Mgombea uwakilishi wa Jimbo la Konde kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi-CCM-Zawadi Amour Nassor akiomba kura kwa wananchi wa shehia ya Tondooni akiwa katika mkutano wake wa Kampeni kuomba ridhaa ya wananchi.
*******************************
Na Masanja Mabula ,Pemba.
“MLIPUKO wa ugonjwa wa COVID 19 nusura ufifishe ndoto yangu ya kugombea nafasi ya uwakilishi , lakini nilipiga moyo konde na kuchukua fomu , nashukuru wanachama na chama kuniamini na kuniteuwa kupeperusha bendera ya chama kuwania nafasi hiyo”
Ni maneno yake Mgombea wa nafasi ya uwakilishi jimbo la Konde kupitia Chama Cha Mapinduzi –CCM-Zawadi Amour Nassor aliyoyasema wakati akizungumza na makala haya.
Katika mazungumzo yake Bi Zawadi ambaye kitaaluma ni Mwalimu alisema awali virusi vya CORONA vilitaka kuwa kikwazo katika kufikia malengo yake kukabiliana na mfumo dume.
Alisema alichokibaini baada ya kuingia kwenye kinyanganyiro hicho ni kuwepo na baadhi ya wanaume wenye mawazo mgando kana kwamba nafasi hizo wamejimilikisha na kuamini kuwa ni mali yao.
“Kama sio ujasiri basi nisingeweza kujitokeza kushindana na wanaume kuwania nafasi hii,kwani hata mlipuko wa Ugonjwa wa COVID 19 nao ukitaka kuwa sababu ya kukwamisha malengo yangu”alisema.
“Ama kweli msemo wa kwamba ukitaka kujua uhondo wa ngoma ingia ucheze, nimeingia na nimeona kwamba mfumo dume umejengwa na baadhi ya wanaume kwa lengo la kuwakandamiza wanawake”alifahamisha.
Mgombea huo ambaye ni mwanaharakati anayetetea haki za watoto na kupinga masuala ya udhalilishaji alisema moto aliousha wa kupambana na matendo hayo kamwe hautazima badala yake atauendeleza ili kukomesha matendo hayo.
Akiwa msaidizi Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Konde Msingi, Bi Zawadi alifanikiwa kuibua vitendo vya udhalilishaji waliokuwa wakifanyiwa wanafunzi wa kike skuli hiyo na ambapo baadhi ya watuhumiwa walifikishwa mahakamani.
Alipoulizwa na mwandishi wa makala haya kwamba ujasiri wa kushindana na wanaume aliupata wapi, Zawadi alisema ni kutokana na uwezeshaji unaotolewa na Chama wa Waandishi wa Habari wanawake TAMWA.
Bi Zawadi alisema kama kungekuwapo na taasisi nyengine zenye kufanya kazi kwa malengo sawa na TAMWA wanawake wa Pemba wangekuwa wamekombolewa kwa kutoka kwenye wimbi la mfumo dume
“Nimeshiriki vikao tofauti vinavyoratibiwa na TAMWA, kwa kweli walinijengea uwezo na uthubutu wa kuwania nafasi kupitia Jimbo kwani walitutaka tuondoe dhana ya kwamba ‘MWANAMKE AKIWEZESHWA ANAWEZA’kumbe bila ya kuwezeshwa tunaweza”alieleza.
Akiwa katika mkutano wa Kampeni shehia ya Tondooni Mgombea huyo alisema amekuwa mwanaharakati anayepinga matendo ya udhalilishaji , hivyo anafahamu changamoto zinazowakabili wanawake na iwapo atachagulia atazipatia ufumbuzi.
Alisema kuteuliwa kwake na Chama cha Mapinduzi kugombea nafasi hiyo ya uwakilishi, akinamama wanatakiwa kujawa na matumiani kwamba saa ya ukombozi wao imefika.
“Nakuja kumaliza changamoto za wanawake , nimekuja kuwapa matumaini kwamba saa za ukombozi wenu ndizo hizi zimetimia , nawaomba kura zenu za ndio”alisema.
HISTORIA YAKE KISIASA.
Zawadi alianza kujihusisha na siasa tangu akiwa mwanafunzi wa sekondari katika skuli ya Utaani lakini alishindwa kujitokeza kutokana na kwamba alikuwa bado mwanafunzi.
Alisema kwa wakati huo , wanafunzi wengi waligoma kuendelea na masomo hali iliyomlazimu kuhama kutoka skuli ya Konde na kuhamia Skuli ya Utaani Wete.
AHADI ZAKE KWA WAJASIRIAMALI HUSUSANI WANAWAKE
Akiwa kwenye mkutano wa Kampeni Zawadi anatoa ahadi ya kuboresha maisha ya wajasiriamali wanawake kwa kuwapatia elimu ya vitendo pamoja na kuangalia zaidi fursa ya mikopo kutoka taasisi za kibenki.
“Zipo fursa nyingi kutoka taasisi za kibenki, hivyo nitahakikisha fursa hiyo inawafikia na wote mnanufaika jambo ambalo litasaidia kukuza mitahi yenu”alieleza.
