***************************************
- Vitambulisho Vya Wajasiriamali Wadogo Ni Maono ya JPM Yanayotekelezeka.
Na Lillian Shirima – Habari MAELEZO
Rais John Pombe Magufuli amekuwa ni kiongozi mwenye maono makubwa kwa nchi yetu ya Tanzania, ni kiongozi mwenye fikra za kuleta mageuzi makubwa ya kiuchumi na jasiri kufanya maamuzi mbalimbali ikiwemo kubadilisha mifumo ya utendaji kazi isiyokuwa na tija kwa taifa.
Aidha amefanya jitihada kubwa kushughulikia changamoto za wananchi zikiwemo kero na bughudha walizokuwa wakikutana nazo wajasiriamali wadogo maarufu kwa jina la Wamaachinga na Mama lishe lakini wapo Watanzania wachache wanaobeza jitihada hizo hasa katika kipindi hiki cha uchaguzi.
Akiwa Mkoani Mbeya mwishoni mwa Septemba, katika kampeni za Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28, mwaka huu, Rais John Magufuli alisema, anafahamu kwa lengo la kutafuta kura wapo watu wanaopenyeza maneno ya uongo kuhusu vitambulisho vya wajasiriamali wadogo lakini anaamini wafanyabiashara wengi wadogo wanaelewa umuhimu wa vitambulisho hivyo.
“Mama lishe na wamachinga wanafahamu bughudha walizokuwa wakipata, hata hapa Mbeya ulikuwa ukienda mahali unafukuzwa na mgambo, ukigeuka hivi unafukuzwa, bidhaa zao zinamwagwa, ndio maana tukaanzisha vitambulisho, mtu unalipa shilingi 20,000, lakini unakitumia kwa mwaka mzima na hivi vitambulisho vimekuwa na faida kubwa kwa wananchi wa maisha ya kawaida”. Amesema Rais Magufuli.
Aidha, Rais Magufuli amefafanua kuwa wajasiriamali wadogo wanahitajji kujengewa mazingira mazuri na serikali ili wewe wafanyabiashara wakubwa hivyo ni wajibu wa serikali kuwalinda.
Ili maendeleo yawe na maana lazima yawe na mahusiano na watu pia yamguse mtu mmoja mmoja na kumweka huru. Rais Magufuli amekuwa na maono ya mbali juu ya wajasiriamali wadogo, ameweka utaratibu wenye tija kwa wajasariamali wadogo kuweza kushiriki kwenye uzalishaji na kuchangia pato la taifa.
Disemba, 2018, Rais Magufuli alianzisha utaratibu wa kutoa vitambulisho maalum 670,000 kwa wakuu wa mikoa yote ya Tanzania Bara kwa ajili ya kuwagawia wajasiriamali katika mikoa yao wakiwemo wa machinga na mama lishe na kusisitiza kuwa wafanyabishara hao hawana budi kuchangia shilingi 20,000 kwa kila kimoja ili kurudisha gharama ya utengenezaji wake ambapo fedha zinazopatikana zitatumika kutengeneze vitambulisho vingine.
Vitambulisho hivyo vinatoa fursa kwa wafanyabiashara wadogo wadogo kuendesha shughuli zao mahali popote nchini, kupata mikopo kwenye mabenki na vilevile vinarahisisha upatikanaji wa bima za afya. Kutokana na faida za kuwa na vitambulisho hivyo, Rais Magufuli amewataka wafanyabiashara wadogo wasidanganywe na watu wenye nia ovu kuhusu vitambulisho hivyo.
Upotoshaji wa taarifa au propaganda zinazofanywa wa baadhi wa watu wachache wenye nia ovu ni viashiria vya uchochezi na vinapaswa kukemewa vikali ili kuepusha vurugu na uvunjifu wa amani hususan kipindi hiki cha Uchaguzi Mkuu wa ngazi ya urais, ubunge na udiwani
Aidha, maisha yetu ya kila siku yanatufundisha kuwa baadhi ya watu wana aina ya haiba fulani inayoweza kuwashawishi watu wengine kwa urahisi bila kutarajia hivyo ni muhimu kuelewa haiba sio sawa na uongozi. Uongozi ni karama, si kila mtu anaweza kuwa kiongozi.
