************************************
Na.Beatrice Sanga-MAELEZO
Uchaguzi huu wa mwaka 2020 ni wa sita tangu chaguzi za vyama vingi kuanza nchini Tanzania, ukitanguliwa na chaguzi kama hizo za mwaka 1995, 2000, 2005,2010, na 2015.katika chaguzi zote zilizopita CCM iliongoza kwenye nafasi ya urais katika pande zote mbili.
kwa upande waTanzania Benjamin Mkapa alishinda urais wa muungano mwaka 1995 kwa asilimia 61.8, akashinda tena mwaka 2000 kwa asilimia 71.7. Jakaya Kikwete alishinda kwa asilimia 80.28 mwaka 2005 na kushinda tena uchaguzi wa mwaka 2010 kwa asilimia 62.8, mwaka 2015 John Pombe Magufuli alishinda urais wa muungano kwa asilimia 58.46.
Hata hivyo uchaguzi wa mwaka huu unaonekana kuwa na ushindani mkubwa zaidi kwa upande wa urais ambapo wagombea wa urais kupitia vyama mbalimbali vya siasa vikiwemo chama cha mapinduzi (CCM) chama cha demokrasia na maendeleo (CHADEMA), chama cha wananchi CUF, na chama cha Alliance for democratic change(ADC) vimesimamisha wagombea kwa ajili ya kumpata raisi wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania.
Kuelekea uchaguzi mkuu 2020 Tume ya taifa ya uchaguzi NEC yenye jukumu lakusimamia na kuratibu uendeshaji wa uchaguzi wa rais na wabunge kama ilivyoanishwa katika Ibara ya 74(6) ya katiba ya jamhuri wa muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, imekuwa ikitoa miongozo mbalimbali ikiwemo utoaji wa elimu ya mpiga kura yenye lengo la kuhamasisha wananchi kutumia haki yao ya msingi na ya kikatiba ya kujitokeza na kushiriki kuchagua viongozi watakao waongoza katika miaka mitano ijayo.
Aidha sambamba na utoaji wa wa elimu ya mpiga kura tume imekuwa ikitoa miongozo mbalimbali juu ya makosa ya uchaguzi na maadili ya uchaguzi wa rais, wabunge na madiwan, ambayo yanaweza kufanywa na wapiga kura ambao ni wananchi au wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi ambapo miongoni mwa makosa hayo ni kujaribu kupiga kura zaidi ya moja katika uchaguzi, kujaribu kupiga kura kwa kutumia kadi ya mtu mwingine, kujaribu kupiga kura wakati hauruhusiwi kisheria kupiga kura na kuchana orodha ya wapiga kura au mabango yoyote ya elimu kwa mpiga kura yaliyopo vituoni.
Makosa mengine ambayo yameainishwa na NEC ni pamoja na kutoa hongo/takrima, vitendo hivi vinawezapelekea au kusababisha ukosekanaji wa haki hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu ambapo kwa mujibu wa kifungu cha 94 sheria ya taifa ya uchaguzi, sura ya 343 adhabu ya makosa ya utoaji hongo/takrima ni faini isiyopungua shilingi laki moja au kifungo kisichopungua mwaka mmoja na kisichozidi miaka mitatu au vyote kwa pamoja
Kwa mujibu wa kifungu cha 81 cha sheria ya taifa ya ya uchaguzi sura ya 343 na kifungu cha 82 cha sheria ya uchaguzi ya serikari za mitaa sura ya 292 mwenye mamlaka ya kutangaza matokeo ya uchaguzi ni msimamizi au msimamizi msaidizi wa uchaguzi, hivyo basi ni kosa kutoa siri yoyote inayohusu mgombea au mchakato wowote unaoendelea katika kituo cha kupigia kura ili kuhakikisha kuwa utangazaji na utoaji wa taarifa yoyote ya uchaguzi unafanywa na watu waliopewa idhini kwa mujibu wa sheria.
Mtu atakaye kutwa na kosa hili atapata adhabu ya faini isiyopungua shilingi laki moja na isiyozidi laki tatu au kifungo kisichopungua miezi sita na kisichozidi miezi kumi au vyote kwa pamoja hii ni kwa mujibu wa kifungu cha sheria ya taifa ya uchaguzi, sura ya 343.
Wananchi na wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi wanapaswa kuyafahamu na kuyaepuka makosa haya ya uchaguzi ambayo yanaweza kusababisha kupotea kwa haki, kuleta migogoro katika kipindi cha uchaguzi lakini pia kupoteza demokrasia ya nchi yetu hasa katika kipindi hiki ambacho tunaelekea katika uchaguzi mkuu.
Jumapili ya 25 oktoba, watanzania wataelekea katika vituo vya kupigia kura kwa ajili ya kuchagua viongozi wao, wananchi watachagua rais, wabunge, na madiwan watakao watumikia katika miaka mtano ijayo NEC inatakiwa kuendelea kutoa hamasa kwa wananchi ili wajitokeze kwa wingi siku ya kupiga kura na kuchagua viongozi watakao waletea maendeleo katika miaka mitano ijayo.