Sekta ya elimu.
Zawadi Amour Nassor , alisema akiwa mwakilishi wa Jimbo hilo ataanzisha mfuko maalumu wa kusaidia wanafunzi wanashindwa kujiunga na elimu ya juu kutokana na changamoto ya mikopo.
Anasema mfuko huo utaundiwa kamati ya wataalamu ambayo itakuwa na jukumu la kupokea maombi kutoka kwa wanafunzi au wazazi wao na kuyapitia kabla ya kutoa maamuzi.
“Huu utakuwa ni mfuko wenu wananchi, nyie wenyewe mtaunda kamati ambayo itakuwa na jukumu la kupitia maombi yanayowasilishwa kabla ya kutoa maamuzi”alisema.
Sekta ya Michezo.
Mgombea huyo alisema akiwa mwakilishi wa Jimbo la Konde ataanzisha mashindano ya mpira wa miguu na mikono ambayo yatajulikana kama ‘MWAKILISHI CUP’haya pia yatakuwa na kamati yake inayojitegemea.
Anaeleza kwamba kamati hiyo itatunga sheria zake wenyewe na itawashirikisha pia viongozi kutoka shirikisho la Mpira wa miguu Wilaya ya Micheweni –ZFF-ili yatambulike kisheria.
“Natambua kwamba watu wengi wanapenda mpira wa miguu, hata sisi akinamama tunapenda pia , lakini nataka kuuendeleza na mpira wa mikono ili uweze kusaidia kutoa ajira kwa vijana”alisisitiza.
Baadhi ya wananchi wanamzunguzia Bi Zawadi kama ni lulu iliyokuwa imejificha na kwa sasa TAMWA wameiibua na inatarajia kuwa ni mkombozi na shujaa ya maendeleo.
Sheha wa shehia ya Msuka Magharibi Maraim Khatib akizungumza na makala haya juu ya Mgombea huyo alisema anamatumiani makubwa ya jimbo hilo kubadilika kimaendeleo kutokana na uwezo alionao Bi Zawadi.
Naye Halima Othman Idd mjasiriamali anayejishughulisha na utengenezaji wa sabuni za maji kwa kutumia malighafi za ndani anasema kutokana na ujasiri alioonyesha Bi Zawadi wa kugombea pamoja na wanaume ndani ya chama ni ishara kwamba wanawake wamejenga uthubutu.
“Wajasiriamali katuahidi mengi na sisi tunamuunga mkono , kwani nani aliyekuwa hataki afanikiwe na huyu ameonyesha nia ya kutuwezesha kielimu na kitaalumu nitampigia kura”alisema.
Akitaja sifa za Mgombea huyo, mmoja wa walimu aliyejitambulisha kwa jina moja na Masoud alisema ni miongoni wa wanafunzi wake wenye msimamo na wanaojiamini na anayeheshimu maamuzi yake.
“Nimesomesha wanafunzi wengi, lakini kwa huyu najivunia kwani anasimamo na hayumbishwi pia anapenda kusimamia haki, kwa kweli Jimbo la Konde wamepata mtu atakaye wavusha hadi kwenye sayari ya maendeleo, mimi sina shaka naye”alifahamisha.
Mratibu wa Chama cha waandishi wa habari wanawake TAMWA-Ofisi ya Pemba , Fat-hiya Mussa Said akizungumza na baadhi ya wanawake wajasiriamali katika Ofisi za Kilimo Weni anatumia fursa hiyo kuwataka wanawake kuwaunga mkono wanawake walioteuliwa na vyama vyao kugomnea nafasi za uongozi katika uchaguzi mkuu.
Alisema wanawake wengi huwa ni kampeni meneja wa wanaume na wakashinda , iweje sasa washindwe kuwapigia kampeni wanawake wenzao ili washinde uchaguzi kinazingatiwa ni uwamuzi tu.
“Wapo wanawake huwa ni makampeni meneja wa wanaume na wanashinda , iweje sasa mbinu hizo zikatumika kuwafanyia kampeni wagombea wanawake, hili linawezekana”alisema.
Akizungumza na vyombo vya habari katika makao makuu wa Ofisi ya TAMWA Mkoroshoni Chake Chake Pemba , Afisa Miradi wa TAMWA Pemba Asha Musaa Omar aliwataka kutumia vyema kalamu zao na taaluma yao kuwaelimisha wanawake wanaochaguliwa kuingia kwenye vyombo vya kutunga kufuata maadili ya mzanzibari.
“Baadhi ya wanawake wanapopata uongozi huvaa nguo zisizoendana na maadili, hivyo naomba sana waandishi wa habari kuwaelimisha na kuwahamisha kufuata maadili ya silka ya mzanzibari”alisisitiza.
Uchaguzi Mkuu unatarajia kufanyika tarehe 28/10/2020 ambapo wananchi wa Zanzibar watapata fursa ya kuwachagua viongozi mbali mbali akiwemo Rais wa Jamuhuri ya Muungano, Rais wa Zanzibar, Wabunge , Wawakilishi pamoja na Madiwani.