Na John Walter-Babati
Walemavu Wilayani Babati Mkoani Manyara wamepatiwa elimu ya mpiga kura itakayowawezesha kushiriki vyema katika zoezi la kupiga kura Octoba 28 mwaka huu na pia kutambua vipaumbele walivyopewa na tume ya uchaguzi pindi wanapofika katika vituo vya kupigia kura.
Akizungumza na Makundi ya Walemavu Wilayani Babati, Mkurugenzi wa asasi ya Kiraia yaa COSITA, Patrice Gwasma alisema kuwa wameamua kutoa elimu hiyo ili waweze kutumia haki yao ya kikatiba ya kuchagua kiongozi wanayemtaka atakayepigania maslahi yao.
Gwasma alisema kuwa kundi hilo muhimu linahitaji kupata elimu ya mpiga kura na kuhamasishwa umuhimu wa kushiriki katika zoezi la uchaguzi .
“Tume imetoa kipaumbele cha kuwahudumia mapema walemavu aina zote, hii inaonyesha jinsi gani makundi haya yanapata fursa za kupiga kura bila usumbufu huku wakizingatia sharia za uchaguzi” Alisema Mkurugenzi.
Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Walemavu Mkoa wa Manyara (SHIVYAWATA) Joseph Masasi amepongeza asasi hiyo ya kiraia kwa kutimiza wajibu wa kutoa elimu ya Mpiga kura hususan kwa walemavu kundi ambalo limekua likisahaulika mara kwa mara .
Kwa upande wao walemavu waliopata elimu hiyo, wameiomba serikali kuwepo watu wenye uwezo wa kuwaongoza wenye ulemavu wa macho kuweza kuwachagua watu wanaowahitaji.
Aidha wameomba kutengewa mazingira rafiki yatakayowawezesha kupiga kura bila kikwazo.
Aidha Wameishukuru Taasisi ya COSITA kwa kuwawezesha kupata mafunzo hayo kwa kuwa elimu hiyo itawasaidia kutumia haki yao ya kikatiba kuchagua viongozi bora na kuyaomba mashirika mengine kufika vijijini na wilaya za pembezoni ili kuwafikia walemavu wengi zaidi.