukuma maji pamoja na kufanya mahojiano na wananchi kwenye maeneo yao ili kupata uelewa wa hali halisi ya upatikanaji wa huduma kwa lengo la kuboresha zaidi.
Alisema Serikali kupitia Wizara ya Maji jukumu lake ni kuhakikisha kila Mtanzania anafikiwa na huduma ya majisafi na salama kwani ni haki yake ya msingi na hivyo ni vyema mamlaka za maji zikatambua hilo na zikajikita katika kuhakikisha maji safi na salama yanamfikia kila mwananchi.
“Bodi muende mbele zaidi katika kuboresha huduma, maji ni uhai, maji hayana mbadala unapokabidhiwa jukumu la kufanya kazi kwenye Sekta ya Maji utambue unatekeleza ibada ya kumkomboa mwananadamu,” Mhandisi Kemikimba alisema.
Mhandisi Kemikimba vilevile alizitaka Bodi kuzielekeza Menejimenti zao kuhakikisha zinakuwa na mipango ya kuvipatia maji viwanda sambamba na kuandaa mikakati thabiti ya kushirikisha sekta binafsi kwa lengo la kuboresha hali ya huduma kwenye maeneo yao.
“Mnapaswa kuorodhesha viwanda vilivyopo kwenye maeneo yenu na muwe na mipango madhubuti ya kuhakikisha mnawafikishia huduma bila kujali ni kiwanda cha kitu gani,” alielekeza Mhandisi Kemikimba.
Aliwakumbusha washiriki wa mafunzo kuhakikisha wanazingatia maelekezo yaliyotolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga wakati wa ufunguzi ambayo ni kutozoea matatizo ya wateja na badala yake kuyafanyia kazi kwa wakati, kupunguza upotevu wa maji kwa kuhakikisha kila mteja ana dira na kuajiri watumishi wenye sifa.
Akizungumzia mafunzo, Mhandisi Kemikimba alisema Wizara ina matumaini kwamba washiriki wameelewa vyema mada zilizowasilishwa kwao na wataalam mbalimbali na aliwaasa kuhakikisha wanatekeleza vyema dhamana waliyokabidhiwa ya kuzisimamia Mamlaka za Maji.
“Zingatieni maelekezo ya Katibu Mkuu na mkumbuke mnalojukumu la kuhakikisha Mamlaka mnazoziongoza zinakua mfano bora wa utoaji huduma, mnapaswa kuyaishi mliyojifunza na mtoe uongozi uliotukuka ili wananchi wapate haki yao ya msingi ya kufikishiwa huduma ya majisafi na salama,” alisisitiza Mhandisi Kemikimba.
Kwa upande wa Kanda ya Ziwa, mafunzo hayo yametolewa kwa Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira za Maswa, Shinyanga, Bukoba, Mwanza, Kahama, KASHWASA, Musoma, Bunda, Bariadi, Sengerema, Geita, Muleba, Biharamulo na Mugango-Kyabakari.
Mafunzo mengine ya namna hiyo yanatarajiwa kufanyika Nyanda za Juu Kusini ambayo yatashirikisha Mamlaka za Maji kwenye ukanda huo zikiwemo Mamlaka za Sumbawanga, Mbeya, Njombe, Rukwa na Songwe huku lengo kuu likiwa ni kuongeza uelewa kwa Bodi na Menejimenti kutambua majukumu yao ya kuhakikisha kunakuwa ma huduma bora ya majisafi na usafi wa mazingira.