Katibu Tawala wa Wilaya ya Ilala, Chalangwa Selemani(pili kushoto), Meneja wa NMB Kanda wa Kanda ya Dar es Salaam – Donatus Richard na Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingu Pugu Station,Valentine Mhagama (katikati) wakipiga makofi baada ya makabidhiano ya viti na meza kwa ajili ya Walimu wa Shule ya Pugu Station . Kushoto ni Meneja wa NMB Tawi la Ilala Christine Lifiga na kulia ni Meneja Mwandamizi Mahusiano ya Serikali wa NMB, Mkunde Joseph.
…………………………………………………….
Benki ya NMB, imeendelea kutatua kero katika Sekta za Elimu na Afya, kwa kutoa misaada yenye thamani ya Sh. Milioni 35 katika mikoa mbalimbali nchini, vikiwemo viti 35, meza 35 vyenye thamani ya Sh. Milioni 8 kwa matumizi ya Walimu wa Shule ya Msingi Pugu Station, iliyoko Manispaa ya Ilala.
Akizungumza wakati akikabidhi msaada wa shule ya Msingi Pugu kwa Katibu Tawala (DAS), Ilala, Charangwa Seleman, Meneja wa NMB Kanda ya Dar es Salaam, Donatus Richard alisema changamoto katika sekta za elimu, afya na hata majanga ni kipaumbele cha Benki yake, huku akiishukuru Kamati ya Shule hiyo kwa kuwafikiria wao, walipotafuta ufumbuzi wa uhaba wa viti na meza za walimu.
Kwa upande, DAS Charangwa aliipongeza NMB kwa kuwajibika ipasavyo kwa jamii inayofanya nayo biashara.
Ukiondoa Pugu Station, hapo kabla NMB ilitoa misaada ya vifaa mbalimbali kwenye Sekta ya Elimu na Afya katika Wilaya za Songea mkoani Ruvuma, Mkuranga mkoani Pwani na Kinondoni jijini Dar es salaam vyenye thamani ya Sh. Milioni 27.
Vifaa hivyo vilipokelewa na wakuu wa wilaya hizo mwishoni mwa wiki iliyopita, ambapo katika Wilaya ya Songea, Benki hiyo imetoa viti 50, meza 10 na makabati 10 katika Shule ya Sekondari Madaba, vilivyokabidhiwa kwa Serikali ya Wilaya na Kaimu Meneja wa NMB Kanda ya Kusini – Daniel Zake.
Katika Wilaya ya Mkuranga, benki hiyo imetoa vifaa mbalimbali kwa Shule ya Msingi Mkamba Kizapala na Zahanati ya Kijiji cha Kisemvule vyenye thamani ya Shilingi Milioni 10.
Wakati Shule ya Msingi Mkamba ikipokea mabati 160 kwa ajili kuezekea vyumba vitatu vya madarasa na Ofisi moja ya Walimu, Zahanati ya Kisemvule ilikabidhiwa vitanda 8, magodoro 8, foronya na mashula 25.
Wilayani Kinondoni, Benki hiyo ilikabidhi msaada wa madawati 50 kwa Shule ya Msingi Mbezi Juu, viti na meza zake 20 kwa ajili ya walimu wa Shule ya Sekondari Bunju A, zote za jijini Dar es Salaam, msaada wote ukiwa na thamani ya Shilingi milioni 12.
NMB kupitia Programu ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR), imekuwa na utaratibu wa kurejesha kwa jamii sehemu ya faida, ambako hutenga asilimia moja ya faida yake kwa mwaka kusaidia utatuzi wa changamoto mbalimbali katika Sekta za Elimu, Afya na Majanga kote nchini.