Sifa mojawapo ya kiongozi ni kuwa na maono yanayojenga picha inayotekelezeka, kuwa mbunifu wa miradi mbalimbali ya maendeleo ili kuonesha tofauti kati yako na wafuasi wako katika suala zima la kuwajibika na kujituma kwenye majukumu yenye tija kwa maendeleo ya wote.
Rais Magufuli ametengeneza mazingira ya wajasiriamali wadogo kutambua dhana ya uwajibikaji, uaminifu na uzalendo kwa nchi yao. Kitambulisho cha gharama ya shilingi 20,000 ni kadirio la kodi ya mapato kwa mwaka kwa wajasiriamali wadogo ambayo ni rafiki kulingana na kipato chao kwani awali walitozwa ushuru usiopungua shilingi 1,000 kila siku sawa na shilingi 360,000 kwa mwaka.
Licha ya Rais Magufuli kuwapatia wajasiriamali wadogo vitambulisho kwa gharama hiyo ndogo, vitambulisho hivyo pia ni motisha na vijana wengine wengi kushiriki katika masuala ya uchumi na sio kuwaachia wachache walio na ajira rasmi kulipa kodi.
Aidha Rais Magufuli anaiona fursa ya wajasiriamali wadogo kujitegemea kiuchumi na kuondokana na mawazo ya kuajiriwa baada ya kuhitimu masomo badala yake anawajengea uwezo kufanyakazi huru tena kwa mafanikio na hatimaye kuwaajiri vijana wenzao.
Chini ya uongozi wake, serikali imekuwa ikutumia mapato ya ndani ambayo ni fedha zitokanazo na kodi za wananchi kuleta maendeleo. Mathalani, katika suala la afya, Serikali imetumia jumla ya shilingi trilioni 3.1 kugharamia huduma za afya ikiwa ni pamoja na ununuzi dawa na vifaa tiba, ujenzi wa hospitali kubwa, zahanati, vituo vya afya na ukarabati na majengo ya hospitali.
Tangu Serikali ilipoanza kutoa elimu bila malipo kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne imetumia kiasi cha shilingi trilioni 1.2. huku fedha nyingi zinatumika kulipa mishahara ya watumishi wa umma, na kugharamia miradi mingine ya maji, uboreshaji ya sekta ya usafiri na usafirishaji inayochochea ukuaji wa uchumi na ongezeko la ajira kwa Watanzania.
Mbali na miradi ya huduma za kijamii ipo miradi ya mikubwa ya maendeleo inayogharimu kiasi kikubwa cha fedha kama vile ujenzi wa Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere utakaogharimu shilingi trilioni 6.5 na ujenzi wa reli ya treni ya kisasa (SGR) utakaogharimu shilingi trilioni 7.
Hiyo ni baadhi tu ya mifano michache ya huduma za kijamii na miradi ya maendeleo inayohitaji kiasi kikubwa cha fedha.
Rais Magufuli amekuwa akitumia utaratibu mzuri wa kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa kuwashirikisha watu wote wenye uwezo wa kufanya kazi au shughuli zitakazowawezesha kuinua hali zao za maisha hivyo suala la ulipaji wa kodi linabaki kuwa jukumu la kila mmoja wetu kulingana na pato lake iwe kwa mwezi au mwaka, ambapo kodi hiyo inatumika katika kutekeleza baadhi ya miradi..
Maono yake kwa wajasiriamali wadogo na Watanzania kwa ujumla yanatekelezeka, tusikubali kupotoshwa na taarifa zisizo sahihi bali tuunge mkono juhudi zinazofanyika katika kuleta maendeleo ya taifa letu, kwani mchango wa wajasiriamali hawa ni muhimu katika kukuza uchumi ambapo tunashuhudia miradi mingi ikitekelezeka kutokana na pesa za ndani.