**********************************
Na John Walter- Babati.
Mwekezaji wa sekta ya Utalii kutoka Taasisi ya Chemchem iliyopo wilayani Babati mkoa wa Manyara, ametoa basi lenye thamani ya sh 200 milioni kwa Kijiji cha Vilima Vitatu kwa ajili ya kuwasafirisha kila siku wanafunzi wa kijiji hicho kwenda na kurudi katika Shule ya Sekondari ya Kata ya NKaiti ili kupambana na tatizo na Utoro.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa gari hilo kwa viongozi wa kijiji hicho kilichopo ndani ya jumuiya ya uhifadhi wanyamapori ya Burunge mkuu wa wilaya ya Babati Lazaro Twange alimshukuru Mwekezaji huyo kwa kujitolea kusaidia kijiji huku akiwataka wananchi na wanafunzi watakaotumia gari hilo kulitunza ili liweze kudumu.
Mkurugenzi mkuu wa Chemchem Nicolas Francois alimkabidhi funguo za gari hilo Mkuu wa Babati ,Lazaro Twange katika hafla iliyofanyika kijijini hapo Oktoba Mosi mwaka huu.
Francois alisema lengo la msaada huo ni kuboresha elimu katika kijiji hicho kilichopo kata ya Nkaiti kwa kuwapunguzia adha wanafunzi kusafiri umbali wa zaidi ya kilomita 10 kwenda shule na kurudi.
Akizungumzia msaada huo, Mkurugenzi wa Chemchem Nicolas Francois alisema wametoa msaada huo ili kusaidia kukuza elimu katika kijiji hicho hasa kutokana na kuwa na mchango mzuri wa kukuza sekta ya Utalii.
“Msaada huu,kutokana na mapato ya watalii wanaokuja hapa hivyo kama mkiendelea kutunza mazingira,kupambana na ujangili, tutaendelea kupokea watalii na kupata fedha za kuchangia maendeleo” alisema Francois
Francois alisema gari hilo ambalo limenunuliwa nchini Japan hadi kufika katika kijiji hicho na kufanyiwa taratibu zote limegharimu kiasi cha shilingi Milioni 200 na ni gari la pili kutolewa baada ya gari walilolitoa mwaka 2016 kuharibika na kurejeshwa kwao.
Afisa elimu sekondari wilaya ya Babati, Paulina Mpare alisema umbali mrefu ni chanzo cha wanafunzi wengi kukatisha ndoto zao kwa kurubuniwa na wenye vyombo vya moto hususani boda boda.
“Kama Msimamizi wa idara ya Elimu nimekutana na tatizo kubwa la utoro kwa wanafunzi , walikuwa hawafiki shuleni kwa wakati na mara nyingi wakifika wanakuwa wamechoka , hata suala la ufunishaji luilikuwa ni tatizio” alisema Mpare
Alisema kutolewa basi hilo kutasaidia kupunguza vikwazo vilivyokuwa vikiwakuta wanafunzi hao, kuondoa utoro na mimba za Utotoni kwani sasa watasafiri kwa wakati kwenda shule na kurejea majumbani.
Afisa maendeleo wa taasisi ya Chemchem Walter Pallangyo alisema licha ya kutoa gari, Taasisi ya Chem chem itakuwa ikilifanyia matengenezo pamoja na kumlipa mshahara dereva huku kijiji kikichangia mafuta pekee.
Mwenyekiti wa kijiji cha vilima vitatu Abubakary Msuya alipongeza msaada huo na kuahidi kusimamia gari hilo na kuhimiza wananchi kulitunza basi hilo na kuchangia mafuta.